Tafuta

Vatican News
Papa Francisko azindua rasmi Mwaka wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa, Rota Romana. Papa Francisko azindua rasmi Mwaka wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa, Rota Romana.  (Vatican Media)

Papa Francisko azindua Mwaka wa Mahakama ya Rota Romana!

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amekazia: umoja na uaminifu; mpango mkakati wa utume wa maisha ya ndoa na familia; umoja, ukarimu na upendo aminifu kwa watu wa ndoa, kwani Kanisa linataka kujielekeza zaidi kwa ajili ya kudumisha imani, afya na ustawi wa watu wa ndoa na familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa “Rota Romana”, imezindua rasmi Mwaka wa Mahakama 2019 kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 29 Januari 2019. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia: umoja na uaminifu; mpango mkakati wa utume wa maisha ya ndoa na familia; umoja, ukarimu na upendo aminifu kwa watu wa ndoa, kwani Kanisa linataka kujielekeza zaidi kwa ajili ya kudumisha imani, afya na ustawi wa watu wa ndoa na familia!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, ulimwengu mamboleo kwa sasa hautengenezi mazingira yatakayowasaidia waamini kukuza na kudumisha imani, kiasi kwamba, inawawia vigumu kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili mintarafu Sakramenti ya Ndoa. Ni wajibu wa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anajibidisha kikamilifu katika shughuli za kichungaji, kwa kutoa msaada wa mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na wanandoa na familia. Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa inatekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia taalimungu na Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa kuhusu Sakramenti ya Ndoa, ili kukuza na kudumisha umoja na uaminifu, mambo msingi katika maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa Katoliki.

Watu wa ndoa wanapaswa kuwa mashuhuda wa ufunuo wa imani katika Sakramenti ya Ubatizo! Hii ni dhamana nyeti na fungamani, ili kukuza na kudumisha amani, heshima pamoja na kushirikishana utajiri wa kiutu, kimaadili na maisha ya kiroho. Kwa njia hii, mwanaume na mwanamke wanakuwa sasa si wawili tena, bali mwili mmoja, hadi pale kifo kitakapowatenganisha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, umoja na uaminifu ni nguzo msingi kwa wanandoa na katika kukuza na kudumisha uhusiano na mafungamano binafsi na yale ya kijamii. Pale mambo yanapokwenda kinyume na wanandoa kukimbilia kwenye Mahakama za kiraia, kwa kawaida ahadi zinazotolewa haziheshimiwi kutokana na ukosefu wa uaminifu katika dhamana waliojitwalia.

Umoja na uaminifu ni tunu ambazo zinapaswa kuchambuliwa kwa umakini zaidi kwa wanandoa watarajiwa, kama sehemu ya mpango mkakati wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Maaskofu pamoja na mapadre, wanaowasindikiza wanandoa katika hatua mbali mbali za majiundo na maendeleo yao. Baba Mtakatifu anakazia kwanza kabisa: umuhimu wa majiundo ya awali, kabla ya kufunga ndoa na majiundo endelevu, kwa kuhakikisha kwamba, wanandoa wanapata malezi na majiundo makini ili kutambua na kuambata tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, dhamana na majukumu wanayojitwalia kwa kufunga ndoa Kanisani!

Maaskofu na Mapadre watambue kwamba, kutokana na dhamana na utume wao wa shughuli za kichungaji, kadiri ya maeneo yao, wanapaswa kuwashirikisha wanajumuiya kutoka katika Jumuiya za Kikanisa chini ya uongozi wa Askofu mahalia na paroko husika. Lengo ni kujenga na kudumisha umoja na uwajibikaji, unaowashirikisha waamini, ili kweli Sakramenti ya Ndoa iliweze kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa kuwasindikiza hatua kwa hatua katika malezi na majiundo yake: kiroho na kimwili! Paulo Mtume, alikuwa na wasaidizi katika utekelezaji wa dhamana na utume wake wa kimisionari.

Wasaidizi hawa walikuwa ni zawadi ya Roho Mtakatifu inayoendelea kutolewa hata kwa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Kumbe, ni wajibu wa wakleri kutambua na kuthamini karama za wanandoa, imani na utume wao ndani ya Kanisa kama walivyokuwa akina Aquila na Priscilla. Wanandoa wanapaswa kusaidiwa ili kuzamisha maisha yao katika Maandiko Matakatifu, hususan “Lectio Divina”, Katekesi endelevu; Ushiriki mkamilifu katika Sakramenti za Kanisa, na hasa zaidi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu pamoja na ushauri wa maisha ya kiroho. Wanafamilia wasaidiwe kujiunga na utume wa familia na katika mashirika na vyama vya kitume, ili waendelee kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Baba Mtakatifu anawataka wanandoa kuhakikisha kwamba, wanadumisha umoja, ukarimu na upendo aminifu, kwa kusaidiana; kwa kuombeana na kutakatifuzana; ili kuwa kweli ni mashuhuda wa Jumuiya za Kikanisa; Injili wazi, inayotangazwa kila kukicha. Inasikitisha kuona kwamba, wanandoa wanaoishi kwa pamoja kwa miaka mingi si sehemu ya habari zinazochukua uzito wa juu katika vyombo vya mawasiliano! Lakini pale, kashfa ndani ya ndoa inapojitokeza, wengi wanakimbilia kuandika na kuzipatia uzito wa juu kabisa!

Wanandoa wanaoishi katika umoja na uaminifu ni mashuhuda wazuri wa watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kwa hakika, uaminifu ni jambo linalowezekana kama ilivyo hata kwa maisha ya Daraja Takatifu, dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa kikamilifu na Maaskofu pamoja na Mapadre wao kama ilivyokuwa kwa Aquila na Priscilla kwa Paulo Mtume na Apollo.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wadau wote wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa “Rota Romana” kwa utume wao kwa ajili ya ustawi wa watu wa Mungu, kwa kuendeleza haki kwa njia ya hukumu wanazotoa kwa kuzingatia haki msingi za Sakramenti ya Ndoa. Haki hizi ni kwa ajili ya huduma ya roho na imani ya wanandoa. Hukumu zinazotolewa hazina budi kujikita katika Mafundisho ya Kanisa kwa kutambua dhana ya ndoa, haki na wajibu kama zinavyofafanuliwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Kisakramenti.

Rota Romana 2019
29 January 2019, 14:46