Tafuta

Papa Francisko alipokutana kwa faragha na Maaskofu Katoliki wa Chile kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Papa Francisko alipokutana kwa faragha na Maaskofu Katoliki wa Chile kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia. 

Papa Francisko apongeza juhudi za Maaskofu Chile!

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na sera, mikakati na maamuzi yaliyochukuliwa na Maaskofu Katoliki wa Chile, ameamua kwa mkono wake mwenyewe kuwaandikia Maaskofu ili kuwapongeza na kuwatia shime katika mchakato huu wa toba na wongofu wa ndani unaopania kupyaisha maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo imelitikisa sana Kanisa nchini Chile, kiasi kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki nchini humo baada ya kukutana kwa faragha na Baba Mtakatifu Francisko na baadaye katika mkutano wake maalum, limeamua kuanza mchakato wa toba na wongofu wa ndani unaolenga kupyaisha maisha na utume wa Kanisa, dhamana inayowashirikisha watu wote wa Mungu nchini humo! Maaskofu 32 wa Chile wanaomba msamaha kwa kutotimiza vyema wajibu na dhamana yao kwa wakati muafaka! Maaskofu wote kwa pamoja wanakiri dhambi!

Maaskofu wanawataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, kwa njia ya matendo yenye mvuto na mashiko, daima wakijikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya: ukweli, haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mtikisiko huu wa kimaadili na kiimani, umekuwa ni fursa kwa familia ya Mungu nchini Chile, kujiangalia upya, tayari kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji utakaojenga na kudumisha utamaduni wa nidhamu ili hatimaye, kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia kutoka katika undani wake!

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na sera, mikakati na maamuzi yaliyochukuliwa na Maaskofu Katoliki wa Chile, ameamua kwa mkono wake mwenyewe kuwaandikia Maaskofu ili kuwapongeza na kuwatia shime katika mchakato huu wa toba na wongofu wa ndani sanjari na kushirikiana na waendesha mashtaka wa Serikali dhidi ya wakleri waliojihusisha na vitendo vya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wa dogo.

Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kutambua na kukiri makosa ya kutotimiza wajibu wa kuwasilikiza waathirika na kuwachukulia hatua za kinidhamu watuhimiwa, ili kupambana na hali hiyo, mapema kabisa. Maaskofu wamejizatiti kabisa katika tafakari, mang’amuzi na hatimaye, kutoa maamuzi magumu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Chile! Hatua hii itakuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa.

Kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake, ameendelea kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wahusika, pamoja na kukutana na kuzungumza na waathirika wa nyanyaso hizi. Mama Kanisa katika kuendeleza Utume wake wa kutaka kudhibiti uhalifu unaoweza kutendwa na waamini: lengo likiwa ni kumrekebisha mhalifu; kutenda haki kwa waliokosewa; na kuondoa kashfa (Rej. CIC, c. 1341). Kati ya makosa ya uhalifu, yapo yale ambayo yanatambuliwa kuwa ni makosa makubwa ya uhalifu, Delicta graviora, na yametengwa ili kushughulikiwa, sio tena na Askofu Jimbo wala Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume, bali na Mahakama maalumu ya Baba Mtakatifu.  

Mahakama hiyo ni Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Makosa husika yanayoshughulikiwa na Mahakama hiyo ni makosa dhidi ya Sakramenti ya Kitubio, dhidi ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na dhidi ya Amri ya sita ya Mungu. Kuhusu Sakramenti ya Kitubio, makosa ambayo mchakato wake umetengwa ili kushughulikiwa na Kiti Takatifu, yaani Mahakama ya Baba Mtakatifu ni: makosa ya Padri kuvunja siri ya kitubio, kumtongoza kimapenzi kwa maneno au ishara mwamini anayekuwa katika kitubio, au kutumia kwa namna yeyote maongezi ya kwenye kitubio kwa kumuumiza aliyetubu kwake.

Kanisa nchini Chile katika kipindi hiki cha toba na wongofu wa ndani, linataka kujikita katika mchakato wa kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika maisha na utume wa Kanisa. Ili kufikia azma hii, kuna haja kwa familia ya Mungu nchini Chile kurejea tena katika chemchemi ya Uso wa huruma ya Mungu, Kristo Yesu, ili awapatie neema ya kufanya toba ya kweli ili hatimaye, Kanisa nchini Chile liwe ni Jumuiya ya watu waliokombolewa na kutakaswa kwa huruma na upendo wa Mungu. Huruma na msamaha wa Mungu ushuhudiwe kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa linataka kumwlisha ukweli na huruma ya Mungu katika utume wake na kwa matarajio kwamba, matukio kama haya hayatajirudia tena nchini humo.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

09 August 2018, 15:59