Cerca

Vatican News
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu, Abu Dhabi, Falme za Kiarabu Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu Abu Dhabi, Falme za Kiarabu. 

Ziara ya Papa Francisko Abu Dhabi: Ujumbe kwa watu wa Mungu!

Falme za Kiarabu ni nchi ambayo kwa sasa inajielekeza zaidi ili kuwa ni mfano bora wa maridhiano; udugu wa kibinadamu na mahali ambapo ustaarabu na tamaduni mbali mbali zinakutana na hivyo kuwawezesha watu kupata mahali salama ambapo wanaweza kufanya kazi, kuishi kwa uhuru na kuheshimiana hata katika tofauti zao msingi! Baba Mtakatifu anafurahia kuwatembelea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, kuanzia tarehe 3 hadi 5 Februari 2019, anatarajia kufanya hija ya kitume ya ishirini na saba huko Abu Dhabi, kwenye Falme za Kiarabu, ili kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini unaoongozwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu". Akiwa huko kwenye Falme za Kiarabu, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa mahubiri yake pamoja na hotuba kwenye mkutano wa majadiliano ya kidini. Hii ni mara ya kwanza katika historia kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kutembelea Falme za Kiarabu.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa familia ya Mungu kwenye Falme za Kiarabu wakati huu anapojiandaa kufanya hija ya kitume nchini mwao, kwanza kabisa anapenda kuwatakia amani. Falme za Kiarabu ni nchi ambayo kwa sasa inajielekeza zaidi ili kuwa ni mfano bora wa maridhiano; udugu wa kibinadamu na mahali ambapo ustaarabu na tamaduni mbali mbali zinakutana na hivyo kuwawezesha watu kupata mahali salama ambapo wanaweza kufanya kazi, kuishi kwa uhuru na kuheshimiana hata katika tofauti zao msingi!

Baba Mtakatifu anasema, anafurahia kwenda kukutana na watu wanaoishi leo yao huku wakiwa na mwono mpana kwa maisha ya siku za mbeleni. Sheikh Zayed, Muasisi wa Falme za Kiarabu anakumbukwa sana kwa maneno yake ya hekima aliposema, utajiri wa kweli wa nchi si katika vitu, bali utajiri wa taifa lolote lile unafumbatwa katika watu wanaojenga leo na kesho ya taifa lao, kimsingi utajiri wa kweli ni rasilimali watu! Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kumpongeza na kumshukuru Mfalme Mrithi Mohammed bin Zayed Al Nahyan aliyemwalika ili kuhudhuria na hatimaye, kushiriki katika mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu". Baba Mtakatifu anapenda kuwashukuru viongozi wote wa Falme za Kiarabu kwa ushirikiano, ukarimu na udugu waliouonesha ili kuweza kufanikisha hija hii ya kitume!

Baba Mtakatifu anamshukuru kwa namna ya pekee kabisa Imam Ahmad Muhammad Al-Tayyib, Imam mkuu wa Msikiti mkuu wa Al-Azhar, ulioko Cairo, nchini Misri, bila kuwasahau wale wote waliojisadaka kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huu, kwa ujasiri na utashi wa kutaka kuthibitisha kwamba imani kwa Mwenyezi Mungu inawaunganisha watu na wala haipaswi kuwaganya; imani ina mvuto kwa watu, licha ya tofauti zao msingi; imani kimsingi inafukuzia mbali chuki na uhasama. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu anayemkirimia fursa hii ya kuandika ukurasa mpya nchini humo ya mahusiano kati ya dini na kuendelea kukazia kwamba wote ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa njia ya video kwa familia ya Mungu Falme za Kiarabu kwa kusema anasubiri kwa hamu kukutana na kusalimiana na watoto wa Zayed katika nyumba ya Zayed; kwenye nchi ambayo imejaa utajiri wa maendeleo na amani; nchi yenye kung’ara kwa mwanga wa jua na utulivu; nchi ambayo watu wanaishi kwa maridhiano na hatimaye kuweza kukutana.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu ataondoka mjini Roma, Jumapili jioni tarehe 3 Februari na kuwasili majira ya saa 4:00 za usiku kwa saa za Abu Dhabi. Jumatatu, tarehe 4 Februari, Baba Mtakatifu atafanyiwa mapokezi ya kitaifa na hatimaye, kumtembelea Mfalme Mrithi Mohammed bin Zayed Al Nahyan. Jioni, Baba Mtakatifu atafanya mkutano wa faragha na Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam, katika Msikiti mkuu wa Sheikh Zayed na baadaye kushiriki katika mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa kuhusu udugu wa kibinadamu, ulioandaliwa na Mfuko wa Kumbu kumbu ya Mwanzilishi wa Ghuba ya Uajemi.

Hatimaye, tarehe 5 Februari 2019, Baba Mtakatifu Francisko atafanya ziara binafsi ya kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu Abu Dhabi ambalo liko karibu na Kanisa la Mtakatifu Paulo katika eneo la Musaffah. Baadaye, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Zayed na baadaye, ataaga na kuondoka kurejea tena mjini Vatican kuendelea na shughuli zake za kitume!

Papa: Falme za Kiarabu
31 January 2019, 16:10