Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anakazia umuhimu wa: kusindikiza, kung'amua na kushirikisha familia katika maisha na utume wa Kanisa. Papa Francisko anakazia umuhimu wa: kusindikiza, kung'amua na kushirikisha familia katika maisha na utume wa Kanisa. 

Papa Francisko: Zingatieni: Kuwasindikiza, kung'amua na kushirikisha wana ndoa!

Baba Mtakatifu Francisko katika sura ya nane anakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Kuwasindikiza, kung’amua na kushirikisha familia dhaifu! Anapenda kujikita katika mambo makuu mawili: kwanza kabisa ni juu ya Mafundisho tanzu ya Sakramenti ya Ndoa na Nidhamu ya Sakramenti ya Ndoa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Furaha ya Upendo ndani ya familia “Amoris laetitia” “AL” ni Wosia wa Kitume uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu Injili ya familia na kuchapishwa rasmi tarehe 19 Machi 2016, Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu mume wake Bikira Maria, sanjari na kumbu kumbu ya miaka mitatu tangu Baba Mtakatifu Francisko alipoanza utume wake rasmi kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wosia huu wa kitume ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia zilizoadhimishwa kunako mwaka 2014 na mwaka 2015.

Baba Mtakatifu Francisko katika sura ya nane anakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Kuwasindikiza, kung’amua na kushirikisha familia dhaifu! Anapenda kujikita katika mambo makuu mawili: kwanza kabisa ni juu ya Mafundisho tanzu ya Sakramenti ya Ndoa na Nidhamu ya Sakramenti ya Ndoa. Ikumbukwe kwamba, Sakramenti ya Ndoa ni kielelezo cha umoja na upendo wa Kristo kwa Kanisa lake, mwaliko wa kuwapokea, kuwasaidia na kuwasindikiza waamini wanaokabiliwa na matatizo na changamoto katika maisha ya ndoa na familia. Hapa kazi ya Kanisa inafananishwa na hospitali iliyoko kwenye uwanja wa vita.

Viongozi wa Kanisa waendelee kukazia mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa; wawe na mang’amuzi ya kichungaji kwa kesi maalum, ili kuamriwa kadiri ya tamaduni na mazingira ya watu husika. Lengo ni kufikia utimilifu wa maisha ya ndoa na familia mintarafu mwanga wa Injili! Njia ya Kanisa ni ile ambayo imeoneshwa kwa njia ya huruma, kwa kuwashirikisha waamini wote katika maisha na utume wa Kanisa bila ubaguzi wala kuwatenga. Hapa jambo la msingi ni kuwa na maamuzi makini kwa mtu mmoja mmoja na katika shughuli za kichungaji kwa ujumla wake!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hakuna sheria au kanuni maalum inayotarajiwa kutolewa na Mababa wa Sinodi wala katika Wosia huu wa kitume kama sheria ya Kanisa inayoweza kutumika kwa watu wote. Waamini waliotengana wanapaswa kuchunguza dhamiri zao, ili kudumisha imani na matumaini yao kwa huruma ya Mungu. Mapadre kwenye kiti cha huruma ya Mungu wawasaidie waamini kuunda dhamiri nyofu, jambo linalohitaji unyenyekevu, usiri na upendo kwa Kristo, Kanisa na Sheria zake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kumekuwepo na giza nene la kufahamu sheria za Kanisa hali ambayo kimsingi inagumisha maamuzi: nyanyaso, hofu, ukosefu wa ukomavu katika upendo.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti inayopania kuwaimarisha wanyonge na wala si nishani kwa waamini wema na watakatifu! Baba Mtakatifu anawahimiza viongozi wa Kanisa kujikita katika sheria ya upendo na kukazia mafundisho yake sanjari na kuwa na sera na mikakati makini ya kuimarisha ndoa ili kuepuka mipasuko isiyokuwa na tija. Hakuna sababu ya kuhukumu, kushutumu wala kumtenga mtu, bali wote wanahamasishwa kuishi katika huruma ya Mungu inayomwambata kila mtu, bila kubeza Injili. Mikakati ya shughuli za kichungaji iwe na upendo wenye huruma, tayari kusaidia, kuelewa, kusamehe, kusindikiza, kuamini na kujumuishwa. Waamini wanaoishi katika mazingira tete wawe na ujasiri wa kuwaendea Mapadre au waamini walei ili hatimaye, waweze kupata mwanga utakaowasaidia kuelewa hali ya maisha yao. Mapadre wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini, upendo na utulivu, ili kuwasaidia kugundua nafasi yao katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, elimu na malezi kwa watoto ni wajibu msingi kwa wazazi, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa hekima, busara na uhuru. Wazazi na walezi wawe na dhamiri nyofu na haki ya kuchagua aina ya elimu kwa watoto wao, ili waweze kufanya maamuzi makini wakati wanapokabiliwa na hali tete; wawasaidie kuwa na dira na mwelekeo chanya wa maisha. Malezi yawasaidie watoto kuwajibika katika kufanya maamuzi yao.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

10 August 2018, 16:17