Cerca

Vatican News
Papa Francisko awataka vijana kukita maisha yao katika sala na uinjilishaji Papa Francisko awataka vijana kukita maisha yao katika sala na uinjilishaji.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Vijana kiteni maisha katika sala na uinjilishaji

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Wajenge mazoea ya kusali kama njia ya kuzungumza na Mungu hasa zaidi kutoka katika undani wa maisha yao, daima wakikumbuka kwamba, jumuiya ya waamini iko nyuma yao katika uinjilishaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza na kuwashukuru vijana kutoka Jimbo Katoliki la Viviers, nchini Ufaransa, walioamua kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufanya hija kwenye masalia ya watakatifu mbali mbali kutoka Jimbo Katoliki la Rioja, nchini Argentina, kama kielelezo cha kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika huduma ya mapendo kwa maskini! Ni katika Jimbo la Rioja ambako Padre Longueville kutoka Jimbo Katoliki la Viviers alikouwawa, akiwa pamoja na wenzake: Padre Carlos, Wenceslao na Askofu Enrique, mashuhuda wa Kristo Yesu, aliyethubutu kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Wajenge mazoea ya kusali kama njia ya kuzungumza na Mungu hasa zaidi kutoka katika undani wa maisha yao, daima wakikumbuka kwamba, jumuiya ya waamini iko nyuma yao. Amelitaka Kanisa, kuwasaidia vijana ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao. Amewataka vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji, wakiwa na msukumo na ari mpya ya kimisionari, ili kuonja upendo wa Kristo unaotakasa na kuokoa, daima wakikimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama na nyota ya uinjilishaji mpya!

Baba Mtakatifu ameyasema hayo, Jumatatu, tarehe 29 Oktoba 2018 wakati alipokutana na kuzungumza na vijana wa Jimbo Katoliki la Viviers na kwa niaba yao, akawashukuru waamini wote wa Jimbo hili. Katika hija ya kufuata nyayo za mashuhuda hawa wa Injili, wamegundua ukuu na changamoto zinazoikabili mihimili ya Injili na marafiki wa Yesu ambaye anakaza kusema, hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi!

Baba Mtakatifu anafurahi na kuwashukuru kwa mang’amuzi na uzoefu wa sala uliofumbatwa katika: umoja, udugu na huduma huko Jimboni Rioja. Vijana wanaendelea kuhamasishwa kujikita zaidi katika njia ya Yesu anayetumikia, kwa kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie ili waweze kuwa kweli wajenzi wa madaraja katika watu na jirani kwa watu waliojeruhiwa na kutengwa ili kushuhudia upengo wa Baba wa milele na furaha ya Injili! Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka vijana wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mtakatifu Francois Regis, Mtakatifu Therese Couderc pamoja na Mwenyeheri Charles de Foucauld na hatimaye, kuwapatia waamini wa Jimbo Katoliki la Viviers baraka zake za kitume!

Vijana Ufaransa

 

30 October 2018, 11:09