Tafuta

Vatican News
Watakatifu wapya ni watu waliothubutu kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Watakatifu wapya ni watu waliothubutu kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa.  (ANSA)

Watakatifu ni watu waothubutu kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa!

Watakatifu wote kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo VI na Oscar Romero, wamesadaka maisha yao kwa ajili ya Injili; wakawa karibu na maskini na watu wa Mungu, kielelezo cha upendo kwa Kristo Yesu na jirani zao. Hivi ndivyo walivyofanya pia watakatifu kama: Vincenzo Romano, Maria Caterina Kasper, Nazaria Ignazia, Francesco Spinelli na Nunzio Sulprizio.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa kuwatangaza watakatifu wapya saba, wakiwemo Papa Paulo VI na Askofu mkuu Oscar Romero, Jumamosi, jioni, tarehe 13 Oktoba 2018 amemtembelea Papa Mstaafu Benedikto XVI kwenye Monasteri ya Mater Ecclesiae, ili kumsalimia na kumtakia heri, wakati huu Mama Kanisa anapomshangilia na kumtukuza Mungu kwa ushuhuda wa utakatifu wa maisha, aliyolikirimia Kanisa kwa njia ya watoto wake. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Paulo VI ndiye aliyemsimika Papa Mstaafu Benedikto XVI kuwa Kardinali kunako tarehe 27 Juni 1977.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, Jumapili ya XXVIII ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, tarehe 14 Oktoba 2018 sanjari na kuwatangaza watakatifu wapya ndani ya Kanisa amekazia kuhusu umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya waamini; upendo wa dhati unaofumbatwa katika sadaka ya maisha, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu anayetoa yote na kudai zaidi ili kuweza kupata furaha ya maisha ya uzima wa milele inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu kama walivyofanya watakatifu wapya waliotangazwa na Mama Kanisa kama kielelezo na mfano bora wa kuigwa!

Baba Mtakatifu anasema, Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu na lina ukali kuliko upanga ukatao kuwili, kwani linagusa undani wa mtu na hivyo kumletea mageuzi katika maisha. Kristo Yesu ndiye Neno wa Mungu aliye hai anayezungumza kutoka katika sakafu ya nyoyo za waamini wake. Huu ndiyo mwaliko na changamoto ya kumkimbilia ili kuweza kukutana na Kristo Yesu kama alivyofanya yule kijana tajiri anayesimuliwa katika Injili, ili kuweza kupata utimilifu wa maisha na kurithi uzima wa milele. Lakini, haitoshi kushika Sheria na Amri za Mungu, bali kujisadaka bila ya kujibakiza kama alama ya upendo na mshikamano wa dhati na Kristo Yesu.

Huu ni mwaliko wa kuuza vyote na kuanza kumfuasa Kristo kila siku ya maisha. Ndani ya Kristo, mwamini anakutana mubashara na Mwenyezi Mungu anayempenda daima na kumkirimia maana ya maisha na nguvu ya kuweza kujisadaka bila ya kujibakiza kama kielelezo cha upendo wa dhati. Yesu anawaalika waja wake kung’oa ndani mwao yale yanayosumbua nyoyo zao na kumkimbilia Yeye, muhtasari wa wema wote. Yesu katika mafundisho yake, ameonya kwamba, utajiri unaweza kuwa ni kikwazo kikubwa katika mchakato mzima wa wokovu kama anavyokaza kusema Mtakatifu Paulo kwamba, uchu wa fedha na mali ni shina la mabaya duniani na wala hakuna nafasi kwa Mungu na jirani!

Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua kwa kusema, Kristo Yesu anawakirimia waja wake yote na anawadai zaidi, kwani Kristo ndiye Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, aliyejisadaka na kuwa mtumishi wa wote, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake pale juu Msalabani, ndiyo maana anawataka wafuasi wake kujisadaka bila ya kujibakiza hata kidogo. Anawataka kufanya maamuzi magumu kwa kumpenda Mungu na jirani zao! Hii ni changamoto hata kwa Kanisa kuweza kujiuliza ikiwa kama linatangaza na kuhubiri mambo mema, au Kanisa ambalo ni mchumba mwaminifu wa Kristo linalojitosa katika upendo wake au Kanisa linataka kukumbatia malimwengu kama kielelezo cha usalama wake?

Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kuomba neema ya kujibandua na malimwengu, taratibu na miundo mbinu ambayo kamwe haikidhi tena mchakato wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, vinginevyo Kanisa litagubikwa na uchoyo, ubinafsi na machungu nyoyoni kama alivyoondoka yule kijana akiwa na huzuni kubwa moyoni mwake, hata baada ya kukutana na hatimaye, Yesu kumkazia macho kwa upendo. Huzuni ni kielelezo cha upendo butu katika maisha, hali inayomfanya mwamini kukosa furaha ya kweli.

Leo hii, Kristo Yesu anawaalika waamini kurejea tena katika kisima cha furaha, kwa kukutana naye, kwa kufanya maamuzi thabiti, kiasi hata cha kuthubutu kumfuasa bila ya kujibakiza kama walivyofanya watakatifu katika maisha na utume wao! Ndivyo alivyofanya Mtakatifu Paulo VI kwa kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili katika majadiliano, huduma kwa maskini pamoja na kuwa na mwono mpana zaidi katika maisha na utume wa Kanisa hata pale ambapo hakueleweka sana. Katika shida, magumu na changamoto za maisha, Mtakatifu Paulo VI ameshuhudia uzuri na furaha ya kumfuasa Kristo Yesu bila ya kujibakiza. Ni Baba wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, aliyeonesha moyo wa uchaji wa Mungu na hivyo kujitahidi kuishi kitakatifu wito kwa watu wote.

Watakatifu wote kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Oscar Romero, wamesadaka maisha yao kwa ajili ya Injili; wakawa karibu na maskini na watu wa Mungu, kielelezo cha upendo kwa Kristo Yesu na jirani zao. Hivi ndivyo walivyofanya pia watakatifu kama: Vincenzo Romano, Maria Caterina Kasper, Nazaria Ignazia, Francesco Spinelli na Nunzio Sulprizio.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata Mtakatifu Nunzio Sulprizio katika ujana wake ameonesha na kushuhudia ujasiri, moyo wa unyenyekevu kwa kukutana na Kristo Yesu katika mateso, ukimya na sadaka ya maisha pasi na kujibakiza hata kidogo. Watakatifu wote hawa kila mmoja kadiri ya hali na mazingira yake, ameweza kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yake bila ya kujibakiza, woga na makunyanzi! Ni watu ambao wamethubutu na kuacha yote katika maisha! Hawa ni mifano bora ya kuigwa katika maisha na ufuasi wa Kristo Yesu!

Watakatifu wapya
14 October 2018, 14:09