Tafuta

Vatican News
Katika kipindi cha Mwaka 2017- 2018 kuna Makardinali na Maaskofu 154 waliofariki dunia. Katika kipindi cha Mwaka 2017- 2018 kuna Makardinali na Maaskofu 154 waliofariki dunia.  (AFP or licensors)

Mama Kanisa anawakumbuka Makardinali na Maaskofu 154 waliofariki duniani kati ya mwaka 2017-2018

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna jumla ya viongozi wa Kanisa 154 waliofariki dunia. Kuna Makardinali tisa kati yao ni Kardinali Jean- Louis Tauran, aliyekuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Kutoka Barani Afrika, Kanisa linawakumbuka kwa namna ya pekee Maaskofu 13. Kutoka Afrika Mashariki na Kati ni Maaskofu 6.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, Kristo Yesu ameshinda mauti! Kila anayemwamini maisha yake yatapyaishwa na upendo wa huruma ya Baba kwa ajili ya maisha ya heri na uzima wa milele. Kila mwaka ifikapo tarehe 2 Novemba na zaidi sana mwezi Novemba ni kipindi ambacho Mama Kanisa anatualika kwa ajili ya kuwaombea marehemu walioko toharani. Huo ndio utajiri wa Kanisa linapogawa mastahili ya Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu kwa wahitaji walioko safarini kuelekea mbinguni kwa Baba mwenye huruma na mapendo!

Maana ya Kikristo ya Kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani katika: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, ambaye ndani yake mna tumaini moja la maisha ya uzima wa milele. Kwa Mkristo siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Ubatizo, “kufanana” kamili na “sura ya Mwana”, kulikotolewa kwa mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme wa Mbinguni, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi!

Kifo ni jambo linalosababisha majonzi na machungu, lakini kwa waamini wenye imani na matumaini hawana haja ya kuogopa Fumbo la Kifo katika maisha yao, kwani wanaunganishwa kwa namna ya pekee na Kristo Yesu, aliyeshinda dhambi na mauti! Baba Mtakatifu Franciko, Jumamosi, tarehe 3 Novemba 2018, majira ya saa 5:30 kwa saa za Ulaya, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha mwaka 2017 - 2018.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna jumla ya viongozi wa Kanisa 154 waliofariki dunia. Kuna Makardinali tisa kati yao ni Kardinali Jean- Louis Tauran, aliyekuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Kutoka Barani Afrika, Kanisa linawakumbuka kwa namna ya pekee Maaskofu 13. Kutoka Afrika Mashariki na Kati ni Maaskofu 6, kati yao ni Askofu Cornelius Kipng’eno Arap Korie wa Jimbo la Eldoret, Kenya; Askofu mstaafu Vincent Mojwok Nyiker wa Jimbo Katoliki la Malakal, Sudan ya Kusini, Askofu Emmanuel Kanyama, Jimbo Katoliki la Dedza, Malawi; Askofu Jean Damascene Bimenyimana, Jimbo Katoliki la Kyangugu, Rwanda, Askofu Mstaafu Joseph Oyanga, Jimbo Katoliki la Lira, Uganda na mwishoni ni Askofu mstaafu Nestorius Timanywa wa Jimbo Katoliki Bukoba, Tanzania.

Papa: Misa Makardinali
02 November 2018, 16:03