Cerca

Vatican News
Wafiadini wa Algeria ni mashuhuda na vyombo vya upatanishho, amani na utafiki Wafiadini wa Algeria ni mashuhuda na vyombo vya upatanisho, amani na urafiki.  (ANSA)

Wafiadini wa Algeria ni vyombo vya amani, upatanisho na urafiki!

Wafiadini wa Algeria ni vyombo vya amani na mashuhuda wa umoja na udugu, kielelezo cha utukufu wa Mungu aliye hai! Ni watu waliosimika maisha yao katika sala na tafakari ya Neno la Mungu, mambo yaliyomwilishwa katika Injili ya huduma kwa watu wa Mungu nchini Algeria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, tarehe 8 Desemba 2018 yameacha chapa ya pekee kwa familia ya Mungu nchini Algeria, inayojitahidi kumwilisha moyo wa udugu, urafiki na huduma katika uhalisia wa maisha, changamoto na mwaliko wa kuganga na kuponya madonda ya kihistoria yaliyopita tayari kujenga na kudumisha sanaa na utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kama alivyofanya Askofu Pierre Claverie wa Oran pamoja na watawa wenzake 18 waliotangazwa kuwa Wenyeheri, huko Algeria.

Hawa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika huduma. Ni watu walioteseka, wakanyanyaswa, kudhulumiwa na hata kuuwawa kati ya mwaka 1994 hadi mwaka 1996 wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Algeria. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kuwatangaza wafiadini hawa kuwa Mwenyeheri, mifano bora ya kuigwa katika imani inayomwilishwa katika Injili ya huduma ya upendo, inayowachangamotisha wananchi wa Algeria kuishi kwa pamoja katika amani na kwamba, Kanisa linataka kutangaza na kushuhudia: Injili ya upendo inayosimikwa katika majadiliano ya kidini, amani, utulivu na urafiki!

Kwa upande wake, Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu katika mahubiri yake, amekaza kusema kwamba, wafiadini hawa wameshiriki katika mateso na kifo cha Kristo Yesu kwa njia ya sadaka ya maisha yao, lakini sasa wanashiriki ukuu, utukufu na ushindi wa Kristo Yesu huko mbinguni. Ni watu waliothubutu kukita maisha yao katika tasaufiya ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha kuwa tayari kuyamimina maisha yao kama mbegu ya upatanisho na amani nchini Algeria.

Wafiadini hawa ni vyombo vya amani na mashuhuda wa umoja na udugu, kielelezo cha utukufu wa Mungu aliye hai!  Ni watu waliosimika maisha yao katika sala na tafakari ya Neno la Mungu, mambo yaliyomwilishwa katika Injili ya huduma kwa watu wa Mungu nchini Algeria. Wafiadini hawa wanaendeleza Injili ya huruma ya Mungu na msamaha, chachu ya maisha mapya yanayofumbatwa katika mchakato wa upatanisho, haki na amani.

Wakati huo huo, Askofu mkuu Paul Desfarges wa Jimbo kuu la Algiers anasema, Wenyeheri hawa wapya ni neema kwa familia ya Mungu nchini Algeria, nchi ambayo tangu karne ya kwanza, imeshuhudia damu ya wafiadini, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, hadi dakika ya mwisho, daima wakiendelea kuchuchumilia utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika uhalisia wa kila siku, kama alama ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Upendo wa Kristo unawadai kusamehe na kusahau, kwa kuendeleza majadiliano ya kidini.

Wafiadini wa Algeria
10 December 2018, 09:21