Cerca

Vatican News
Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Mwandishi wa Habari Alexei Bukalov kutoka Urussi kilichotokea tarehe 28 Desemba 2018. Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Mwandishi wa Habari Alexei Bukalov kutoka Urussi kilichotokea tarehe 28 Desemba 2018.  (ANSA)

Papa Francisko asikitishwa na kifo cha mwandishi wa habari!

Baba Mtakatifu amemkumbuka Alexei Bukalov, aliyekuwa mwandishi wa habari wa TASS kutoka Urussi, gwiji la hija za kipapa, aliyefariki dunia tarehe 28 Desemba 2018 akiwa na umri wa miaka 78. Amefuatana na Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na mara ya mwisho alikuwa kwenye hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea Panama kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, Jumatano tarehe 23 Januari 2019, amepata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amemkumbuka Alexei Bukalov, aliyekuwa mwandishi wa habari wa TASS kutoka Urussi, gwiji la hija za kipapa, aliyefariki dunia tarehe 28 Desemba 2018 akiwa na umri wa miaka 78. Amefuatana na Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na mara ya mwisho alikuwa kwenye hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko.

Kimsingi Marehemu Alexei Bukalov, alikuwa ni mtu wa watu, mcheshi na mchapakazi, aliyefanikiwa kwa taaluma yake, kuelezea matukio mbali mbali ya Kanisa kwa wasikilizaji na wasomaji wake nchini Urussi. Baba Mtakatifu, kwa masikitiko makubwa amesema, kwa mara ya kwanza, katika ndege hii, anakosekana Bwana Alexei Bukalov, aliyempenda na kumheshimu sana kutokana na kazi yake. Alikuwa ni mtu mwenye utu na wala hakuogopa kukutana na kuzungumza na jirani zake; kwa hakika alikuwa ni mtu mwenye maneno machache na aliyebahatika kuifahamu vyema diplomasia ya Vatican.

Baba Mtakatifu amewaomba wale wote waliokuwa kwenye msafara wake, kukaa kimya kwa kitambo kidogo, ili kumkumbuka na kumwombea Marehemu Alexei Bukalov na hatimaye, akahitimisha kwa sala ya Baba Yetu. Waandishi wa habari, wamempongeza Baba Mtakatifu kwa kitendo hiki cha kiungwana! Mwishoni, amewatakia wote kazi njema ya kuwahabarisha watu matukio muhimu yanayojiri katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019.

Kabla ya Baba Mtakatifu kuzungumza na waandishi wa habari, Monsinyo Maurizio Rueda Beltz, Mratibu wa Hija za Kipapa, amemtambulisha kwa mara ya kwanza Dr. Alesandro Gisotti, Msemaji mkuu wa muda wa Vatican ambaye anashiriki kwa mara ya kwanza katika tukio hili tangu alipoteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko.

Papa: Waandishi wa habari
23 January 2019, 13:46