Tafuta

Papa Francisko wakati wa katekesi tarehe 1 Agosti 2018 Papa Francisko wakati wa katekesi tarehe 1 Agosti 2018 

Papa Francisko: Likizo ni wakati wa kujipumzisha na kupyaisha maisha ya kiroho!

Likizo ni muda muafaka wa kuimarisha mafungamano ya kiroho na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na tafakari kuhusu uzuri wa kazi ya uumbaji inayoonesha na kushuhudia wema na ukarimu wa Mungu kwa binadamu. Baba Mtakatifu anapenda kusisitizia kwamba, likizo, kiwe ni kipindi cha amani, furaha, sala na maisha ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa Katekesi yake kuhusu Amri za Mungu, Jumatano tarehe 1 Agosti 2018 amewataka waamini kujenga na kudumisha moyo wa kujisadaka katika huduma makini kwa Mungu na jirani kama njia ya kupanua upendo na kurutubisha karama zao. Anawataka waamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, kama alivyofanya Bikira Maria. Kwa wananchi wengi wa Ulaya na Marekani, mwezi Agosti ni kipindi cha likizo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni muda muafaka kwa watu kujichotea nguvu ya kimwili, kiakili na kiroho.

Likizo ni muda muafaka wa kuimarisha mafungamano ya kiroho na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na tafakari kuhusu uzuri wa kazi ya uumbaji inayoonesha na kushuhudia wema na ukarimu wa Mungu kwa binadamu. Baba Mtakatifu anapenda kusisitizia kwamba, likizo, kiwe ni kipindi cha amani, furaha, sala na maisha ya kiroho. Tarehe Mosi, Agosti, 2018, Kanisa limefanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Alfonsi Maria Liguori, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, ni mtakatifu msimamizi wa wanataalimungu maadili na waungamishaji. Huyu ni kati ya watakatifu waliojitwalia umaarufu kunako karne ya kumi na nane, kutokana na mtindo wake wa maisha, uliokuwa na mvuto pamoja na mguso kwa watu aliokutana nao; makini kwa mafundisho kuhusu Sakramenti ya Upatanisho.

Mtakatifu Alfonsi alikuwa anawahimiza Mapadre kuhakikisha kwamba, waamini wanapata Sakramenti hii, ili waonje upendo, furaha na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambaye daima yuko tayari kumpokea mwamini anayetubu na kuongoka. Ana mchango mkubwa pia kuhusu maisha ya sala za Kikristo.  Mtakatifu Alfonsi alikuwa anasema kwamba, sala ni njia muhimu ya kuwa na uhakika wa kupata wokovu na hii ndiyo maana ya sala. Ikumbukwe kwamba, lengo la Sala ni kumfikia Mwenyezi Mungu, kwani mwanadamu ameumbwa kwa upendo wa Mungu ili aweze kumkirimia utimilifu wa zawadi ya maisha, kwani kutokana na dhambi, mwanadamu amejikuta akiwa mbali na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Anayesali anaokolewa na asiyesali anapata hukumu ya milelle. Ni vigumu mtu kuokoka bila kusali, lakini inawezekana kabisa kwa kusali mtu akaweza kuokoka, kwani neema ya sala amekirimiwa kila mwamini.

Kila fursa katika maisha ya mwamini inaweza kutumiwa kama njia ya sala, hususan nyakati za shida na karaha. Ni mwaliko wa kuendelea kumwamini Mungu kwani Yeye daima yuko tayari kumsaidia mwanadamu katika mahangaiko yake. Waamini wasiogope kumkimbilia Mungu wakati wa shida na mahangaiko yao ya ndani. Jambo la msingi ni kuomba afya njema ya roho na mwili inayotolewa na Yesu Kristo mwenyewe. Mwamini anapenda kuonja uwepo wa Yesu unaookoa na kumkirimia mwanadamu uwezo wa kuwa kweli ni mwanadamu na mwenye furaha.

Kwa njia ya sala waamini wanaweza kupokea neema za Mungu na kupata mwanga unaomwezesha mtu kupambanua mema na mabaya, kwa kuimarisha dhamiri nyofu, kwa kufurahia jambo jema liliotambuliwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mwanadamu kila siku anazungukwa na vishawishi, kumbe hawezi kukosa kusali ili apate neema ya kupambana na hatimaye, kuishinda vishawishi na dhambi. Waamini wanahitaji neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili kufanyika azma hii, kwa kutambua udhaifu wa maisha ya kibinadamu, mwaliko wa kuomba pia fadhila ya unyenyekevu na kutegemea huruma ya Mungu. Mwanadamu ni maskini kwa sababu Mungu ni mwingi wa utajiri.

Kwa njia ya sala, mwamini anaweza kumwomba Mwenyezi Mungu nguvu anayohitaji kutenda mema, kwani Bwana hawezi kumnyima mtu anayemwendea kwa unyenyekevu na moyo mkuu. Mtakatifu Alfonsi Maria wa Liguori anafundisha kwamba, uhusiano wa dhati na Mwenyezi Mungu ni muhimu sana katika maisha na unafumbatwa katika njia ya Sala binafsi na ushiriki wa Sakramenti za Kanisa; ni fursa makini zinazoweza kuongeza uwepo wa Mungu katika maisha ya mwamini, anayemwongoza mapito yake, anayapatia mwanga pamoja na kuwakarimia usalama na amani ya ndani, hata wakati wa mateso.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

01 August 2018, 16:35