Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Mambo ya Nyakati za Mwisho: Jiwekeeni hazina kwa matendo ya huruma. Papa Francisko: Mambo ya Nyakati za Mwisho: Jiwekeeni hazina kwa matendo ya huruma.  (ANSA)

Papa Francisko: Mambo ya Nyakati za Mwisho: Jiwekeeni hazina kwa matendo ya huruma

Yesu katika ufafanuzi wa Mambo ya Nyakati za Mwisho, anawarejesha wanafunzi wake kuhusu kazi ya uumbaji kadiri ya mpango wa Mungu; alama ya uhai, lakini jua kutiwa giza, mwezi kushindwa kutoa mwanga, nyota za mbinguni kuanguka na nguvu za mbinguni kutikisika ni alama ya mwisho wa nyakati, Kristo Yesu atakapokuja katika utukufu wake pamoja na watakatifu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXXIII ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa inajikita katika Mambo ya Nyakati za Mwisho yaani: Kifo, Hukumu, Jehanamu na Paradiso. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 18 Novemba 2018 amesema, Kristo Yesu aliwafundisha wanafunzi wake mambo ya mwisho wa nyakati, kama angalisho la kuwataka wautumie vyema muda walionao sasa, kwa kukesha, tayari kutoa hesabu ya matendo yao hapa duniani.

Papa Francisko anasema, Yesu katika ufafanuzi wa Mambo ya Nyakati za Mwisho, anawarejesha wanafunzi wake kuhusu kazi ya uumbaji kadiri ya mpango wa Mungu; alama ya uhai, lakini jua kutiwa giza, mwezi kushindwa kutoa mwanga, nyota za mbinguni kuanguka na nguvu za mbinguni kutikisika ni alama ya mwisho wa nyakati, Kristo Yesu atakapokuja katika utukufu wake pamoja na watakatifu wote. Hii ndiyo siku ile ambayo wafuasi wake wataweza kuiona Uso wake ukingara utukufu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu; Uso wa upendo na ukweli.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, historia ya jumuiya kama ilivyo historia ya mtu binafsi ina maana ya pekee na ni matunda ya maamuzi ya kweli. Yesu anasema, kila historia ya maisha ya jamii na watu binafsi ina hatima na lengo linalopaswa kufikiwa, yaani kukutana na Mwenyezi Mungu milele yote. Kumbe, hakuna sababu ya kuwa na hofu wala wasi wasi ya jinsi atakavyokuja Siku ile ya Mwisho kwani kila kitu kimefichika katika Fumbo la Baba wa milele. Lakini ikumbukwe kwamba, mbingu na nchi zitapita, lakini maneno ya Kristo Yesu hayatapita kamwe!

Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, maneno ya Kristo Yesu yanakuwa ni mwanga unaoyaangazia maisha yao badala ya kujiamini kipumbavu. Baba Mtakatifu anawaalika waamimini kujiachilia bila ya kujibakiza katika upendo wa Baba wa milele sanjari na kujiaminisha kwenye huruma yake isiyokuwa na mipaka. Hakuna mtu awaye yote anayeweza kuzikwepa siku za mwisho wa nyakati. Nguvu ya fedha na uchumi inayowapatia baadhi ya watu kiburi cha kudhani kwamba, wanaweza kununua kila kitu na kila mtu, “haitafua dafu tena”. Waamini watakwenda mbele ya Mwenyezi Mungu wakiwa na shehena ya matendo ya huruma waliyotekeleza wakiwa hapa duniani.

Baba Mtakatifu anahitimisha tafakari yake kwa kumwomba Bikira Maria, ili awasaidie waamini kutambua kwamba, hapa duniani ni wapita njia, wanayo mapungufu yao ya kibinadamu, ili awasaidie kujiwajibikia wenyewe, jirani na dunia katika ujumla wake.

Papa: Mambo ya Nyakati za Mwisho

 

18 November 2018, 10:39