Tafuta

Vatican News
Papa Francisko pamoja na waandamizi wake kuanzia tarehe 10-15 Machi 2019 watakuwa na mafungo ya kiroho huko Ariccia, nje kidogo ya Roma! Papa Francisko pamoja na waandamizi wake kuanzia tarehe 10-15 Machi 2019 watakuwa na mafungo ya kiroho huko Ariccia, nje kidogo ya Roma! 

Papa na waandamizi wake: Mafungo ya Kwaresima: 2019

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia tarehe 10-15 Machi 2019, watasitisha shughuli zote za kitume na kwenda “kujichimbia Mlimani”, kwenye nyumba ya mafungo ya “Divin Maestro” huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma, ili kujipatia muda wa kusali na kutafakari, tayari kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka 2019 unaoongozwa na kauli mbiu “Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu” anasema, Kwaresima ya Mwana wa Mungu ni mchakato wa kuingia katika Jangwa la Kazi ya Uumbaji. Lengo ni kurejesha tena mazingira kuwa ni Bustani ya umoja na Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kabla ya dhambi ya asili. Kwaresima kiwe ni kipindi cha kupandikiza matumaini ya Kristo hata katika kazi ya uumbaji, kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru na utukufu wa watoto wa Mungu.

Kwaresima ni kipindi kilichokubalika, waamini wakitumie kikamilifu, kwa kutubu na kumwongokea Mungu. Ni wakati muafaka wa kuachana na ubinafsi, uchoyo na kuanza kujielekeza zaidi kwa ajili ya huduma, ustawi na maendeleo ya jirani wanaoteseka, ili kushirikishana tunu za maisha ya kiroho na kimwili. Kwa njia hii, waamini wataweza kuupokea ushindi wa Kristo Mfufuka katika maisha yao kwa kushinda dhambi na kifo na kuanza mchakato wa kutumia nguvu, hii kuleta mabadiliko katika kazi ya uumbaji.

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia tarehe 10-15 Machi 2019, watasitisha shughuli zote za kitume na kwenda “kujichimbia Mlimani”, kwenye nyumba ya mafungo ya “Divin Maestro” huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma, ili kujipatia muda wa kusali na kutafakari, tayari kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Ni muda wa kwenda jangwani ili kujichotea nguvu za maisha ya kiroho, tayari kupambana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuliandama Kanisa na jamii katika ujumla wake! Mafungo haya yataongozwa na Abate Bernardo Francesco Maria Gianni kutoka Abasia ya “San Miniato al Monte”.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, mafungo haya yatapambwa kwa namna ya pekee na: Ibada ya Misa Takatifu, Tafakari, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na Masifu. Tema inayoongoza tafakari hizi kutoka kwa Abate Bernardo Francesco Maria Gianni ni “Mji wenye tamaa kali. Kwa ajili ya mwono na alama za Kipasaka Ulimwenguni”. Hii ni sehemu ya Shairi lililotungwa na Mario Luzi, mwezi Desemba 1997. Kila siku itaongozwa na tema maalum!

Kwa ufupi, Abate Bernardo Francesco Maria Gianni kutoka Abasia ya “San Miniato al Monte” alizaliwa huko Prato kunako mwaka 1968. Mwaka 2009 akachaguliwa kuwa Mkuu wa Abasia ya “San Miniato” na mwaka 2015 akachaguliwa kuwa Abate. Abate Bernardo alikuwa ni mjumbe wa Kikosi Kazi cha maandalizi ya Kongamano la Kanisa la Italia Kitaifa lililoadhimishwa Novemba 2015 na Baba Mtakatifu Francisko akashiriki kikamilifu!

Papa: Mafungo ya Kwaresima
28 February 2019, 08:01