Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Tema ya Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani 2019: "Siasa safi ni huduma ya amani" Papa Francisko: Tema ya Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani 2019: "Siasa safi ni huduma ya amani" 

Papa Francisko: Siku ya Kuombea Amani Duniani 2019: Siasa safi ni huduma ya amani!

Maadhimisho ya Siku ya 52ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani”. Siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu pia ana adhimisha Siku ya Kuombea Amani Duniani. Maadhimisho ya Siku ya 52 kwa Mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani”. Siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi yanayowashirikisha wadau mbali mbali mbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani.  

Siasa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu na kwamba, siasa safi hutekelezwa kwa kufuata katiba, sheria na kanuni maadili; mambo msingi katika kukuza na kudumisha misingi ya amani, haki, ustawi na maendeleo ya wengi. Siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo katika jamii; ni matunda ya ukomavu yanayojikita katika uongozi bora, maridhiano, utawala wa sheria, uvumilivu, uaminifu na bidii. Kamwe tofauti za kiitikadi kisiwe ni chanzo cha vita, kinzani, vurugu na mipasuko ya kijamii inayowatumbukiza watu kwenye majanga na maafa makubwa!

Siku ya Kuombea Amani Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu  Paulo VI, tarehe Mosi, Januari 1968. Mtakatifu Yohane XXXIII katika Wosia wake wa Kitume, Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anakaza kusema amani ya kweli inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Naye Mtakatifu Paulo VI anasema, amani ni jina jipya la maendeleo endelevu na fungamani. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani duniani kwa kuzingatia utu wa binadamu na haki zake msingi!

Ujumbe Baba Mtakatifu kwa ajili ya Siku ya Kuombea Amani Duniani hutumwa kwa wakuu wa nchi na Jumuiya ya Kimataifa na pia ujumbe huu huonesha dira na mwelekeo wa utendaji wa shughuli za kidiplomasia zitakazotekelezwa na Vatican. Mtumishi wa Mungu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania aliwahi kusema kwamba, ili nchi iweze kuendelea na watu wake kufurahia maendeleo yao, inahitaji mambo makuu manne: watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Siasa safi inajikita katika dhamana ya kuwawakilisha watu kikamilifu!

Papa: Amani 2019

 

 

06 November 2018, 11:49