Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Papa Francisko kwa Vijana wanaoshiriki Siku ya Vijana Wazawa Amerika ya Kusini. Utamaduni wao! Ujumbe wa Papa Francisko kwa Vijana wanaoshiriki Siku ya Vijana Wazawa Amerika ya Kusini. Utamaduni wao! 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa vijana wazawa Amerika ya Kusini

Papa Francisko anawahamasisha Vijana kutoa shuhuda za tamaduni za Makanisa yao mahalia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kwani lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linasimama kidete kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima Kanisa nikijielekeza katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika usawa na utu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wazawa wa Amerika ya Kusini kuhakikisha kwamba wanagundua mizizi ya asili na utamaduni wao, tayari kutoka kifua mbele kupambana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Anasema, baada ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, huko Cracovia, Poland, mwaka 2016 aliwataka vijana waliokuwa wanajitolea katika huduma mbali mbali kujibidisha kufanya kumbu kumbu ya historia ya maisha yao ya nyuma, ili kujenga matumaini kwa mambo ya mbeleni kwa ujasiri na uthubutu mkubwa!

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Wazawa Amerika ya Kusini iliyozinduliwa Alhamisi, tarehe 17 Januari 2019 huko Soloy, nchini Panama. Maadhimisho haya yanahitimishwa rasmi Jumatatu, tarehe 21 Januari 2019. Mkutano huu ni utangulizi wa Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano, tunza na maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria anaendelea kufanya hija pamoja na waamini kwa kuwaongoza vijana wa kizazi kipya, ili waweze kukita maisha yao katika imani, udugu na mapendo.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, kwa vijana wazawa kutoka Amerika ya Kusini anapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kuandaa na hatimaye, kushiriki katika maadhimisho haya yanayofanyika kwa mara ya kwanza katika ngazi ya kimataifa. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu analipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Panama kwa kushirikiana vyema na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM ili kufanikisha tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana mahalia! Hii iwe ni nafasi ya kuadhimisha, kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kwa kuendelea pia kujikita katika utajiri na amana ya tamaduni asilia.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni fursa ya kuwashukuru wahenga wao kwa urithi wa historia na ujasiri wa kuisongesha mbele, licha ya changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo. Hii inaonesha kwamba, upo uwezekano mkubwa wa kujenga ulimwengu mpya kwa kufanya rejea kwenye mapokeo na tamaduni njema zilizopita. Vijana wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanajibidisha zaidi kutunza mizizi ya urithi wa tadamuni zao, ili hatimaye, waweze kukua, kuchanua na kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Vijana wanahamasishwa kutoa ushuhuda wa tamaduni za Makanisa yao mahalia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kwani lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linasimama kidete kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima Kanisa nikijielekeza katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika usawa na utu. Tema mbali mbali ambazo zimekuwa zinajadiliwa katika maadhimisho haya zimekua ni chachu kwa vijana kutafuta majibu muafaka mintarafu mwanga wa Injili, ikizingatiwa kwamba, katika ulimwengu mamboleo, kuna kashfa ya utengano; maskini na baadhi ya watu kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, waathirika wakuu ni vijana na hasa zaidi vijana wazawa. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa na utambuzi makini kwamba, wao ni sehemu ya watu wao, mwaliko ni kusimama kidete kupinga utamaduni usiojali wala kuthamini utu na heshima ya wengine. Vijana wathubutu kuzamisha mizizi ya tamaduni zao katika maisha, huku wakiwa na matumaini kwa maisha ya mbeleni yenye msingi thabiti!

Vijana wapende na kuheshimu mila, desturi na tamaduni zao njema, ili waweze kukua, kukomaa na kuchanua kama mitende ya Lebanoni! Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kusema, hii ndiyo changamoto pevu iliyoko mbele ya vijana wazawa huko Amerika ya Kusini. Ni matumaini yake kwamba, “atakapotinga timu Panama” kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, ataweza kukutana na kuzungumza nao mubashara! Lakini kwa sasa anawatakia mafanikio mema katika maadhimisho haya na mwishowe, anapenda kuwapatia baraka zake za kitume.

Papa: Vijana Panama 2019
19 January 2019, 11:45