Cerca

Vatican News
Papa Francisko wakati akirejea kutoka Panama amewatumia salam na matashi mema viongozi katika nchi ambamo amepitia! Papa Francisko wakati akirejea kutoka Panama amewatumia salam na matashi mema viongozi katika nchi ambamo amepitia!  (AFP or licensors)

Siku ya Vijana Duniani 2019: Salam na matashi mema!

Baba Mtakatifu kwanza kabisa amemshukuru Rais wa Panama na watu wake, kwa ukarimu waliomwonjesha na kwamba, anaendelea kuwaombea amani, utulivu, ustawi na maendeleo fungamani. Kwa viongozi wengine wa nchi amewaombea: neema, amani, afya njema na ustawi. Amewatakia pia usalama na furaha tele katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 28 Januari 2019 amewasili mjini Vatican baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume nchini Panama ambako ameshiriki katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani. Mara baada ya kuwasili, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, lililoko mjini Roma ili kutoa shukrani zake kwa Bikira Maria, Afya ya Warumi kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani! Falsafa ya kushukuru ni kuomba tena!

Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea mjini Vatican, amebahatika kutuma salam na matashi mema kwa wakuu wa nchi za: Panama, Colombia, Jamhuri ya Watu wa Dominican, Uholanzi, Marekani, Ureno, Ufaransa na hatimaye Italia. Kwa viongozi wote hawa pamoja na wananchi wao, Baba Mtakatifu kwanza kabisa amemshukuru Rais wa Panama na watu wake, kwa ukarimu waliomwonjesha na kwamba, anaendelea kuwaombea amani, utulivu, ustawi na maendeleo fungamani. Kwa viongozi wengine wa nchi amewaombea: neema, amani, afya njema na ustawi. Amewatakia pia usalama na furaha tele katika maisha yao!

Baba Mtakatifu alipowasili kwenye anga la Italia, amemtumia salam na matashi mema Rais Sergio Mattarella wa Italia, akimtaarifu kwamba, amerejea kutoka nchini Panama. Baba Mtakatifu anasema, nchini Panama, amekutana na vijana jasiri, wenye ari na moyo mkuu wanaotaka kujikita katika leo na kesho inayofumbata amani na udugu; kwa kuendelea kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo! Anapenda kumhakikishia Rais Mattarella na familia ya Mungu nchini Italia katika ujumla wake, sala zake za daima.

Papa: Matashi mema

 

 

29 January 2019, 14:13