Cerca

Vatican News
Papa Francisko, Jumapili tarehe 14 Oktoba 2018 amewatangaza watakatifu wapya saba, mifano bora ya kuigwa na waamini. Papa Francisko, Jumapili tarehe 14 Oktoba 2018 amewatangaza watakatifu wapya wapya saba, mifano bora ya kuigwa na waamini.  (AFP or licensors)

Wasifu wa Mt. Paulo VI, Oscar Romero & Nunzio Sulprizio na wenzao!

Watakatifu Paulo VI, Askofu mkuu Oscar Romero na wenzao wametangazwa na Mama Kanisa, tarehe 14 Oktoba 2018 kuwa ni mifano bora ya kuigwa na familia ya Mungu katika huduma na utakatifu wa maisha. Ni waamini waliomtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa matendo yenye mvuto na mashiko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Paulo VI, Askofu mkuu Oscar Arnulfo Romero Galdamez; Mtakatifu Francesco Spinelli, Muasisi wa Shirika la Masista Waabuduo Sakramenti Kuu; Mtakatifu Vincenzo Romano, Padre wa Jimbo, Mtakatifu Maria Caterina Kasper; Bikira na mwanzilishi wa Shirika la Wahudumu wa Maskini wa Kristo Yesu pamoja na Mtakatifu Nazaria Ignazia wa Mtakatifu Theresa wa Yesu wametangazwa na Mama Kanisa, tarehe 14 Oktoba 2018 kuwa ni mifano bora ya kuigwa na familia ya Mungu katika huduma na utakatifu wa maisha. Ni waamini waliomtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa matendo yenye mvuto na mashiko.

Mifano yao bora ya maisha, urafiki wa kuungana na Mwenyezi Mungu; umeweza kuliangazia Kanisa na Ulimwengu mwanga wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, mambo msingi katika mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko. Wamekuwa ni mifano bora ya kuigwa kama watoto wateule wa Mungu na kamwe, hawakusita kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Mtakatifu Paulo VI ni kiongozi wa Kanisa aliyesimamia vyema mchakato wa maadhimisho na utekelezaji wa maazimio ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Akawa ni kiongozi wa kwanza wa Kanisa kufanya hija za kichungaji nje ya Italia ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro akatoa kipaumbele cha pekee kwa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia ya kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika haki, amani na maridhiano. Ni kiongozi aliyesimama kidete kutangaza, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Mtakatifu Oscar Armulfo Romero ni shuhuda wa Injili ya Kristo; mtetezi wa Kanisa, utu na heshima ya binadamu. Alikuwa ni chombo cha huruma, upendo, haki, upatanisho na amani ya kweli; mambo aliyotaka kuona yanamwilishwa nchini El Salvador. Ni matumaini ya familia ya Mungu nchini El Salvador kwamba, kifodini cha Askofu mkuu Oscar Romero kitaendelea kuzaa matunda ya umoja na mshikamano wa Kanisa; haki, amani, maridhiano na mafungamano ya kitaifa nchini El Salvador, kama sehemu ya mchakato ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki amani, utu na heshima ya binadamu.

Ni shuhuda aliyesimama kidete kuwalinda na kuwatetea maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi kwamba utu na heshima yao vikawekwa rehani. Mtakatifu Romero alitekeleza dhamana na wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Askofu, mintarafu Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Mtakatifu Nunzio Sulprizio anawaalika vijana watambue maisha yao ya ujana kuwa ni upendeleo na neema ya pekee. Ujana ni umri wa kutenda mema, ni neema ya kuwa na nguvu na muda wa kuboresha maisha bora: kiroho na kimwili. Kama ilivyo kwa Sakramenti ya Ubatizo, ujana ni hazina ya kulinda, kuenzi, kuelimisha, kukuza na kuiendeleza kwa ajili ya matunda bora na yanayodumu.

Hii ni changamoto kwa vijana kuwa ni chachu, chumvi na mwanga wa ulimwengu kwa njia ya maisha yao adili na manyofu badala ya kutopea katika mmong’onyoko wa maadili na utu wema; kwa kupenda sana anasa na starehe zinazowatumbukiza katika janga la utumwa mamboleo unaofifisha utu na heshima yao kama binadamu! Mtakatifu Sulprizio anaendelea kuichangamotisha jamii kuwatendea haki wafanyakazi, kwa kuboresha hali ya maisha, mazingira ya kazi yao; kuwasaidia kupambana na ukali wa maisha kwa kuwapatia mshahara unaokidhi mahitaji yao msingi pamoja na kuthamini utu na heshima yao! Wafanyakazi wajitahidi kumwilisha imani katika matendo.

Tukio hili la kihistoria ambalo linakwenda sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Kutokana na sababu za umri na afya kuwa na “mgogoro kidogo”, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI hakuweza kuhudhuria katika Ibada hii, ingawa amewasindikiza kwa sala zake. Ni matumaini ya watu wa Mungu kwamba, watakatifu hawa wapya watalisaidia Kanisa kuganga na kuponya makovu ya mipasuko ya mitazamo katika maisha na utume wa Kanisa, ili kweli Kanisa liweze kuendelea kuwa ni shuhuda wa Injili ya maisha, matumaini na amani kwa watu wa Mungu.

Wakati huo huo, Kardinali Rosa Chavez, Askofu mkuu wa San Salvador amethibitisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha nia ya kutembelea El Salvador, wakati atakapokua anakwenda kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanayongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38  Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mama wa Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu.

Watakatifu wa Mungu
14 October 2018, 13:49