Tafuta

Vatican News
Kardinali Fernando Filoni akiwa nchini Angola Kardinali Fernando Filoni akiwa nchini Angola 

Kardinali Filoni akutana na kuzungumza na familia ya Mungu nchini Angola

Kardinali Filoni amekutana na kuzungumza na familia ya Mungu, kutoka Jimbo Katoliki la Luanda, Caxito na Viana na kuwataka kuendelea kupyaisha maisha yao kwa kukutana na Kristo Yesu katika: Sala, Sakramenti, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji na ushuhuda katika mchakato wa uinjilishaji mpya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 18 Novemba 2018, Siku ya II ya Maskini Duniani, kitakuwa ni kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST. Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, atakutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu. Jumapili iliyopita, tarehe, 11 Novemba 2018 Kardinali Filoni amekutana na kuzungumza na familia ya Mungu, kutoka Jimbo Katoliki la Luanda, Caxito na Viana na kuwataka kuendelea kupyaisha maisha yao kwa kukutana na Kristo Yesu katika: Sala, Sakramenti, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji na ushuhuda makini katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo!

Tarehe 12 Novemba 2018, Kardinali Filoni amekutana na kuzungumza na Maaskofu wanaotoka Jimbo kuu la Saurimo na kuwataka kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, ili kuendeleza Kanisa la Kristo nchini Angola. Ukuaji wa Kanisa nchini Angola uende sanjari ya miundo mbinu ya uinjilishaji, kwa kuwashirikisha watawa na waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la waamini wanaoshiriki katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, wanaoshiriki kikamilifu katika Mafumbo ya Kanisa na mshikamano unaojionesha wakati wa shida na magumu.

Kardinali Fernando Filoni katika siku yake ya kwanza nchini Angola, amelitaka Kanisa kuwahamasisha waamini ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa kuendeleza kazi ya uinjilishaji iliyofanywa na wamisionari waliojisadaka na kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Injili kwa familia ya Mungu nchini Angola. Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST inafanyika baada ya kuhitimisha mwezi Oktoba, uliotengwa rasmi na Mama Kanisa kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari; Kanisa limemaliza maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, changamoto na mwaliko wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kujibu matamanio halali ya vijana sanjari na kuendelea kujikita katika toba na wongofu wa kimisionari.

Lengo la maadhimisho haya ni kuiwezesha familia ya Mungu nchini Angola, Sao Tome na Principe kukuza na kudumisha ari na mwamko wa utume wa kimisionari, kwa kuonesha upendo kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kujizatiti katika mchakato wa uinjilishaji. Wakleri na watawa nchini Angola watambue kwamba, wao ni watu wa Mungu wanaopaswa kukita maisha yao katika sala ili kutekeleza vyema dhamana na utume wao kwa watu wa Mungu.

Kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu yanayoendelea kulichafua Kanisa sehemu mbali mbali za dunia, kwa kukazia zaidi mashauri ya Kiinjili yanayofumbatwa katika: Utii, Ufukara na Usafi kamili. Hizi ni nyenzo msingi katika kupyaisha shughuli za kichungaji na kimisionari nchini Angola na kwamba, wao watambue kuwa ni viongozi wa jumuiya ya waamini, kumbe wanapaswa kujitosa bila ya kujibakiza kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na upendo kama alivyofanya Kristo mwenyewe kwa Kanisa lake!

Kardinali Fernando Filoni akizungumza na Maaskofu kutoka Jimbo kuu la Saurimo kuwataka kujenga na kudumisha urika, umoja na mshikamano kati yao ili kuendeleza mchakato wa kazi ya uinjilishaji nchini Angola. Amekazia baadhi ya vipaumbele katika maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu ili kweli watu wa Mungu waweze kuwa ni mwanga na chumvi kwa njia ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha yao. Hata kama siasa ni sehemu ya vinasaba vya uinjilishaji nchini Angola, lakini haiwezi kupewa msukumo wa pekee, bali wahakikishe kwamba, matatizo na changamoto za maisha na utume wa Kanisa zinapewa ufumbuzi wa kudumu.

Maaskofu wawe makini katika uteuzi wa vijana wanaotaka kujiunga na maisha na wito wa kipadre na kitawa; malezi awali, endelevu na fungamani yatolewe kwa majandokasisi wanaojiandaa kuwa Mapadre. Utume wa familia na vijana upewe kipaumbele cha pekee ili kuwasaidia waamini kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kardinali Filoni amekiri uwepo wa mazingira magumu na tete kwa wakleri na watawa, lakini, wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanakita maisha yao katika kanuni maadili, sheria na taratibu za Kanisa.

Kardinali Fernando Filoni anasema, kinzani na mipasuko ya ndani; ukabila, ushirikina, ukata ni kati ya “magonjwa ambayo” Maaskofu katika kutekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu wanapaswa kuyavalia njuga ili kamwe yasiendelee kulichafua Kanisa la Kristo nchini Angola. Malezi na majiundo ya Kipadre yapewe kipaumbele cha kwanza; shughuli za malezi na majiundo seminarini zisimamiwe barabara na Maaskofu na kwamba, Kanisa liendelee kujielekeza zaidi katika majiundo makini kwa waamini walei, ili waweze kwa njia ya maisha yao, waweze kuyatakatifuza malimwengu. Mwishoni, Kardinali Fernando Filoni amaewataka Maaskofu Katoliki nchini Angola kuhakikisha kwamba mchakato wa uinjilishaji mpya unakwenda sanjari na utamadunisho, ili kuondokana na mila, desturi na tamaduni zinazosigana na tunu msingi za Kiinjili.

Angola
13 November 2018, 16:23