Tafuta

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Morocco inaongozwa na kauli mbiu "Mhudumu wa Matumaini" Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Morocco inaongozwa na kauli mbiu "Mhudumu wa Matumaini" 

Hija ya Papa Francisko nchini Morocco: Mhudumu wa matumaini!

Papa Francisko anasema, hija hizi za kitume ni mbinu mkakati wa kutaka kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; na kama fursa ya waamini wa dini hizi mbili kuweza kufahamiana, hasa wakati huu wa kumbu kumbu ya miaka mia nane, tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na Sultani Al-Malik al Kamil.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Mfalme Mohammed VI pamoja na Maaskofu Katoliki nchini Morocco, kutembelea nchi yao kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019. Hija hii ya kitume inaongozwa na kauli mbiu “Mhudumu wa matumaini”. Safari hii inafuatiwa na hija ya kitume ambayo Baba Mtakatifu anatarajiwa kuifanya huko katika nchi za Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 3-5 Februari 2019.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa mabalozi na wawakilishi wa mashirika mbali mbali ya Kimataifa mjini Vatican kwa mwaka 2019, alikazia hija hizi za kitume kama mbinu mkakati wa kutaka kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; na kama fursa ya waamini wa dini hizi mbili kuweza kufahamiana, hasa wakati huu wa kumbu kumbu ya miaka mia nane, tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na Sultani Al-Malik al Kamil.

Hii ni hija ya kitume inayofumbatwa katika majadiliano ya kidini pamoja na fursa ya watu kukutana; ni fursa kwa waamini wa dini ya Kiislam kuweza kukutana na ndugu zao Wakristo, mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika nembo ya hija ya Baba Mtakatifu nchini Morocco. Msalaba wa Kikristo unafumbatwa katika alama ya mwezi inayopambwa kwa rangi za bendera ya Morocco. Katika hija hii ya kitume huko Morocco, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutembelea mji wa Rabat na Casablanca. Baba Mtakatifu Francisko anataka kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo, haki na mshikamano wa dhati na kwamba, tofauti mbali mbali zisiwe ni chanzo cha vurugu na mitafaruku ya kijamii na kidini.

Papa: Morocco
12 January 2019, 14:43