Tafuta

Vatican News
Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania, Furaha ya Injili! Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania, Furaha ya Injili! 

Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania: furaha ya Injili!

Tanzania inapomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya miaka 150 ya uinjilishaji ni wakati muafaka kwa waamini: Mosi, kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani; Pili, kutathmini safari hii ya miaka 150 katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania; Tatu ni kujipanga kwa ajili ya kuendelea kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa familia ya Mungu nchini Tanzania, wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa wamisionari waliojisadaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili nchini Tanzania, Jubilei ya miaka 100 ya wakleri nchini Tanzania sanjari na kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Tanzania ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican pamoja na mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania.

Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, katika mahojiano maalum na Vatican News wakati huu familia ya Mungu nchini Tanzania inapomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya miaka 150 ya uinjilishaji anasema, ni wakati muafaka kwa waamini: Mosi, kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani; Pili, kutathmini safari hii ya miaka 150 katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania; Tatu ni kujipanga kwa ajili ya kuendelea kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ndani na nje ya Tanzania.

Askofu mkuu mwandamizi anasema, Miaka 150 ya uinjilishaji nchini Tanzania ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya zawadi ya imani, kwa kutambua kwamba, Kanisa na Wakristo wote ni zawadi ya Mungu na nguvu injilishi. Wakristo wanapaswa kujitambua hivyo na waone fahari kuuishi Ukristo wao na kwa namna ambayo inaliimarisha Kanisa; kuwajenga, kumtukuza Mungu na binadamu kukombolewa!

Hiki ni kipindi cha kujitathmini kwa kutambua kwamba, safari ya miaka 150 si haba! Kanisa nchini Tanzania limetoka mbali. Ni wakati wa kujihoji kuhusu ukomavu wa Kanisa kulingana na miaka 150 ya imani: Tathmini hii ifanywe na mwamini mmoja mmoja, familia na Kanisa la Tanzania katika ujumla wake. Pili ni uimara wa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji kama njia muafaka ya kulipa fadhila na ukarimu wa wamisionari waliojitosa na kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Baada ya kupokea bure zawadi ya imani, sasa ni zamu ya watanzania kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ndani na nje ya Tanzania. Watanzania wawe ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji ndani ya Kanisa, Tanzania nan je ya Tanzania. Askofu mkuu Ruwa’ichi anatambua idadi kubwa ya wamisionari, yaani waamini walei, watawa na wakleri wanaoendelea kujisadaka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo sehemu mbali mbali za dunia. Ni wakati wa kufanya tathmini ya kina kuhusu uwezo wa kujitegemea na kulitegemeza Kanisa mahali kwa kuwa na mihimili ya uinjlishaji inayotosheleza walau mahitaji ya Kanisa mahalia pamoja na kuwa na nyenzo za kutosha katika huduma fungamani zinazogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa la Tanzania linahitaji rasilimali vitu na fedha ili kusongesha mbele mchakato mzima wa uinjilishaji.

Kanisa la Tanzania halina budi kutambua kwamba, limeanza kama Kanisa lenye kupokea rasilimali watu, fedha na vitu kwa ajili ya kuinjilishwa. Kumbe, miaka 150 ya uinjilishaji nchini Tanzania ni fursa muhimu kutambua kwamba, sasa waamini wanapaswa kulitegemeza Kanisa na ni aibu kwa Kanisa la Tanzania kuendelea kutegemea misaada kutoka nje kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Wakristo wa Tanzania wanadaiwa kwa haki kabisa kujitoa na kujitosa, ili kulitegemeza Kanisa, ili liweze kufanikisha mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anakaza kusema, Kanisa la Tanzania katika maadhimisho ya Miaka 150 ya uinjilishaji ni muda muafaka wa kujipanga ili kuweza kufanikisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Hii ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji unaogusa maisha ya mtu binafsi, familia, marika, makundi ya waamini na jamii ya watanzania katika ujumla wake. Ni mchakato unaowadai watanzania kuutekeleza kwa: kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu; kwa kusali, kutafakari; kuchambua na kupembua ili kubaini vipaumbele, sera na mikakati; nyakati na utekelezaji wake.

Miaka 150 ya Ukristo
31 October 2018, 14:45