Tafuta

Vatican News
Papa Francisko tarehe 7 Julai 2019 amekutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican. Papa Francisko tarehe 7 Julai 2019 amekutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican.  (ANSA)

HOTUBA YA PAPA FRANCISKO KWA MABALOZI 2019

Khalifa wa Mtakatifu Petro anatumwa kutekeleza dhamana yake kama sehemu ya utii wa Kristo Yesu aliyemtaka Mtakatifu Petro kuwalisha kondoo wake! Ndiyo maana Vatican na Kanisa katika ujumla wake, linaguswa sana na uchungu, fadhaa mahitaji ya familia ya binadamu: kiroho na kimwili, kwa kuendelea kuwa sikivu kwa mahangaiko yanayomsibu mwanadamu ulimwenguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 7 Januari 2019 amekutana na kuzungumza na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kama sehemu ya mapokeo na utaratibu wa kutakiana heri kwa mwaka mpya wa 2019. Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Mikataba mbali mbali ambayo Vatican imetiliana sahihi na Nchi pamoja na Mashirika ya Kimataifa kama vile UNESCO ambayo kwa mwaka 2019 inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Amegusia hija za kitume alizotekeleza katika kipindi cha mwaka 2018 na zile anazotarajia kuzifanya kwa Mwaka 2019 kama sehemu ya mbinu mkakati wa kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kidiplomasia.

Baba Mtakatifu amefafanua umuhimu wa kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa kama matokeo ya Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia, ili kutafuta suluhu ya amani kwa pamoja. Amekazia umuhimu wa kudumisha haki na wajibu na kwamba, siasa safi ni chombo cha huduma ya amani duniani. Kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Haki Msingi za Binadamu litolewe ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwalinda na kuwatetea wanyonge; kwa kuwa ni sauti kwa wale wasiokuwa na sauti hasa wakimbizi na wahamiaji duniani, daima: utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza.

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa kwa Mwaka 2019 inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 30 ya Tamko la Haki ya Mtoto Duniani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za watoto; utu na heshima yao kama binadamu. Watoto wajengewe mazingira mazuri ya maisha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho na kimwili. Kanisa pia linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa “Mulieris dignitatem” yaani “Utu na wito wa wanamke”. Amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni jukwaa na wajenzi wa amani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Jumuiya ya Kimataifa.

Papa Francisko amegusia juu ya Mkutano 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP 24 uliohitimishwa hivi karibuni huko Katowice, Poland; Kuanguka kwa Ukuta wa Berlini kunako mwaka 1989 pamoja na Mkataba wa Laterani ambao mwaka huu, unatimiza miaka 90 tangu ulipotiwa sahihi na huo ukawa ni mwanzo wa Nchi ya huru ya Vatican.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amesema, Khalifa wa Mtakatifu Petro anatumwa kutekeleza dhamana yake kama sehemu ya utii kwa Kristo Yesu aliyemtaka Mtakatifu Petro kuwalisha kondoo wake! Ndiyo maana Vatican na Kanisa katika ujumla wake, linaguswa sana na uchungu, fadhaa na mahitaji ya familia ya binadamu: kiroho na kimwili, kwa kuendelea kuwa sikivu kwa mahangaiko yanayomsibu mwanadamu katika ulimwengu mamboleo na kwamba, Kanisa linataka kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa kila binadamu. Si lengo la Kanisa kutaka kuingilia mambo ya ndani ya nchi husika. Ametaja kwamba, Vatican na Nchi ya Benin, pamoja na San Marino wameridhia kwa pamoja mkataba wa ushirikiano na Kanisa ili kutoa fursa ya kufundisha dini shuleni.

Vatican pia imeridhia Mkataba na  Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO kuhusu umuhimu wa utamaduni kama chombo cha kujenga na kudumisha amani na maridhiano kati ya watu, hasa mwaka huu UNESCO inapoadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Ushirikiano huu unapania kujenga na kudumisha haki msingi za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria Barani Ulaya. Vatican pia imejiunga na malipo ya huduma kwa kutumia Euro. Papa amegusia hija za kitume alizofanya nchini Chile, Perù, Sweden, Ireland, Lithuania, Latvia na Estonia. Ziara zote hizi zinalenga kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano.

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa Nicaragua kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini humo! Uhusiano kati ya Vatican na Vietnam unaendelea kuimarisha na kwamba, hivi punde Vatican itakuwa na Balozi wake wa kudumu nchini humo, kielelezo cha umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa mahalia. Vatican inaendelea pia kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na China baada ya kuwekeana sahihi mkataba wa muda kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia; sanjari na kuendelea na upatanisho, ili kukuza ari na mwamko wa uinjilishaji mpya na kwamba, kwa mara ya kwanza katika historia, Maaskofu wote nchini China wana umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, hali inayopania pia kuimarisha uhuru wa kidini.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mkataba wa Versailles uliotiwa sahihi kunako mwaka 1919 ulipania kusitisha Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, na huo ukawa mwanzo wa mchakato wa kuundwa kwa Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1945, ingawa hata leo hii bado kuna vita, migogoro na kinzani, lakini Umoja wa Mataifa umekuwa ni mahali pa kuyakutanisha mataifa ili kutafuta suluhu ya amani katika misingi ya ukweli na uwazi, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Umoja wa Mataifa. Kuna vita ambavyo vimesahaulika; kuna mataifa na Mashirika ya Kimataifa ambayo yamejitwalia madaraka kiasi hata cha kutaka kupandikiza ukoloni wa kiitikadi kama sehemu ya utandawazi hali inayokinzana na mila, desturi na tamaduni za watu mahalia.. Haya ni mambo yanayoendelea kudhohofisha nguvu ya Umoja wa Mataifa, kiasi hata cha baadhi ya nchi kukosa imani kwa Umoja wa Mataifa. Diplomasia ya kimataifa katika ulimwengu mamboleo inawajibisha, ndiyo maana hii pia ni sehemu ya utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa wanadiplomasia na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa amesisitizia kuhusu: haki, wajibu na majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kukazia haki ya kimataifa kama kigezo msingi cha suluhu ya matatizo na kinzani zinazojitokeza katika medani za kimataifa. Kuna haja kwa viongozi wa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, kuwasikiliza wananchi wao sanjari na kukazia haki. Siasa safi ni chombo cha huduma ya amani, inayopania kudumisha maridhiano na utulivu kati ya watu na kwamba, amani ni amana na tunu msingi kwa familia ya binadamu! Siasa safi inajikita katika umoja; utu, heshima na haki msingi za binadamu; umoja na mshikamano, mambo msingi yanayokaziwa katika Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Changamoto endelevu kwa sasa ni kuweza kupambana na: Ubaguzi, ukosefu wa haki na usawa pamoja na misimamo mikali ya kidini, kisiasa na kiitikidadi.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea maskini na wanyonge katika jamii; kwa: Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya jamii inayowakirimia hifadhi na usalama, ombi ambalo limepokelewa kwa mikono miwili na Jumuiya pamoja na watu wenye mapenzi mema. Hawa ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita, nyanyaso na dhuluma za kidini. Baba Mtakatifu anazipongeza nchi za Yordan na Lebanon kwa kuonesha ukarimu na kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji huko Mashariki ya Kati, mahali ambako walengwa wa nyanyaso na dhuluma hizi ni Wakristo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika kipindi cha Mwaka 2019 anatarajia kufanya hija ya kitume huko Morocco na Nchi za Falme za Kiarabu ambako kuna idadi kubwa ya waaamini wa dini ya Kiislam. Lengo ni kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ili waamini wa dini hizi mbili waweze kufahamiana, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na  Sultan Al Malik al- Kamil.

Papa Francisko anawaalika wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuangalia hatima ya wakimbizi na wahamiaji wanaokimbia: umaskini, vita, dhuluma, nyanyaso pamoja na majanga asilia; kwa kutetea: haki zao msingi, utu na heshima yao; kwa kuonesha umoja na mshikamano kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Wakimbizi na wahamiaji kutoka Colombia na Venezuela wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma kwa kuheshimu na kuzingatia sheria za Kimataifa. Kimsingi, “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Ingawa Mkataba huu hauzifungi kisheria nchi husika, lakini ni muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa kama chombo cha rejea katika mchakato wa kudumisha uhai na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linaendelea kuwekeza katika utume wa Vijana, kama ilivyokuwa kwa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana sanjari na maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019. Lengo ni kuendelea kuwekeza zaidi katika maisha na utume wa vijana, kwa kuwahakikishia fursa za ajira, ili hatimaye, waweze kuunda familia, kulea na kukuza watoto wao. Mwaka 2019, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto. Huu ni wakati wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete dhidi ya nyanyaso na dhuluma kwa watoto wadogo. Kanisa linaendelea kujipanga ili kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, ili haki na ukweli viweze kutawala. Mkutano kati ya Papa Francisko na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu  Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, unapania kuona ukweli wa athari zilizosababishwa na kashfa hii.

Mwaka 2019, Kanisa linaadhimisha pia kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa Kitume, “Mulieris dignitatem” yaani “Utu na wito wa wanawake”. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha mahusiano ya dhati kati ya mwanaume na mwanamke; kwa kuheshimiana na kuthaminiana; ili kuondokana na nyanyaso dhidi ya wanawake na wasichana zinazoendelea kusikika majumbani. Juhudi hizi zinapaswa pia kuheshimu na kuimarisha tofauti kati ya mwanamke na mwanaume kadiri ya mpango wa Mungu kwani zinakamilishana.

Papa Francisko anasema, Shirika la Kazi Duniani, ILO, mwaka 2019 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ukuaji hafifu wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na hupatikanaji wa kazi zenye staha na zinazoheshimu utu na heshima ya binadamu ni kati ya changamoto endelevu kwa Shirika la Kazi Duniani. ILO inahimizwa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, linajizatiti katika kupambana na kazi za suluba miongoni mwa watoto wadogo, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo pamoja na kuhakikisha kwamba, wafanyakazi wanapata ujira stahiki, changamoto pevu katika Nchi changa duniani bila kusahau ubaguzi wa wanawake katika maeneo ya kazi!

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa ijikite katika ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu na wajenzi wa amani; kwa kukataa falsafa ya vita, kinzani na mipasuko na kuanza kujikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Ethiopia na Eritrea ni mfano bora wa kuigwa; jitihada hizi zinapaswa pia kuigwa na Sudan ya Kusini na kwamba, kuna matumaini huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ingawa bado vita imepamba moto! Papa anasema, anafuatilia kwa umakini mkubwa hali tete huko DRC, akiwa na matumaini kwamba, nchi hii itaweza kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kweli, tayari kuanza kucharuka katika maendeleo fungamani ya watu wake.

Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa familia ya Mungu nchini Mali, Niger, Nigeria na Cameroon ambako vitendo vya kigaidi vinaendelea kuvuruga misingi ya haki, amani na mafungamano ya kijamii. Papa anasema, licha ya matatizo na changamoto zinazoliandama Bara la Afrika, lakini bado limeendelea kujipambanua kwa tunu msingi za maisha na utu; kwa ukarimu; amani na maridhiano kati ya waamini wa dini mbali mbali; kwa kukuza na kuendelea kudumisha demokrasia shirikishi sanjari na haki jamii. Ili kukuza na kudumisha uchumi fungamani, nchi nyingi Barani Afrika zimeendelea kuwekeza katika ujenzi na maboresho ya miundo mbinu ya maendeleo.

Vatican inaendelea kuimarisha uhusiano wake na Korea kwa njia ya majadiliano ya kidiplomasia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Venezuela, Israeli na Palestina zitaweza kujikita katika majadiliano ili kupata suluhu ya amani, kama ilivyo hata kwa Yemen na Iraq. Daima ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Biashara haramu ya silaha duniani ni tishio kwa: amani, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi na usalama duniani. Lakini, waathirika wakuu ni watu wanaotoka katika nchi maskini zaidi duniani. Baba Mtakatifu anasema, kamwe ushirikiano wa Kimataifa hauwezi kutawaliwa kwa mtutu wa bunduki, sera za vitisho pamoja na silaha za maangamizi.

COP24 Katowice: Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kubwa ya maendeleo duniani. Athari zake ni pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; kuongezeka kwa joto; ukame; mafuriko; njaa, vita kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na ongezeko kubwa la wadudu waharibifu wa mimea, na magonjwa ya mifugo na binadamu; kukauka kwa vyanzo vya maji; kuyeyuka kwa theluji n.k. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kushirikiana ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu anasema, Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatakayofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba 2019 yataongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia inakazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali:kuhusu: haki jamii, malezi, katekesi, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia.

Baba Mtakatifu pia amegusia kuhusu kuanguka kwa Ukuta wa Berlin kunako mwaka 1989 na huo ukawa ni kuporomoka kwa vita baridi, mwanzo wa Umoja wa Ulaya na mchakato wa ujenzi wa: amani, urafiki, ushirikiano na mshikamano kati ya watu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Mwaka 2019 Nchi ya Vatican moja ya nchi ndogo kabisa duniani, tarehe 11 Februari, 2019 inatimiza miaka tisini tangu Kanisa Katoliki lilipotiliana sahihi mkataba na Serikali ya Italia iliyokuwa inaibuka baada ya kutenganisha Kanisa na Serikali. Mkataba wa Laterani uliifanya Vatican kutambuliwa rasmi kama nchi huru yenye uwezo wa kujiamria mambo yake yenyewe katika medani za kimataifa bila kuingiliwa na Serikali ya Italia. Papa Pio XI alilitaka Kanisa kuendelea kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Italia: kiroho na kimwili; kwa kutumia amana na utajiri wake wa kihistoria, kitamaduni na kisanaa; mambo yanayofumbatwa katika Ukristo. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuihakikishia Italia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, ili iendelee kuwa aminifu kwa Mapokeo, kwa kuendelea kupyaisha udugu wa mshikamano ambao umeipambanua Italia kwa miaka mingi.

Papa: Ujumbe Mabalozi 2019
07 January 2019, 14:11