Cerca

Vatican News
Papa Francisko asema, wanasayansi ni wahudumu wa familia ya binadamu! Papa Francisko asema, wanasayansi ni wahudumu wa familia ya binadamu!  (Vatican Media)

Papa Francisko: wanasayansi ni wahudumu wa familia ya binadamu! Unakosekana utashi wa kisiasa tu!

Tafiti kadhaa za kisayansi zinaonesha kwamba, ongezeko kubwa la joto duniani kwa miaka ya hivi karibuni ni matokeo ya ongezeko la hewa ya ukaa angani, matumizi makubwa ya nishati mafuta pamoja na ukataji miti ovyo! Ni wajibu wa wanasayansi kuonesha madhara na kutafuta suluhu ambazo zitapaswa kufanyiwa kazi na viongozi husika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sera, mipango na mikakati mingi ya Jumuiya ya Kimataifa inashindwa kutekelezwa kwa umakini mkubwa kutokana na kukosekana kwa utashi wa kisiasa ili: kudhibiti mashindano ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha; kusitisha vita na kinzani mbali mbali, ili hatimaye, kuwekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani na teknolojia rafiki; kwa kuhakikisha kwamba: watu wengi zaidi wanapata maji safi na salama kama sehemu muhimu ya maboresho ya afya zao; uhakika wa chakula na lishe bora pamoja na huduma msingi za afya. Yote haya ni kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi yanayohitaji mtaji mkubwa, lakini zaidi utashi wa kisiasa.

Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 12 Novemba 2018 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi za Kipapa za Sayansi wanaofanya mkutano wao wa mwaka kuanzia tarehe 12 - 14 Novemba 2018. Baba Mtakatifu anasema, katika miaka ya nyumba, sayansi ilijitwalia nafasi ya kujiendeshea shughuli zake kwa kujitegemea, kiasi hata cha kubeza tunu msingi za maisha ya kiroho, hali ambayo ilionekana kuhatarisha maendeleo ya wengi. Ni kweli kwamba, sayansi na teknolojia vina nafasi ya pekee katika maisha ya watu, lakini pia: tunu msingi za maisha, tamaduni na mapokeo ya watu yanachangia pia katika ukuaji wa sayansi inayopania kumkirimia mwanadamu furaha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kuhakikisha kwamba tunu msingi za maisha ya watu ambazo ni nguzo zinazowafungamanisha watu, jamii na sayansi zinadumishwa ili kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani kwa ajili ya mafao ya wengi. Majadiliano katika ukweli na uwazi na mang’amuzi ni mambo msingi yanayoweza kuisaidia sayansi kupambana na changamoto zinazoweza kumwandama mwanadamu kwa siku za usoni, hali inayohitaji uwajibikaji wa jumla kutoka kwa jumuiya ya wana sayansi pamoja na kuzingatia tunu msingi za maisha ya kiroho pamoja na kutambua uwepo wa Mungu. Wanasayansi wanapaswa kutambua kwamba, wao ni vyombo na wahudumu wa familia ya binadamu na maendeleo yake fungamani.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, athari za mabadiliko ya tabianchi, tishio la amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa kutokana na mashindano ya kutengeneza na kulimbikiza silaha za kinyuklia ni mambo yanayopaswa kutekelezwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema. Hii inatokana na ukweli kwamba, silaha za kinyuklia zinaweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya kazi za binadamu na madhara yake ni makubwa sana katika: ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.

Tafiti kadhaa za kisayansi zinaonesha kwamba, ongezeko kubwa la joto duniani kwa miaka ya hivi karibuni ni matokeo ya ongezeko la hewa ya ukaa angani, matumizi makubwa ya nishati mafuta pamoja na ukataji miti ovyo! Ni wajibu wa wanasayansi kuonesha madhara na kutafuta suluhu ambazo zitapaswa kufanyiwa kazi na viongozi husika; kwa kuendelea kuwekeza katika teknolojia rafiki, hali ambayo inahitaji ushirikiano katika masuala ya: fisikia, kemia na baiyolojia; hali ya hewa na masuala ya kijenetiki kama sehemu muhimu sana ya huduma kwa familia ya binadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, leo hii watu wengi wanataka kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii yao; kwa kukazia haki msingi za binadamu; kwa kupambana na: utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, kazi za shuruti, ukahaba; mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu. Taasisi za Kipapa za Sayansi zimekuwa mstari wa mbele katika mapambano haya na Baba Mtakatifu Francisko anasema, yuko pamoja nao hadi kieleweke! Bado kuna haja ya kujifunga kibwebwe ili kupata maendeleo endelevu na fungamani yatakayosaidia kukomesha baa la njaa na utapiamlo duniani; watu kuwa na uhakika wa maji safi na salama; mambo ambayo yanahitaji mabadiliko katika mfumo na mtindo wa maisha, lakini zaidi ni utashi wa kisiasa.

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema, Kanisa linawataka wanasayansi kujikita katika kanuni maadili, amana na urithi wa binadamu; kuchangia katika huduma ya maendeleo endelevu na fungamani pamoja na kurithisha ujuzi na maarifa katika masuala ya: tafiti, chakula na lishe, afya, elimu, mawasiliano, ustawi na amani. Tafiti zao zisaidie watu kupata chakula na lishe ya kutosha; maji safi na salama; afya bora na ustawi na kwamba, sera za kisiasa na kiuchumi zilenge ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza. Haya ndiyo matumaini ya familia ya binadamu kwa wanasayansi!

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni Dr. Joachim von Braun aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Rais mpya wa Taasisi za Kipapa za Sayansi. Ni kiongozi aliyebobea katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini duniani; balaa la njaa, sera za mabadiliko chanya ya kisayansi na teknolojia kama chombo cha huduma!

Papa: Taasisi za Kisayansi
13 November 2018, 17:27