Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Majilio ni kipindi cha kukesha na kusali; toba na wongofu wa ndani. Papa Francisko: Majilio ni kipindi cha kukesha na kusali; toba na wongofu wa ndani.  (ANSA)

Majilio ni kipindi cha kusali na kukesha; toba na wongofu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Njia ya Bwana inaandaliwa kwa toba na wongofu wa ndani; kwa kuondokana na matendo yanayoweka ubadiri na ukakasi katika maisha ya waamini, tayari kuungana na Kristo Yesu, ili kuwaonjesha jirani udugu unaosimikwa katika upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Majilio ni kipindi cha kumngojea Kristo Yesu, Masiha na Mkombozi wa ulimwengu anayekuja, kwa kukesha na kusali; matendo yanayomwilishwa katika hija ya toba na wongofu wa ndani kama anavyokazia Yohane Mbatizaji katika mahubiri yake mintarafu Ubatizo wa toba kwa maondoleo ya dhambi. Yohane Mbatizaji anasema kwamba, yeye ni sauti ya mtu aliaye nyikani, itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake. Kila bonde litajazwa, na kila mlima na kilima kitashushwa; palipopondeka patakuwa pamenyoka, na palipoparuza patalainishwa!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 9 Desemba, 2018 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anakaza kusema, njia ya Bwana inaandaliwa kwa toba na wongofu wa ndani; kwa kuondokana na matendo yanayoweka ubadiri na ukakasi katika maisha ya waamini, tayari kuungana na Kristo Yesu, ili kuwaonjesha jirani udugu unaosimikwa katika upendo! Haiwezekani kuwa na uhusiano mwema na Kristo Yesu, wakati kuna mashimo makubwa ya mahusiano na watu wengine! Upendo kwa Mungu na jirani ni mambo msingi katika Kipindi cha Majilio.

Ni wakati muafaka wa kuporomosha vilima vya majivuno na kiburi, kwa kujenga mahusiano na mafungamano mema na jirani; kwa kujikita katika upatanisho kwa kuwa wa kwanza kuomba msamana na maondoleo ya dhambi walizotenda! Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si rahisi sana kuomba msamaha, lakini Mwenyezi Mungu anaweza kuwasaidia waamini wenye mapenzi mema kuomba na kupata msamaha. Wongofu wa ndani ni mchakato unaomwezesha mwamini katika hali ya unyenyekevu kutambua dhambi na mapungufu yake ya kibinadamu; ukosefu wa uaminifu na hali ya kutotekeleza vyema wajibu!

Mwamini wa kweli ni yule anayethubutu kumwilisha wongofu wa ndani kwa njia ya upendo kamili kwa jirani kama anavyokazia Yohane Mbatizaji, kama njia inayofungua mapito jangwani, kwa kuonesha matumaini, kwa wale waliokata tamaa na hatimaye, kushindwa katika maisha! Huu ni mwaliko kwa waamini kuondokana na hali ya kukata tamaa, kwa kujifungia katika ubinafsi, kiasi hata cha kumezwa na malimwengu, kwa sababu Kristo Yesu ni kiini cha maisha ya waamini na kwamba, maneno yake ni mwanga angavu, ni upendo na faraja!

Yohane Mbatizaji, aliwataka watu wa nyakati zake, kwa ari nguvu na ukali kutubu ili wapate maondoleo ya dhambi! Yohane Mbatizaji, alikuwa na uwezo wa kusikiliza kwa makini; akatenda kwa wema na huruma kwa wale wote waliomwendea wakitaka kutubu dhambi zao na hatimaye, kubatizwa kwa maondoleo ya dhambi. Huu ni mwaliko kwa waamini kujikita katika ushuhuda unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha! Mafundisho ya Yohane Mbatizaji yalijikita katika ukweli; kwa njia ya ujasiri akatangaza ukweli ulioamsha matumaini ya ujio wa Masiha. Hata leo hii, wafuasi wa Kristo Yesu, wanatakiwa kuwa watu wanyenyekevu na wajasiri, watakaotoka kifua mbele kutangaza na kuwasha moto wa matumaini kwa ujasiri hata kama Ufalme wa Mungu unaendelea kujengeka siku kwa siku kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuchunguza vyema dhamiri zao na kuangalia mahali ambapo wanaweza kubadilisha kama sehemu ya mchakato wa Kipindi cha Majilio, muda muafaka wa kuandaa mapito ya Bwana! Bikira Maria awasaidie waamini kuandaa siku kwa siku mapito ya Bwana, huku wakianzia kwao wenyewe; kwa kueneza wema katika unyenyekevu; kwa kupandikiza mbegu za amani, haki na udugu!

Papa: j2 Majilio

 

 

 

09 December 2018, 10:00