Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anakazia majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya ili kujenga umoja na mshikamano wa kijamii. Papa Francisko anakazia majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya ili kujenga umoja na mshikamano wa kijamii.  (AFP or licensors)

Papa Francisko kuongoza majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya 23 Oktoba 2018

Tarehe 23 Oktoba 2018 kama sehemu ya maadhimisho ya Sinodi, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza mdahalo kati ya vijana na wazee, utakaofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Augustinianum kilichoko mjini Roma kuanzia majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Ulaya ili kujenga umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sala na sadaka ya wazee ni muhimu sana kwani zinalitegemeza Kanisa, changamoto na mwaliko kwa wazee kuhakikisha kwamba, wanakuwa karibu na vijana ili kuwarithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Waendeleze majadiliano na watoto wadogo pamoja na vijana kwani katika maisha yao, wamebahatika kuwa na kumbu kumbu, ujuzi, maarifa na imani, wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya na kamwe wasijisikie kuwa ni watu waliopitwa na wakati.

Hii ndiyo changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” itakayohitimishwa hapo tarehe 28 Oktoba 218. Tarehe 23 Oktoba 2018 kama sehemu ya maadhimisho ya Sinodi, Baba Mtakatifu ataongoza mdahalo kati ya vijana na wazee, utakaofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Augustinianum kilichoko mjini Roma kuanzia majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Ulaya.

Lengo ni kutaka kuonesha umuhimu wa wazee katika jamii na kwamba, ni kundi linalohitaji kupendwa, kuthaminiwa na kutunzwa. Wazee wamekuwa mstari wa mbele katika dhamana ya kurithisha imani, tamaduni na mapokeo katika Jamii. Hii ndiyo kazi ilivyoshuhudiwa na Wazee kama akina Anna wanaozungumziwa kwenye Maandakiko Matakatifu. Wazee ni kundi linaloshuhudia matumaini hata kwa vijana wa kizazi kipya!

Kutakuwepo na wawakilishi wa wazee na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta, Rais wa Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama pamoja na Padre Antonio Spadaro, SJ., Mkurugenzi mkuu wa Jalida la “Civiltà Cattolica” watashiriki kikamilifu. Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameendelea kujikita zaidi katika kukazia umuhimu wa majadiliano na mafungamano ya kijamii kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya. Matokeo yake, kuna mahojiano 250 yaliyofanywa kutoka katika nchini zaidi ya 30 na ambayo yamekusanywa na kuchapishwa katika kitabu. Kitabu hiki kinachojulikana kama “Sharing the wisdom of time” yaani “Kushirikishana busara ya nyakati” ni msaada mkubwa wa majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya. Kitabu hiki kimehaririwa na Padre Antonio Spadaro.

Baba Mtakatifu anawataka wazee kujifunza kutoka kwa wazee wenzao katika Maandiko Matakatifu, waliojizatiti kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hata katika uzee wao. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanamwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani mwao! Wazee watambue kwamba, wao ni mzizi wa maisha ya jumuiya, kumbe, ni wajibu wao kurithisha uzoefu na kumbu kumbu za maisha. Wazee wawasaidie watoto kung’amua maana ya maisha, tunu za maisha ya Kikristo na kiutu na kwamba, uzoefu wao, tayari ni shahada tosha kabisa katika maisha.

Wazee na wagonjwa waendelee kusali kwa ajili ya kuliombea Kanisa, watoto na vijana; waendelee kuwa karibu na Kanisa na waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, hadi dakika ya mwisho wa maisha yao! Vijana wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa unyenyekevu na wajitahidi kuzungumza kwa ujasiri kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kukuza sanaa na utamaduni wa kusikilizana na kusindikizana katika maisha.

Papa: Vijana na wazee

 

10 October 2018, 09:01