Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Ujumbe wa "Urbi et Orbi" Udugu wa ubinadamu! Papa Francisko Ujumbe wa "Urbi et Orbi": Udugu wa binadamu! 

Papa Francisko: Ujumbe wa: Urbi et Orbi: Udugu wa ubinadamu!

Ujumbe wa Noeli kwa mwaka 2018 unafumbatwa katika udugu kati ya watu wa mataifa na tamaduni; watu wenye mawazo tofauti, lakini wenye uwezo wa kuheshimiana na kusikilizana; udugu kwa watu wa dini mbali mbali, kwani Kristo Yesu amekuja ulimwenguni ili kuwafunulia Uso wa Mungu, wale wote wanaomtafuta Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu aliowaridhia. Kama ilivyokuwa kwa wachungaji kule kondeni, waliondoka wakaenda kwa haraka na kumkuta mtoto mchanga amevishwa nguo za kitoto, amelala katika pango la kulishia wanyama, wakampigia magoti na katika ukimya wakamwabudu. Kiini cha ujumbe wa Noeli kwa mwaka huu ni wema wa Mungu na udugu wa binadamu, unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ili kujenga na kuimarisha ulimwengu unaosimikwa katika haki, bila Kristo Yesu, jitihada za binadamu ni bure kabisa!

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2018 uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Desemba 2018, kwa ajili ya mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi”. Ujumbe wa Noeli kwa mwaka 2018 unafumbatwa katika udugu kati ya watu wa mataifa na tamaduni; watu wenye mawazo tofauti, lakini wenye uwezo wa kuheshimiana na kusikilizana; udugu kwa watu wa dini mbali mbali, kwani Kristo Yesu amekuja ulimwenguni ili kuwafunulia Uso wa Mungu, wale wote wanaomtafuta Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao.

Uso wa Mungu umefunuliwa katika uso wa mwanadamu, aliyezaliwa katika wakati na mahali. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwana wa Mungu amewafunulia walimwengu kwamba, wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu unafumbatwa katika: upendo, ukarimu, utu na heshima ya binadamu; utu ambao watu wote wanashirikishana licha ya tofauti zao za kikabila, lugha na tamaduni, lakini wote wanajisikia kuwa ni sehemu ya udugu wa binadamu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, tofauti zinazojitokeza kati ya binadamu ni amana na utajiri mkubwa unaounda na kujenga familia ya binadamu. Daima kutakuwepo na tofauti, kinzani na mikwaruzo, lakini wote bado wanafungwa pamoja katika kifungo cha upendo wa wazazi wao unaowasukuma kuendelea kupendana. Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote, msingi na nguvu ya udugu wa binadamu! Noeli ya Mwaka 2018 iwe ni fursa ya kugundua udugu unaowaunganisha watu. Waisraeli na Wapelestina warejee tena katika majadiliano na safari ya amani ili hatimaye, kuweza kuhitimisha mgogoro huu ambao umedumu kwa takribani miaka saba, ili watu waweze tena kuuona Uso wa huruma ya Mungu.

Mtoto Yesu asaidie Siria kugundua tena udugu baada ya vita ya miaka hii ya karibuni na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa, isaidie kupatikana kwa suluhu ya kisiasa itakayozima mipasuko na mafao binafsi, ili wananchi wa Siria, hasa wale waliokimbia nchi yao ili kutafuta, hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kwingineko waweze kurejea tena na kupata amani na utulivu nchini mwao! Baba Mtakatifu ameyaelekeza mawazo yake huko Yemen, ili juhudi za Jumuiya ya Kimataifa zinazotaka kusitishwa mara moja vita ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa ili kutoa nafuu kwa wananchi, lakini kwa watoto zaidi wanaoendelea “kupukutika” kwa vita na njaa.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia Bara la Afrika, amewakumbuka mamilioni ya watu wanaokimbia nchi zao au watu wasiokuwa na makazi maluum; makundi yanayohitaji huduma, ulinzi na usalama pamoja na chakula kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Mtoto Yesu, Mfalme wa amani, asaidie jitihada za kusitisha mapambano ya silaha, ili hatimaye, familia ya watu wa Mungu Barani Afrika iweze kuona mapambazuko mapya ya udugu, kwa kubariki jitihada: haki, amani na upatanisho katika ngazi ya kisiasa na kijamii.

Kipindi hiki cha Noeli, kiendelee kuimarisha umoja na udugu wa familia ya Mungu huko Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini, kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa unaopania kuimarisha umoja na mshikamano kati ya nchi hizi mbili, ili hatimaye, kufikia suluhu ya pamoja itakayowahakikishia watu wote: ustawi na maendeleo ya kweli. Baba Mtakatifu amewakumbuka wananchi wa Venezuela kuendelea na juhudi za kutafuta amani na utulivu; kwa kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya maendeleo ya nchi huku wakiendelea kuwasaidia watu wanyonge ndani ya jamii.

Baba Mtakatifu ameiombea Ukrain, inayotamani kupata amani ya kudumu; amani ambayo inayoendelea kucheleweshwa kila kukicha. Ni kwa kuheshimu na kudumisha haki msingi za binadamu, amani inaweza kutawala na nchi kuanza kurejesha tena mambo msingi yatakayowawezesha watu kuishi maisha yanayosimikwa katika utu. Wakristo katika ukanda huu, wajenge na kuimarisha udugu na urafiki. Baba Mtakatifu anawakumbuka wananchi wa Nicaragua, ili kuondokana na kinzani pamoja na mipasuko ya kijamii, ili kujikita katika upatanisho ili kwa pamoja waendeleze mchakato wa upatanisho, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini humo.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawakumbuka watu wanaoendelea kuathirika kutokana na ukoloni wa kiitikadi, kitamaduni na kiuchumi; jambo ambalo linakinzana na kutishia uhuru na utambulisho wao, kwa kuendelea kuteseka kwa balaa la njaa; ukosefu wa huduma bora katika elimu na afya. Baba Mtakatifu amewaombea Wakristo ambao wanaadhimisha Sherehe ya Noeli katika mazingira magumu na hatarishi, ili Kristo aweze kuwakirimia amani na haki zao msingi kuheshimiwa na hasa uhuru wa kuabudu. Watu wote wapate amani na fanaka kwa kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia, kwani wote wanapendwa na Baba wa mbinguni ili kupata na kuishi tena udugu!

Papa: Ujumbe Noeli 2018
25 December 2018, 17:02