Cerca

Vatican News
Papa Francisko amewaomba wanawake wajawazito kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe Papa Francisko amewaomba wanawake wajawazito kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Gudalupe.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Wanawake wajawazito ombeni tunza na ulinzi wa B. M. wa Guadalupe

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wanawake wajawazito wanaosubiri kujifungua hivi karibuni, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe, kwani, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwaweka wanawake wajawazito wenye matatizo ya uzazi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, inyoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo, tarehe 12 Desemba, Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa Katekesi yake, Jumatano tarehe 12 Desemba 2018, amewaalika wanawake wajawazito wanaosubiri kujifungua kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe, kwani, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwaweka wanawake wajawazito wenye matatizo ya uzazi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe.

Kipindi hiki cha Majilio, kiwe ni fursa ya kusubiri kwa imani, matumaini na mapendo, kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu; kwa kuendelea kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuambata na kufumbata tunu msingi za Kiinjili pamoja na kuwafariji wanawake ambao hawakubahatika kupata watoto, watambue kwamba, watoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayetoa kadiri anavyotaka!

Waamini katika shida na mahangaiko yao ya ndani, kamwe wasikate tamaa, bali wawe na ujasiri wa kumkimbilia Mwenyezi Mungu, Baba mwenye huruma na mapendo, ili awaze kuwakirimia amani ya ndani, furaha na utulivu. Waamini wajiandae kumpokea Mtoto Yesu anayezaliwa tena katika maisha yao kwa unyenyekevu na mapendo makuu, kwani Yesu ni ufunuo wa upendo na huruma ya Baba wa milele! Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awe ni nyota angavu inayolinda maisha katika familia!

Papa: Wanawake wajawazito

 

 

12 December 2018, 14:10