Tafuta

Vatican News
Tetemako la ardhi nchini Indonesia limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Tetemako la ardhi nchini Indonesia limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.  (ANSA)

Papa Francisko asikitishwa na maafa yaliyotokea nchini Indonesia

Tetemeko la ardhi nchini Indonesia limesababisha zaidi ya watu 98 kufariki dunia, watu 236 kujeruhiwa vibaya na watu wengine 20, 000 hawajulikani mahali walipo na kwamba nyumba zaidi ya 13, 000 zimeharibika sana na kwamba, kuna maeneo ambayo yamefunikwa kwa vifusi vya maporomoko ya udongo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana taarifa ya maafa yaliyotokea Jumapili, tarehe 5Agosti 2018 huko nchini Indonesia na kusababisha watu zaidi ya 98 kufariki dunia, watu 236 kujeruhiwa vibaya na  watu wengine 20, 000 hawajulikani mahali walipo na kwamba nyumba zaidi ya 13, 000 zimeharibika sana. Miundombinu ya barabara na majengo ya huduma imeharibiwa sana na kwamba, kuna maeneo ambayo yamefunikwa kwa vifusi vya maporomoko ya udongo. Zaidi ya watu 2, 000 wamehamishiwa maeneo salama kwa hofu ya kutokea kwa Tsunamini, kama ile iliyojitokeza kunako mwaka 2004 na kusababisha watu 226, 000 kutoka katika nchi 13 duniani na zaidi ya wananchi 120, 000 kutoka Indonesia walifariki dunia.

Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwenda kwa viongozi mahalia wa Kanisa na serikali anasema, anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa wote walioguswa na kutikishwa na maafa haya. Anawaombea marehemu waweze kupata pumziko la amani mbinguni na majeruhi wajaliwe faraja na hatimaye, waweze kupona haraka ili kuendelea na shughuli zao. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa matetemeko mawili huko nchini Indonesia. Mwishoni ametoa baraka zake za kitume kwa familia ya Mungu nchini Indonesia.

Taarifa kutoka Indonesia zinabainisha kwamba, mji wa Lombok na Bali imeathirika vibaya na kwamba, Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia juhudi za kuokoa maisha ya watu. Kwa sasa Indonesia inahitaji msaada wa kimataifa ili kukabiliana na maafa haya makubwa kwa wananchi wake. Ubalozi wa Indonesia mjini Vatican umemshukuru Baba Mtakatifu kwa ujumbe na mshikamano wake wa dhati na wananchi wa Indonesia ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu sana.

Rais Joko Widodo wa Indonesia amewataka viongozi wa Serikali kuhakikisha kwamba, wanatoa msaada unaohitajika kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi. Kwa sasa watu wanahitaji mahali pa kujihifadhi, chakula, dawa na vyombo vya mawasiliano kwani njia nyingi za mawasiliano zimeharibiwa vibaya sana. Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki nchini Indonesia, Karina yaani, Caritas Indonesia, inaendelea kutoa msaada wa dharura kwa waathirika.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

07 August 2018, 14:07