Tafuta

Vatican News
Vijana wa Sinodi wamfanyia Baba Mtakatifu Sherehe ya shukrani! Vijana wa Sinodi wamfanyia Baba Mtakatifu Sherehe ya shukrani!  (Vatican Media)

Sinodi: Vijana wamfanyia Papa Francisko sherehe ya shukrani

Vijana katika ujumbe wao wanasema, wanapenda kuungana na Baba Mtakatifu pamoja Maaskofu wao mahalia katika raha na shida; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vijana wanaohudhuria Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, Ijumaa jioni, tarehe 26 Oktoba 2018, wamemfanyia sherehe Baba Mtakatifu Francisko kama shukrani inayobubujika kutoka nyoyoni mwao, kwa kuwapatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake. Mababa wa Sinodi wakiongozwa na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi, aliyecharaza kinanda, akikumbukia enzi zake, waliungana na vijana kumshukuru Baba Mtakatifu kwa maadhimisho ya Sinodi ya vijana! Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwapatia wote baraka zake za kitume na kuwaambia kwa sasa, sasa Sinodi imenoga!

Vijana katika ujumbe wao kwa Papa Francisko wanasema, wanapenda kuungana na Baba Mtakatifu pamoja Maaskofu wao mahalia katika raha na shida; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo! Vijana wameonesha ukaribu wao kwa Baba Mtakatifu ambaye katika kipindi cha maadhimisho ya Sinodi ameonesha moyo wa ukarimu, upendo na hasa zaidi sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza kwa makini. Kwa pamoja wameweza kuandika historia ya maisha na utume wa Kanisa.

Vijana wanatamani kuona kwamba, wanapewa nafasi na fursa za kuweza kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, dhamana ambayo imetekelezwa kwa dhati kabisa na Baba Mtakatifu Francisko. Vijana wanasema, ulimwengu mamboleo unahitaji majibu mapya yanayofumbatwa katika nguvu ya upendo! Wanahitaji kuonjeshwa Injili ya Matumaini, ili waweze kuwa na furaha inayowawajibisha kuwa wakarimu kwa kutoa zaidi kuliko kupokea! Vijana wanataka kujisadaka katika mchakato utakaoiwezesha dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; kwa kujikita katika umoja, udugu, haki na upendo.

Vijana wanamwomba, Baba Mtakatifu kuendelea kukoleza safari ya mageuzi inayofumbatwa katika toba na wongofu wa kimisionari na kwamba, wako pamoja naye kwa njia ya sala. Vijana wanataka kuliona Kanisa likitoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni kama hospitali katika uwanja wa mapambano, linapaswa kuwa ni chemmchemi ya huruma na mapendo tayari kuganga kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini! Vijana wanasema, wao wako imara na ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa na sasa wanataka kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa jamii inayofumbatwa na utamaduni wa amani na mshikamano; jamii inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, ambao ni amana na utajiri wa Kanisa.

Katika maadhimisho ya Sinodi, Mababa wa Sinodi wamewachagua wajumbe 16 watakaounda Baraza la Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 kutoka katika Mabara matano, ili kuunda umoja na mshikamano wa Maaskofu, kama unavyofafanuliwa na Katiba Kitume kuhusu Sinodi, iliyotiwa mkwaju na Baba Mtakatifu Francisko, 15 Septemba 2018. Baba Mtakatifu anayo nafasi ya kuteua kiongozi mmoja kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, kadiri ya mwelekeo wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu itakayofuatia pamoja na wajumbe wanne ambao watashirikiana kufanya kazi kwa pamoja kama timu! Kumbe, kimsingi, Baraza la Sinodi litakuwa na wajumbe 21 na orodha yao itachapishwa pale itakapokuwa imekamilika rasmi!

Sinodi Vijana: Wajumbe
27 October 2018, 10:42