Cerca

Vatican News
Kanisa linafanya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki 1978 Kanisa linafanya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki 1978. 

Mtakatifu Yohane Paulo II ameacha ushuhuda wa kudumu katika maisha na utume wa Kanisa!

Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia barua Askofu Marco Brunetti wa Jimbo Katoliki Alba, Italia, ili kumpongeza kwa kuandaa Kongamano la shughuli za kichungaji na kitamaduni, kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya: maisha na mafundisho ya Mtakatifu Yohane Paulo II, hapo tarehe 13 Oktoba 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Ilikuwa ni tarehe 16 Oktoba 1978, Mtakatifu Yohane Paulo II alipochaguliwa kuliongoza Kanisa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Imegota miaka arobaini, tangu siku ile Mwenyezi Mungu alipowashangaza waja wake baada ya kifo cha Mtakatifu Paulo VI na Yohane Paulo wa kwanza. Waandishi wa habari wakautangaza mwaka huo kuwa ni mwaka wa Mapapa watatu ndani ya Kanisa. Kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochaguliwa kuliongoza Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia barua Askofu Marco Brunetti wa Jimbo Katoliki Alba, Italia, ili kumpongeza kwa kuandaa Kongamano la shughuli za kichungaji na kitamaduni, kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya: maisha na mafundisho ya Mtakatifu Yohane Paulo II, hapo tarehe 13 Oktoba 2018.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, washiriki wa kongamano hili watakuwa wamefaidika sana kwani Mtakatifu Yohane Paulo II ameacha kumbu kumbu ya kudumu katika akili na nyoyo za watu na kwamba, haitakuwa rahisi sana kuweza kufutika. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga karama na maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, sanjari na kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kukuza ari na mwamko na huduma za kimisionari.

Kongamano hili, imekuwa ni fursa ya kugundua tena ushuhuda wa uaminifu kwa Mungu na upendo kwa jirani; changamoto na mwaliko uliotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake. Anawataka vijana kumfungulia Kristo malango ya maisha yao; daima wakijitahidi kuwa ni mashuhuda, vyombo na wajenzi wa amani, udugu na mshikamano. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia washiriki wote baraka zake za kitume. Kati ya wawezeshaji wakuu kwenye kongamano hili ni pamoja na Padre Federico Lombard, SJ, aliyezungumzia kuhusu uwezo mkubwa wa Mtakatifu Yohane Paulo II katika tasnia ya mawasiliano ya jamii.

Wawezeshaji wengine, wamegusia hija za kichungaji zilizofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji na ushuhuda wa kimisionari; mchango wa Papa Yohane Paulo II katika kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wanawake ndani na nje ya Kanisa; majadiliano kati ya Mtakatifu Yohane Paulo II na vijana wa kizazi kipya, waliompenda upeo, ushuhuda unaojionesha hadi wakati huu kutokana na maadhimisho ya Siku za vijana kitaifa na kimataifa. Washiriki wa kongamano wameonja: historia, maisha, utume na changamoto alizokabiliana nazo Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Yohane Paulo II
16 October 2018, 15:27