Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika ujenzi wa madaraja ya amani kwa kuwashirikisha vijana! Papa Francisko anawataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika ujenzi wa madaraja ya amani kwa kuwashirikisha vijana!  (ANSA)

Papa Francisko: Jengeni madaraja ya amani kwa kuwahusisha vijana!

Baba Mtakatifu Francisko katika amekazia: umuhimu wa majadiliano ya kidini; madhara ya vita na vitendo vya kigaidi; waamini kama wajenzi wa amani na umuhimu wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu kwa makini kilio cha amani duniani na kwamba, vijana wanapaswa kushirikishwa katika ujenzi wa amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa kushirikiana na Jimbo kuu la Bologna, nchini Italia, kuanzia tarehe 14-16 Oktoba 2018 wanafanya mkutano wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “Madaraja ya Amani” kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa majadiliano ya kidini na kiekumene katika “Roho ya Assisi”. Mkutano huu unawajumuisha viongozi wa kidini, kisiasa na kitamaduni kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Lengo kuu ni kudumisha Injili ya amani na majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni muda wa kushirikishana changamoto za ujenzi wa amani mintarafu majadiliano katika ukweli na uwazi sanjari na kusikiliza shuhuda za watu walionja madhara ya vita pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Professa Marco Impagliazzo, Rais wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio anasema, katika mazingira na changamoto kama hizi kuna haja ya kujenga madaraja ya amani duniani. Mada zinazojadiliwa ni pamoja na: Ulaya na shida zake; Mshikamano kati ya vizazi; Majadiliano ya kidini; Mazingira: Udhibiti wa silaha; Dhamana na wajibu wa waamini walei nyakati za vita; Vita na mapigano Amerika ya Kusini; Hatima ya Bara la Afrika na hatimaye, Kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipoanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, yaani hapo tarehe 14 Oktoba 1978.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Matteo Maria Zuppi wa Jimbo kuu la Bologna wakati wa ufunguzi wa mkutano huu, Jumapili tarehe 14 Oktoba 2018 amekazia: umuhimu wa majadiliano ya kidini; madhara ya vita na vitendo vya kigaidi; waamini kama wajenzi wa amani na umuhimu wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu kwa makini kilio cha amani duniani na kwamba, vijana wanapaswa kushirikishwa katika ujenzi wa amani duniani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa sasa dunia imegeuka kuwa kama tambara bovu kutokana na madhara ya vita yanayoendelea kujionesha sehemu mbali mbali za dunia, kumbe, mikutano kama hii inatoa changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujikita katika kutafuta na kudumisha amani duniani bila kuchoka. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambako mipasuko na migawanyiko inaonekana wazi kabisa, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga madaraja ya amani, ili kukuza na kudumisha umoja; kuganga na kuponya madonda ya kihistoria, ili kukoleza amani na utulivu duniani.

Biashara haramu ya silaha, vita na vitendo vya kigaidi ni kati ya mambo yanayoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu duniani, lakini waathirika wakubwa ni maskini na wanyonge ndani ya jamii. Kumbe, waamini wa dini mbali mbali wanaowajibu wa kujikita katika mchakato wa kutafauta na kudumisha amani duniani, kwani huu ni wajibu msingi wa dini zote duniani. Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuungana nao kwa ajili ya kuombea amani duniani, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa udugu na maelewano hasa katika maeneo ambamo mtutu wa bunduki bado unarindima! Waamini wanaweza kuwa ni wajenzi wa amani na kwamba, ni wajibu wa viongozi kuwa ni madaraja ya ujenzi wa amani duniani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha amani kutoka sehemu mbali mbali za dunia, matumaini ya vijana wa kizazi kipya badala ya kugubikwa na uchoyo pamoja na ubinafsi.

Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha vijana wa kizazi kipya katika shule ya amani, ili waweze kuwa ni wajenzi na walezi wa amani duniani. Hii ndiyo changamoto pevu inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, ili kuwajengea vijana mazingira bora zaidi ya maisha; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima yao, changamoto ya kujenga na kudumisha mshikamano kati ya vizazi, ili kuweza kutembea na kusikilizana.

Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika mambo yanayowaunganisha watu kuliko kuendekeza yale yanayowagawa na kuwasambaratisha. Vijana wawe ni wajenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu badala ya kujenga kuta za utengano. Vijana waelimishwe kuthamini Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; wajenge na kudumisha urafiki ili kuwawezesha vijana kudumisha amani inayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao. Kwa msaada na neema ya Mungu, inawezekana kabisa kujenga amani duniani.

Papa: Madaraja ya amani
15 October 2018, 08:19