Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: ujumbe kwa familia ya Mungu nchini Tanzania katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji Papa Francisko: ujumbe kwa familia ya Mungu nchini Tanzania katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji  (AFP or licensors)

Ujumbe wa Papa Francisko kwa familia ya Mungu nchini Tanzania!

Shukrani kwa wamisionari waliojisadaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili nchini Tanzania sanjari na jubilei ya miaka 100 ya wakleri nchini Tanzania; kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Tanzania ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican pamoja na mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi nchini Kenya, kuwa mwakilishi wake maalum katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji nchini Tanzania, yanayoongozwa na kauli mbiu: “Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji, furaha ya Injili. Kilele cha maadhimisho haya ni kuanzia tarehe 2-4 Novemba 2018. Kardinali Njue katika maadhimisho haya anaambatana na Padre Valentin Bayo, C.S.Sp pamoja na Padre Francis Kangwa, M. Afr.

Baba Mtakatifu katika Barua aliyoandika kwa lugha ya Kilatini kwenda kwa Kardinali Njue anagusia mambo makuu yafuatayo: Shukrani kwa wamisionari waliojisadaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili nchini Tanzania sanjari na jubilei ya miaka 100 ya wakleri nchini Tanzania; kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Tanzania ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican pamoja na mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania. Baba Mtakatifu anachukua fursa hii kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya furaha ya Injili nchini Tanzania, tangu mwaka 1868, Bagamoyo ulipoanza kuwa ni Mlango wa imani, kwa kuwaona Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu wakijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Wamisionari wa Roho Mtakatifu wakafungua njia ya uinjilishaji kwa kuanzia Bagamoyo na kufuatiwa na Shirika la Wabenediktini pamoja na Wamisionari wa Afrika. Kutokana na juhudi, ari na moyo wao wa kujisadaka, Injili ya Kristo ikaenea kwa haraka sehemu mbali mbali za Tanzania na hivyo kujikita katika akili na nyoyo za watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa kuliwezesha Kanisa Katoliki nchini Tanzania, kusherehekea Jubilei ya miaka 100 tangu lilipopata mapadre wake wazalendo. Hawa ni akina PadreAngelo Mwilabule, Celestin Kipanda, Ansgarius Kyakaraba pamoja na Wilbardi Mupapi. Katika orodha hii, Baba Mtakatifu anamkumbuka pia Kardinali Laurian Rugambwa, Kardinali wa kwanza Mwafrika, aliyeteuliwa na Mtakatifu Yohane XXIII kunako mwaka 1960.

Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa kuiwezesha Tanzania na Vatican kufanya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu nchi hizi mbili zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia, hapo tarehe 11 Aprili kwa ridhaa ya Mtakatifu Paulo VI. Nchi hizi mbili zimeendelea kudumisha urafiki kwa kuheshimiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya pande hizi mbili. Baba Mtakatifu analipongeza Kanisa kwa kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Tanzania.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mbegu ya imani iliyopandwa miaka 150 iliyopita huko Bagamoyo imeliwezesha Kanisa la Tanzania kupata idadi kubwa ya waamini, wakleri na maaskofu wazalendo. Leo hii kuna majimbo makuu 6 yaliyogawanyika katika majimbo 29, kwa hakika, hii ni neema na kazi ya Mungu na ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Kanisa nchini Tanzania litaendelea kuchanua na imani kushuhudiwa ikimwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Katika kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji nchini Tanzania anasema Baba Mtakatifu, Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania alimwandia barua kuomba ushiriki wake katika kilele hiki kama kumbu kumbu endelevu ya kazi kubwa iliyofanywa na Padre Anthony Horner, lakini kutokana na umuhimu wa historia na utamaduni wa eneo hili, ameamua kumtuma Kardinali John Njue, kuwa mwakilishi wake maalum katika maadhimisho haya.

Baba Mtakatifu anawapongeza waamini wote waliobahatika kusikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa na kushuhudia kwao, changamoto ni kuendelea kushuhudia furaha ya Injili! Baba Mtakatifu anaitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kuendelea kuombea miito mbali mbali kwa kutambua kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Baba Mtakatifu anaiweka familia ya Mungu nchini Tanzania chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, watakatifu wote, lakini zaidi wamisionari! Mwishoni, anatoa baraka zake za kitume kwa Kanisa na waamini wanaoshiriki maadhimisho haya kwa upendo mkuu!

Papa: Tanzania
30 October 2018, 14:35