Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB limemwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB limemwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko 

Barua ya Maaskofu wa Marekani kwa Papa Francisko

Maaskofu nchini Marekani wameamua kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia zilizoikumba Marekani kwa siku za hivi karibuni, kiasi hata cha kuchafua maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Marekani.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, katika mkutano wake ulioanza Jumatatu, tarehe 12 Novemba 2018, limemwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko, kumshukuru kwa ujumbe aliowaandikia wakati wa “Encuentro V” yaani “Mkutano wa V” uliofanyika huko Texas, Marekani pamoja na kumhakikishia kwamba, watashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya II ya Maskini Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Maskini huyu aliita na Bwana akamsikia”. Kwa mwaka huu siku hii inaadhimishwa, Jumapili, tarehe 18 Novemba 2018.

Maaskofu wanasikitishwa sana na vitendo vya kibaguzi vilivyojitokeza nchi mwao hivi karibuni na kusababisha vifo vya watu kadhaa! Maaskofu nchini Marekani wameamua kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia zilizoikumba Marekani kwa siku za hivi karibuni, kiasi hata cha kuchafua maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Marekani. Maaskofu wanasema, Mkutano wa V uliofanyika huko Texas, ilikuwa ni fursa ya kukutanisha tamaduni za waamini kutoka Amerika ya Kusini, ili ziweze kuadhimishwa na Kanisa kama sehemu ya mchakato wa utamadunisho nchini Marekani.

Maaskofu wanapenda kuungana na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Pili ya Maskini Duniani ambamo anakazia kwa namna ya pekee: Umuhimu wa kusikiliza kilio, kujibu na kuokoa. Maaskofu kama wachungaji, wanapenda hata wao kujikita katika mchakato huu, kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana yao, changamoto kutoka kwa Kristo Mchungaji mwema. Maaskofu wanasema, wanaendelea kutafakari ili kukitafutia majibu kilio cha maskini mamboleo.

Maaskofu wanasikitika na kuomba msamaha kutokana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ambayo imewagusa na kuwatikisa baadhi ya Maaskofu nchini Marekani. Kwa sasa wameamua kujizatiti zaidi ili kupambana na kashfa hii pamoja na kuendelea kubainisha sera na mikakati ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Tema hii itachambuliwa kwa kina na mapana wakati wa mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Duniani, utakaofanyika mwezi Februari, 2019. Maaskofu wanakumbushwa kwamba, wao ni vyombo vya uponyaji!

Maaskofu wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa barua aliowaandikia watu wa Mungu nchini Marekani mintarafu kashfa ya nyanyaso za kijinsia ambazo zimeacha makovu makubwa katika maisha ya watu na kama kielelezo cha matumizi mabaya ya madaraka. Maaskofu wanamwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kupambana dhidi ya kashfa za nyanyaso za kijinsia. Maaskofu katika mkutano wao wanasema, wanaendelea kusikiliza kwa makini hotuba za wataalam na kuuliza maswali, ili kuweza kupata ufafanuzi zaidi.

Maaskofu wanaendelea kutekeleza dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, ili hatimaye, tafakari iliyoanza kunako mwaka 2002 iweze kuzaa matunda ya “Mwongozo wa Kuwalinda Watoto na Vijana”. Licha ya Maaskofu kuivalia njuga kashfa ya nyanyaso za kijinsia nchini Marekani, lakini bado wanawajibika kudumisha ukweli na uwazi, ili wahusika waweze kushughulikiwa kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa na zile za nchi katika ujumla wake. Maaskofu wasipotekeleza vyema dhamana na wajibu wao, matokeo yake ni kashfa kama hizi kufumuliwa na vyombo vya habari na hivyo serikali kuwajibika kisheria!

Maaskofu: USA: Papa
14 November 2018, 10:09