Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asikitishwa na shambulizi la kigaidi huko Giza, Misri. Papa Francisko asikitishwa na shambulizi la kigaidi huko Giza, Misri.  (AFP or licensors)

Papa Francisko asikitishwa na shambuzi la kigaidi huko Misri!

Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Rais Abdel Fattah Al Sis, anasema kwamba, anasikitishwa na vitendo hivi vya kikatili na kwamba, anawakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na shambulio hili pamoja na ndugu na jamaa zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na shambulizi la kigaidi lililotokea siku ya Ijumaa, tarehe 28 Desemba 2018 huko kwenye Piramidi za Giza na kusababisha watalii wanne kupoteza maisha yao. Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Rais Abdel Fattah Al Sis, anasema kwamba, anasikitishwa na vitendo hivi vya kikatili na kwamba, anawakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na shambulio hili pamoja na ndugu na jamaa zao.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, juhudi zitaongezwa ili kuhakikisha kwamba, vitendo vya kigaidi vinavyohatarisha amani, usalama na mafungamano ya kijamii vinatoweka kabisa kwa kujenga mshikamano wa upendo, haki na amani. Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa familia ya Mungu nchini Misri.

Taarifa kutoka Kairo, Misri zinasema kwamba, vikosi vya ulinzi na usalama nchini Misri vimefanya mashambuli dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuwa ni magaidi na kufanikiwa kuuwa watu 40. Mashambulizi haya yanakuja wakati ambapo Misri inaanza kufufua uchumi wake kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya utalii. Bus lilikuwa limebeba watalii 16, kati yao 4 wameuwawa kikatili na wengine 10 wamejeruhiwa vibaya. Wachunguzi wa mambo ya ulinzi na usalama wanabaini kwamba, mashambulizi ya kigaidi kwa sasa yanalenga taasisi, maeneo ya ulinzi na usalama; maeneo ya kitalii pamoja na nyumba za ibada zinazotumiwa na Wakristo nchini Misri.

Itakumbukwa kwamba, Piramidi za Giza ni kati ya majengo yanayojulikana zaidi duniani. Hii ni sehemu ya makaburi ya Giza yaliyokuwa mahali pa kuzika wafalme wa Misri na wakubwa wa milki yao kwa muda wa miaka 2500.  Piramidi hizi ziko kando ya bonde la mto Nile, karibu na mji wa Giza takriban kilometa 15 kutoka Kairo, mji mkuu wa Misri.

Papa: Mauaji Misri

 

 

 

29 December 2018, 15:41