Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Watawa ni mashuhuda na manabii wa matumaini! Papa Francisko: Watawa ni mashuhuda na manabii wa matumaini!  (ANSA)

Papa Francisko: Watawa ni mashuhuda na manabii wa matumaini!

Kanisa linawahitaji manabii wa matumaini, watu wasiokata tamaa licha ya kupungua kwa idadi ya miito duniani pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watawa wazee; kuna changamoto za ukwasi na hali ngumu ya kiuchumi; utandawazi, utamadunisho na mwelekeo wa mashirika haya kimataifa; ubinafsi bila kusahau changamoto za kijamii zinazobeza maisha ya kitawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Hispania, CONFER, kuanzia tarehe 13-15 Novemba 2018 linafanya mkutano wake mkuu, kielelezo makini cha umoja na mshikamano wa kidugu katika Kristo Yesu, wakati wa raha na shida, tayari kupiga moyo konde na kuyaangalia ya mbeleni katika maisha ya kitawa na kimisionari nchini Hispania kwa moyo wa imani, matumaini na mapendo. Huu ni muda kwa watawa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kuwashangaza pamoja na kuwasaidia kutoka katika ubinafsi wao wa kiakili na maisha ya kiroho, tayari kutambua na kuambata uwepo wa Mungu katika maisha yao!

Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyoliandikia Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Hispania, CONFER, analifafanulia juu ya mpango wa Mungu katika maisha na utume wake; mpango ambao unafumbatwa katika matumaini, wakitambua fika kwamba, pale wanapomwita Mwenyezi Mungu kwa moyo wa unyenyekevu anawasikiliza na kuwajibu, kwani anataka wajenge na kudumisha umoja na mshikamano kati yao, daima wakiendelea kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya maisha na utume wao, hata katika hali ya ukimya. Maisha ya kitawa na kazi za kitume kwa sasa yanakabiliwa na changamoto pevu, lakini bado kuna fursa kedekede, ari na mwamko kwa kutambua kwamba, hata leo hii maisha ya kitawa yana maana sana katika utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa linawahitaji manabii wa matumaini, watu wasiokata tamaa licha ya kupungua kwa idadi ya miito duniani pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watawa wazee; kuna changamoto za ukwasi na hali ngumu ya kiuchumi; utandawazi, utamadunisho na mwelekeo wa mashirika haya kimataifa; ubinafsi bila kusahau changamoto za kijamii zinazobeza maisha ya kitawa na hivyo kuonekana kana kwamba, yamepitwa na wakati! Matumaini yawawezeshe watawa kumwomba Bwana wa mavuno ili aweze kupeleka watenda kazi wema na watakatifu katika shamba lake, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji.

Changamoto kubwa anasema Baba Mtakatifu, ni kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya, ili kuwashirikisha ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Ni dhamana kwa watawa kuwaaminisha vijana kuwa wito wao ni  muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, jambo linalohitaji wongofu wa ndani, ili kumpatia nafasi Roho Mtakatifu kutenda kadiri anavyotaka! Hapa watawa wanapaswa kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha yao.

Bikira Maria katika maisha yake, aliyatafakari na kuyahifadhi matendo makuu ya Mungu katika sakafu ya moyo wake, awasaidie watawa kuwa na matumaini katika maisha na wito wao, daima wakijitahidi kuchuchumilia utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Watambue udhaifu na umaskini wao, lakini daima wawe na imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu, anayewapenda upeo. Watawa waishi kwa ajili pamoja na Kanisa, kwa kutoka huko walikojifungia katika ubinafsi, tayari kushirikiana na kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa  jamii na wale waliokata tamaa katika maisha, lakini wanasubiri “cheche za mwanga wa Injili”.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna changamoto pevu katika maisha na utume wa kitawa zinazohitaji majibu na maamuzi magumu yanayopaswa kujikita katika toba na wongofu wa kimisionari, tayari kusoma alama za nyakati sanjari na kuendelea kuwa waaminifu kwa Injili na upendo wa Mungu katika maisha yao. Maamuzi magumu, endelevu na fungamani, yafanyike baada ya sala na tafakari ya kina; mang’amuzi ya kijumuiya pamoja na majadiliano katika ukweli na uwazi na Askofu mahalia.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kuwataka watawa kujifunza kuishi kwa unyenyekevu, huku wakiwa na matumaini kwa kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini!

Papa: Confer 2018

 

 

14 November 2018, 09:53