Tafuta

Vatican News
Papa Francisko. Telepace: tangazeni Injili ya imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mataifa! Papa Francisko. Telepace: tangazeni Injili ya imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mataifa!  (Vatican Media)

Telepace: Tangazeni Injili ya amani, matumaini kwa watu wa Mataifa!

Papa Francisko anakitaka Kituo cha Televisheni cha Telepace kiwe ni antena za maisha ya kiroho; kisaidie malezi na majiundo ya vijana katika shule ya Injili; kiwajengee watu shauku ya ujenzi wa ufalme wa Mungu kwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Kiwe ni chombo hai cha tasaufi inayowapeleka watu kwa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kituo cha Televisheni cha Telepace kinaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwake. Kwa muda wote huu, chombo hiki ambacho ni zawadi kutoka kwa Mungu kimewaunganisha na kuwafanya watu kuwa karibu; kimelinda, kutetea, kuponya, kusindikiza na kuwasaidia watu kufurahia maisha. Ni kituo ambacho kimejipambanua kwa ajili ya huduma kwa Mungu na Kanisa na kamwe hakikutawaliwa na matangazo ya biashara tangu kuanzishwa kwake, daima kimejielekeza kutafuta na kujenga ufalme wa Mungu.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 13 Desemba 2018 alipokutana na kuzungumza na viongozi pamoja na wafanyakazi wa Kituo cha Televisheni cha Telepace kinachorusha matangazo yake nchini Italia, ambacho kinaendelea kuwa kweli ni sauti kwa wale wasiokuwa na sauti katika jamii. Ni kituo ambacho kimeendelea kurusha maadhimisho mbali mbali yanayofanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro tangu mwaka 1990 kwa utashi wa Mtakatifu Yohane Paulo II.

Hiki ni kituo kinachoendelea kurusha Katekesi za Baba Mtakatifu kila Jumatano, Sala ya Malaika wa Bwana, kila Jumapili na katika Siku kuu zilizo amriwa, Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya ukombozi pamoja na maadhimisho mbali mbali yanayofanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kiasi cha kuwafikia watazamaji huko huko majumbani mwao! Kwa hakika kuna uhusiano mkubwa kati ya Kituo cha Televisheni cha Telepace, Vatican na Bikira Maria, Nyota ya Uinjilishaji.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia mambo makuu matatu: kwanza kabisa kituo hiki kiwe ni antena za maisha ya kiroho; kisaidie malezi na majiundo ya vijana katika shule ya Injili; Telepace ijikite katika mambo msingi ya maisha pasi na kujikwaa katika habari nyepesi nyepesi! Baba Mtakatifu anaitaka Telepace iwe ni kituo kinachowajengea watu shauku ya ujenzi wa ufalme wa Mungu kwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Kiwe ni chombo hai cha tasaufi inayowapeleka watu kwa Mungu, hasa kwa kuwashirikisha maskini, wanyonge na wale wanaotengwa na jamii kutokana na sababu mbali mbali. Telepace iwe karibu na wagonjwa, wafungwa na watu ambao wako kufani, ili waweze kufarijika kwa matangazo yake! Hii ndiyo tasauti ya upendo!

Pili, Telepace kiwe ni chombo cha kuwafunda na kuwaelimisha vijana, ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Kanisa kwa kutambua kwamba, vijana wanayo nafasi ya pekee kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu. Vijana waonjeshwe upendo unaoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha. Matangazo yaoneshe matatizo, changamoto na matumaini ya vijana wa kizazi kipya kama walivyokazia Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana iliyohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican. Furaha ya Injili inawaita vijana kujichotea maadili na utu wema kwa kuwafunda katika shule ya Injili, inayowataka wafanyakazi katika tasnia ya habari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Neno la Mungu linalookoa. Mawasiliano yao, yawe ni kiungo cha majadiliano yanayojenga usikivu kwa vijana, ili kufikia lengo hili Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kuthubutu!

Tatu, Telepace kiwe ni kituo kinachojikita kutangaza mambo msingi katika maisha badala ya kukimbilia habari nyepesi nyepesi, kwa kutangaza habari zinazowatajirisha watazamaji wake. Habari za ovyo anasema Baba Mtakatifu Francisko ni chanzo cha chuki, uhasama na wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko; uchu wa mali na madaraka, kiasi hata cha kuwafanya baadhi ya watu kutumbukia katika utamaduni wa kifo, na umbea ambao kamwe si mtaji! Waandishi wa habari wawe ni vyombo vya ujenzi wa amani duniani; sauti ya maskini na wanyonge, waoneshe matatizo na suluhu zake badala ya kuendekeza vita ya maneno ambayo kimsingi ni hatari sana kwa ustawi na mafungamano ya kijamii. Kamwe wafanyakazi wa Telepace, wasithubutu kusaliti jina lao la kutangaza na kushuhudia amani duniani; amani ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; wawe ni njiwa wa amani katika sala na Injili ya upendo.

Papa: Telepace
13 December 2018, 14:23