Tafuta

Vatican News
Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana 2018: matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya! Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana 2018: matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya!  (Vatican Media )

Sinodi ya Vijana: Matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya!

Vijana washirikishwe katika mchakato wa kujadili, kuamua na kutekeleza mambo msingi katika maisha yao; wajengewe uwezo wa uongozi, ili kuchangia: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Wapewe malezi ya kutosha, ili waweze kuchangia karama, vipaji na taaluma yao. Vijana wanataka kuwa kweli ni wamisionari wenye furaha na wainjilishaji wakuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Wajumbe wa vijana waliokuwa wanashiriki katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba 2018 wametoa “Hati ya Utangulizi wa Sinodi” itakayowasilishwa kwa Mababa wa Sinodi kama sehemu ya “Hati ya Kutendea Kazi”. Sehemu ya pili inagusia: Imani na miito; mang’amuzi pamoja na kuwasindikiza. Hapa vijana wanaangalia uhusiano wao na Kristo Yesu; Imani na Kanisa; Maana ya wito katika maisha; Mang’amuzi ya miito; Vijana na dhamana ya kuwasindikiza.

 

SEHEMU YA TATU: Shughuli za elimu na mikakati ya ya Kanisa katika shughuli za kichungaji. Mfumo wa Kanisa: Vijana wanataka kuona Kanisa linalojengwa na Jumuiya ya waamini wanaojikita katika ukweli na uwazi; wakarimu, waaminifu, mashuhuda hai wa imani, watu wanaoweza kukuza na kudumisha mawasiliano na mafungamano ya kijamii, watu wenye furaha na wanaoweza kufikiwa kwa urahisi. Pale Kanisa linapoogelea kwenye mapungufu ya kibinadamu, liwe na ujasiri wa kukiri na kuomba msamaha hasa kutokana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia, uchu wa mali na madaraka; ili kuimarisha utambulisho wake pamoja na kuwajengea vijana imani, kwani vijana wengi kwa sasa hawapendi kuona utawala wa mabavu.

Kanisa liwe ni shuhuda wa ukweli na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kanisa liendelee kuwekeza katika vyombo vya mawasiliano ya jamii, lifafanue kwa kina na mapana usawa wa kijinsia unaotaka kufuta tofauti msingi kati ya mwanaume na mwanamke kadiri ya mpango wa Mungu. Kanisa liwe ni kioo angavu cha majadiliano kati ya Kanisa na Sayansi; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha utunzaji bora wa mazingira. Vijana wanataka kuona Kanisa linalosimikwa katika misingi ya umoja, upendo na mshikamano; kwa kuendelea kuwa ni sauti ya wanyonge na maskini; watu wanaodhulumiwa na kunyanyaswa katika maisha, Kanisa linalojikita katika mahusiano na watu!

Vijana kama wadau wakuu: Vijana wanapaswa kushirikishwa katika mchakato wa kujadili, kuamua na kutekeleza mambo msingi katika maisha yao, kwa kuwajengea uwezo wa uongozi, ili kuchangia: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika ngazi mbali mbali. Wapewe malezi ya kutosha, ili hatimaye, kwa njia ya mifano bora ya maisha, waweze kuchangia karama, vipaji na taaluma yao kwa ajili ya ustawi wa wengi. Vijana wanataka kuwa kweli ni wamisionari wenye furaha wanaotaka kushiriki katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa kwa ari na moyo mkuu; kwa kushirikiana na wazee katika maisha na utume wa Kanisa.

Vijana wanataka kushiriki katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, lakini wanapaswa kuwezeshwa kielimu na kiuchumi. Kanisa lithubutu kuwatafuta na kuwafuata vijana kwenye mitandao ya kijamii, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya kijamii na kiutu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Sera na mikakati mbali mbali inayopaswa kuendelezwa ili kuwawezesha vijana kujenga uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu. Kwanza kabisa watambue umuhimu wa Sakramenti za Kanisa, maisha ya sala, ushiriki mkamilifu wa liturujia na kwamba, wanapaswa kuwa ni mashuhuda na walinzi wa imani katika ulimwengu mamboleo. Vijana waandaliwe vyema kushiriki katika Sakramenti za Kanisa, hususan: Sakramenti ya Ndoa kwa kutambua maana, umuhimu, changamoto, uzuri na utakatifu wake. Sakramenti ya Upatanisho, iwaonjeshe vijana huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni muda muafaka wa Kanisa kutembea na vijana katika maisha na wito wao; utume kwa vijana unapaswa kuendelezwa pamoja na kuimarisha vyama vya utume kwa vijana katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Matukio mbali mbali yawasaidie vijana kukuza imani, matumaini, mapendo na mshikamano wao wa kidugu. Mwelekeo wa maisha na utume wa Kanisa katika masuala ya kijamii na maisha ya kiroho, yawasaidie mchakato wa uinjilishaji miongoni mwa vijana dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kushikamana dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na uhamiaji wa shuruti!

Nyenzo za kutumia: Vijana wanalishauri Kanisa kutumia lugha rahisi iliyoeleweka kwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kukuza ari na hamu ya kusikiliza Injili, katika ukimya na tafakari ya kina pamoja na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Vijana wanalitaka Kanisa kutumia njia za mawasiliano ya kisasa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji, majadiliano ya kidini na kiekumene. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika matumizi ya njia za mawasiliano ya kijamii. Maadhimisho ya matukio mbali mbali ya Kanisa ni muda muafaka wa kujenga utamaduni wa Kanisa kukutana na waamini wa dini mbali mbali duniani. Sanaa na uzuri vitumike katika mchakato wa uinjilishaji kwani mara nyingi vijana wanavutwa sana na muziki, sanaa, kipaji cha ubunifu na mwelekeo mpya.

Vijana wanalitaka Kanisa kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Tafakari ya Neno la Mungu, Taamuli kama njia muhimu sana za kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha yao! Vijana wanahimiza ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo kama njia muafaka ya uinjilishaji mpya. Mashuhuda na wafia dini huko Mashariki ya Kati wanawagusa vijana wengi na kwamba, maisha ya watakatifu ni kielelezo cha utimilifu wa maisha! Dhana ya Sinodi ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa unaowawezesha vijana kukua na kukomaa katika imani na kwamba, huu ni utamaduni unaopaswa kuvaliwa njuga na Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, wazee wana ndoto lakini vijana wana maono!

Kwa muhtasari haya ndiyo yaliyojiri katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, yaliyofanyika mjini Vatican kuanzia tareh 19 hadi tarehe 25 Machi 2018 kama sehemu ya mchakato wa Mama Kanisa kujenga utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza vijana kwa makini!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

15 August 2018, 08:10