Tafuta

Papa Francisko amewaandikia Maaskofu Katoliki Nchini Marekani Barua kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo Papa Francisko amewaandikia Maaskofu Katoliki Nchini Marekani Barua kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo 

Barua ya Papa kwa Maaskofu Katoliki Marekani: Wongofu

anawataka Maaskofu: kukesha na kung’amua; kashfa ya matumizi mabaya ya madaraka kiasi cha kulitumbukiza Kanisa katika kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Umuhimu wa toba na wongofu wa kimisionari; umoja na mshikamano katika urika wa Maaskofu, ili kukuza na kudumisha ukatoliki; kwa kuvunjilia mbali mnyororo wa kashfa za kijinsia kwa kudumisha uongozi bora na utakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa Katoliki nchini Marekani katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, limetikiswa sana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, kiasi hata cha kuchafua dhamana na utume wa Kanisa ndani na nje ya Marekani. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na kusikitishwa na kashfa hizi, mwezi Septemba, 2018 aliwashauri Maaskofu Katoliki Marekani, kufanya mafungo ya kiroho ambayo yameanza tangu tarehe 2 Januari 2019 na yanatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 8 Januari 2019. Haya ni mafungo yanayoendeshwa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa kwa kuongozwa na kauli mbiu “Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri”.

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Barua Maaskofu Katoliki wa Marekani, akiwataka kusimama kidete kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia inayochafua maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu katika barua hii anawataka Maaskofu: kukesha na kung’amua; kashfa ya matumizi mabaya ya madaraka kiasi cha kulitumbukiza Kanisa katika kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Umuhimu wa toba na wongofu wa kimisionari; umoja na mshikamano katika urika wa Maaskofu, ili kukuza na kudumisha ukatoliki; kwa kuvunjilia mbali mnyororo wa kashfa za kijinsia; kwa kujikita katika dhana ya uongozi kama huduma kwa watu wa Mungu na kwamba, Kanisa linapaswa kujikita katika ushuhuda na utakatifu wa maisha!

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kurejea tena katika Injili ya Kristo, kwa kujikita katika sala, tafakari ya kina pamoja na kujenga sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza waamini wao, kama njia ya kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, ili kupyaisha maisha na utume wa Kanisa nchini Marekani. Uongozi ndani ya Kanisa ni dhamana na utume unaosimikwa katika huduma mintarafu Maandiko Matakatifu. Uongozi ndani ya Kanisa si mahali pa kujitafutia umaarufu na utajiri; kwani sumu hii inapoingia katika maisha na utume wa Kanisa matokeo yake ni kinzani na mipasuko isiyokuwa na tija wala mashiko; hali ya kudhaniana vibaya na kutoelewana. Kumbe, kuna haja ya kuzuia kuliko kuganga na kutibu kwa kujikita katika: Neno la Mungu, maisha ya sala, kwa kuwasikiliza waamini pamoja na kujenga umoja wa kidugu!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Kanisa nchini Marekani limeguswa na kutikishwa na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, hali ambayo kimsingi ni dhambi, uhalifu na ukatili mkubwa. Baadhi ya viongozi wa Kanisa wakafunika maovu haya kwa sababu binafsi, badala ya matatizo haya kupatiwa tiba na suluhu ya kudumu matokeo yake, dhambi na uhalifu huu ukasambaa ndani ya Kanisa kama “moto wa mabua” kiasi cha kuliathiri: Kanisa na familia ya Mungu katika ujumla wake, leo hii Kanisa linapaswa kuganga na kuponya madonda makubwa ya kashfa za nyanyaso za kijinsia nchini Marekani, ili kutoa nafasi kwa Mwanga wa Injili kuweza kung’aa tena!

Ili kukabiliana na kashfa hii, inayofumbatwa katika utamaduni wa nyanyaso, ukosefu wa uaminifu kwa upande wa Kanisa, hali inayochafua maisha na utume wa Kanisa, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu; kwa kukuza na kuendeleza hali ya kuaminiana na kuthaminiana kama ndugu; kwa kuheshimu maisha fungamani ya kijumuiya pamoja na kutunza faragha ya watu. Yote haya yanahitaji toba na wongofu wa ndani, ili kupyaisha namna ya kufikiri na kutenda ili kudumisha uongozi bora; kwa kuendeleza: ukweli, uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za Kanisa bila kusahau mahusiano na mafungamano ya kijamii na watu wanaowazunguka.

Toba na wongofu wa kichungaji na kimisionari ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa anasema Baba Mtakatifu Francisko. Utu, heshima, haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kulindwa na kudumishwa kama sehemu ya ushuhuda wa maisha na utume wa Kanisa, ili kuondolea mbali ubinafsi na hali ya viongozi wa Kanisa kutaka kujitafuta wenyewe. Kanisa linahitaji Maaskofu watakaowasaidia waamini kung’amua uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao; viongozi watakaodumisha umoja na mshikamano katika urika wa Maaskofu; viongozi watakao kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo.

Kashfa, matatizo na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa zinaweza kuwa ni chanzo cha kuvuruga umoja na udugu. Ikumbukwe kwamba, uaminifu wa maisha na utume wa Kanisa unafumbatwa katika: toba na wongofu wa ndani; kwa kujenga na kudumisha umoja sanjari na ushuhuda wa utakatifu wa maisha kama kielelezo cha imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu. Viongozi wa Kanisa watambue karama na mapungufu yao ya kibinadamu. Vinginevyo, hawa ni wale watu wanaomtangaza Mungu bila ya Kristo; wanamtangaza Kristo bila ya Kanisa na Kanisa bila ya watu wa Mungu. Ukatoliki unasimikwa katika umoja na udugu na kamwe hauwezi kushushwa na kuonekana kuwa ni masuala ya Mafundisho, Sheria, Kanuni na Taratibu peke yake.

Ukatoliki unawakumbusha waamini kwamba, wanapaswa kusumbukiana kwa pamoja! Kwa kutambua kwamba, kama binadamu wanaweza kutumbukia katika dhambi, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu; kwa kujenga na kudumisha umoja wa watu wa Mungu; kwa kupongeza na kushukuru pale mambo yanapokwenda vizuri. Lakini zaidi, waamini wanapaswa kusikiliza kwa makini; ili kuamua na kutenda katika umoja na mshikamano; kwa kuondokana na majungu na kuanza kujikita katika: toba na wongofu wa ndani; sala na majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na kufanya mang’amuzi. Viongozi wa Kanisa wawe wakweli katika maisha na utume wao, kwa kujikubali jinsi walivyo na kuanza kurekebisha mapungufu yao kama binadamu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, Kanisa linaendelea kuteseka kutokana na uchu wa mali na madaraka; kashfa ya nyanyaso za kijinsia pamoja na matumizi mabaya ya madaraka; changamoto na mwaliko kwa viongozi kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi ili aweze kuwaletea mabadiliko katika maisha, kwa kuendelea kunyenyekea na kujikita katika imani na huduma makini kwa watu wa Mungu inayofumbatwa katika kiini cha Injili. Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu; ni chombo cha kuleta umoja kati ya wanadamu wote; ni mahali pa watu kukutana na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Ushuhuda wa Kanisa unapaswa kusimikwa katika muungamano na mafungamano ya kijamii, ili kudumisha amani na utulivu!

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho anasema Mama Theresa wa Calcutta, Mwenyezi Mungu amewafunulia walimwengu huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Ukosefu wa umoja na mshikamano; kinzani na mipasuko ni kati ya changamoto zinazoweza kukwamisha maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo, ndiyo maana Kristo Yesu, katika Sala ya Kikuhani, anaombea umoja miongoni mwa wafuasi wake.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha barua yake kwa Maaskofu Katoliki Marekani kwa kusema kwamba, mafungo haya ni muda wa kusali, kutafakari, kukaa kimya; kujadiliana na hatimaye, kujenga umoja na mshikamano katika urika wa Maaskofu. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awasindikize katika maisha na utume wao, ili kupyaisha maisha, na kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Kristo Yesu, Mfufuka!

Papa: Maaskofu USA
04 January 2019, 12:05