Cerca

Vatican News
Papa Francisko ametuma salam za rambi rambi kutokana na shambulizi la kigaidi lilikotokea Jijini Nairobi, nchini Kenya. Papa Francisko ametuma salam za rambi rambi kutokana na shambulizi la kigaidi lililotokea Jijini Nairobi, nchini Kenya.  (AFP or licensors)

Papa Francisko atuma salam za rambi rambi nchini Kenya

Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, anawaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na shambulizi hili na anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Baba Mtakatifu anaiombea familia ya Mungu nchini Kenya nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya shambulizi la kigaidi lililotokea katika hoteli ya DusitD2 eneo la 14 Riverside Drive, Jijini Nairobi siku ya Jumanne, tarehe 15 Januari 2019 na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa na wengine kupoteza maisha. Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, anawaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na shambulizi hili na anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Baba Mtakatifu anaiombea familia ya Mungu nchini Kenya nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu!

Taarifa zaidi kutoka Nairobi zinabainisha kwamba, watu waliofariki dunia kutokana na shambulio hili wamefikia watu 21. Katika idadi hii, wameongezeka pia magaidi watano waliouwawa na vikosi vya ulinzi na usalama nchini Kenya katika mapambano ya risasi. Itakumbukwa kwamba, hata Baraza la Makanisa Ulimwenguni limetuma pia salam za rambi rambi kwa familia ya Mungu nchini Kenya pamoja na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano. 

Papa: Kenya
17 January 2019, 14:48