Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Mwenyezi Mungu anakutana na watu katika imani na matendo! Papa Francisko: Mwenyezi Mungu anakutana na watu katika imani na matendo!  (ANSA)

Papa Francisko: Mungu anakutana na watu katika imani na matendo

Bikira Maria amini akawa ni mfano bora wa kuigwa na Zakaria kutokana na mashaka yake, akakiona cha mtema kuni! Bila imani, mwamini hawezi kusikia sauti ya Mungu inayoleta faraja na hivyo kushindwa kuwa ni mjumbe wa faraja na matumaini kwa jirani zake. Hii inatoka na ukweli kwamba, imani inamwezesha mwamini kutoa ujumbe unaogusa maisha ya mtu anayemsikiliza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Majilio inamweka Bikira Maria kuwa ni mfano bora wa imani inayomwilishwa katika matendo, kwa kumtembelea binamu yake Elizabeti, aliyekuwa na mimba ya miezi sita ya mtoto mwanaume, kwa yeye aliyeitwa tasa. Bikira Maria alipoingia nyumbani mwa Zakaria akamwamkia Elizabeti kwa furaha na bashasha kwa kumwona Bikira Maria akiwa ni mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Elizabetiakapaza sauti kwa nguvu na kusema, “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa”.

Na hapa Elizabeti anakiri imani yake kwa Mwenyezi Mungu, akisema “Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana". Kwa bahati mbaya, Zakaria katika uzee wake na kwa kumwangalia mkewe Elizabeti aliyekuwa tasa, hakuamini hata kidogo maneno ya Malaika Gabrieli, akapewa adhabu ya kuwa bubu hadi siku ile yatakapotukia haya na kama sehemu ya mchakato wa kuendelea kukua na kukomaa katika imani.

Tafakari hii ni mwanga angavu unaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anakutana na binadamu katika imani na upendo, kama Bikira Maria alivyo amini akawa ni mfano bora wa kuigwa na Zakaria kutokana na mashaka yake, akakiona cha mtema kuni! Bila imani, mwamini hawezi kusikia sauti ya Mungu inayoleta faraja na hivyo kushindwa kuwa ni mjumbe wa faraja na matumaini kwa jirani zake. Hii inatoka na ukweli kwamba, imani inamwezesha mwamini kutoa ujumbe unaogusa maisha ya mtu anayemsikiliza! Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Majilio, tarehe 23 Desemba 2018 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anakaza kusema, imani inaboreshwa kwa kumwilishwa katika huduma ya upendo, kama alivyofanya Bikira Maria kwa kumtembelea na kumhudumia Elizabeti.

Baba Mtakatifu anasema, waamini wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo. Tukio la Fumbo la Umwilisho, anasema Baba Mtakatifu lilianza kwa tendo la upendo, kielelezo cha upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Sehemu hii ya Injili inawaandaa waamini kuweza kuadhimisha Fumbo la Umwilisho kwa njia ya imani na mapendo, kazi ya Roho Mtakatifu aliyemwezesha Bikira Maria kupata mimba na kumsukuma kwenda kumtembelea na kumhudumia Elizabeti.

Katika furaha na matumaini, hawa wanawake wawili wanakutana na kuanza kumwimbia Mungu utenzi wa furaha, hivi ndivyo ilivyo kwa wale wote wanaomtumainia na kujiaminisha kwake! Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwaombea na hatimaye, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, Jirani na wale wote wanaohitaji msaada zaidi. Kwa njia hii, Injili ya upendo, itaweza kumwilishwa na kukaa kati ya watu wa Mungu!

Papa: Imani na Matendo
23 December 2018, 15:02