Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Jengeni madaraja ya udugu na majadiliano! Papa Francisko: Jengeni madaraja ya udugu na majadiliano!  (ANSA)

Papa Francisko: Jengeni madaraja ya udugu na majadiliano!

Haya ni madaraja ya udugu kati ya Makanisa na Jumuiya za Kikristo yanayohamasishwa na Roho Mtakatifu ili kutembea kwa pamoja kwa ajili ya huduma ya amani na haki. Ni madaraja ya majadiliano na waamini wa dini mbali mbali, ili kujenga mahusiano yanayosimikwa katika kuheshimiana na kuaminiana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 30 Novemba, 2018 amekutana na kuzungumza na Wanachama wa Chama cha Utume wa Shahbaz Bhatti kutoka Pakistan kama kielelezo cha mshikamano wake na wale wote wanaoishi na kuteseka katika mazingira tete. Lakini wakumbuke kwamba, sadaka na ujasiri wao ni chachu ya matunda ya matumaini, sawa na mbegu ya ngano inayozikwa ardhini, inakufa na hatimaye kuzaa matunda mengi. Baba Mtakatifu anasema, haya ni matunda ya: majadiliano, upatanisho, nguvu, ujasiri na unyenyekevu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, moja ya matunda ya mateso na mahangaiko ya Wakristo ni kuendelea kujiunga katika vikundi na vyama, ili kujenga madaraja yanayovuka lugha, tamaduni na dini. Haya ni madaraja ya udugu kati ya Makanisa na Jumuiya za Kikristo yanayohamasishwa na Roho Mtakatifu ili kutembea kwa pamoja kwa ajili ya huduma ya amani na haki. Ni madaraja ya majadiliano na waamini wa dini mbali mbali, ili kujenga mahusiano yanayosimikwa katika kuheshimiana na kuaminiana.

Kilio chao cha mshikamano kimepata jibu makini kutoka nchini Italia, kwa kuwahusisha viongozi wa Makanisa pamoja waamini wenyewe. Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu wa kiinjili unaounganisha ujasiri na unyenyekevu, ili kuwapatia watuhumiwa wa shutuma za uwongo msaada, sanjari na kuendelea kujifunga kibwebwe kupambana na umaskini na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Kwa njia ya sala na mshikamano fungamani, waendelee kuwasaidia ndugu zao sehemu mbali mbali za Pakistan; watu ambao bado wanatengwa na kudhulumiwa.

Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kuwa ni mashuhuda wa Shahbaz Bhatti anayeng’aa kama mashuhuda wa imani wa nyakati hizi, wanaounganishwa kwa imani na ujasiri kwa Kristo Yesu, ili kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo, mahali penye chuki na uhasama. Watambue kwamba, hii kimsingi ni kazi ya Roho Mtakatifu, kumbe waendelee kumwomba Bikira Maria, ili awasaidie kuwa wasikivu kwa Roho Mtakatifu!

Shahbaz Bhatti

 

30 November 2018, 15:31