Tafuta

Vatican News
Papa Francisko akiwa Sarayevo, Juni 2015 Papa Francisko akiwa Sarayevo, Juni 2015 

Papa Francisko: Jengeni mtandao wa wanataalimungu maadili

Sarayevo anasema Baba Mtakatifu ni mji ambao ni kama daraja linalojaribu kuwaunganisha watu, waliotawanyika na kusambaratika kama umande wa asubuhi, ili kuganga na kuponya kinzani na mipasuko ya kijamii, tayari kuanza mchakato wa kuwakusanya na kuwakutanisha watu kutoka katika tamaduni, dini, matabaka na mitazamo mbali mbali ya kisiasa na kiitikadi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kutokana na kuyumba pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema, huu ni muda muafaka wa kujenga madaraja mintarafu maadili ya Kanisa Katoliki katika ulimwengu mamboleo. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa Kongamano la III la Kimataifa kuhusu taalimungu maadili katika Kanisa, lililofunguliwa hapo tarehe 26 na kuhitimishwa rasmi 27 Julai 2018 huko mjini Sarayevo. Huu ni mji anasema Baba Mtakatifu, wenye kielelezo cha pekee katika safari ya amani na upatanisho, baada ya maafa makubwa yaliyosababishwa na vita kutokana na misigano mbali mbali katika eneo hili.

Sarayevo anasema Baba Mtakatifu ni mji ambao ni kama daraja linalojaribu kuwaunganisha watu, waliotawanyika na kusambaratika kama umande wa asubuhi, ili kuganga na kuponya kinzani na mipasuko ya kijamii, tayari kuanza mchakato wa kuwakusanya na kuwakutanisha watu kutoka katika tamaduni, dini, matabaka na mitazamo mbali mbali ya kisiasa na kiitikadi. Tema iliyochaguliwa ni muhimu sana kwa wakati huu ambapo kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu, kumekuwepo na tabia ya kutaka kujenga kuta zinazowatenganisha watu na hivyo kusababisha: dhuluma na nyanyaso na mahangaiko kwa watu wasiokuwa na hatia. Kwa kuzingatia hekima na busara, familia ya Mungu inapaswa kuanza kujielekeza katika kupambana na kuta za utengano, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu, haki na amani.

Mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika ulimwengu mamboleo ni kujizatiti katika kukabiliana na changamoto ya ekolojia, ambayo madhara yake ni makubwa sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Changamoto hii kama ilivyodadavuliwa kwa kina na mapana katika “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote inapaswa kuzingatia kanuni maadili inayofumbatwa katika maadili jamii; mambo msingi yanayohitaji toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kukabiliana na changamoto la wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani.

Haya ni mambo msingi yanayopaswa kupembuliwa kwa kina na mapana hata kabla ya kuanza kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji. Baba Mtakatifu katika mazingira kama haya, anasema, kuna haja ya kuwa na watu pamoja na viongozi waliojipyaisha, ili kuchuchumilia utekelezaji wa kanuni hizi katika uhalisia wa maisha ya watu, daima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza!

Taalimungu maadili inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na changamoto za kiekolojia, kwa kujenga mshikamano wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kupembua, kupanga na hatimaye, kuibua mbinu mkakati muafaka kwa changamoto hizi. Kwa njia hii, jamii inaweza kupata rasilimali watu na vitu ili kupata majibu muafaka yatakayo saidia kutatua matatizo yanayomkumba mwanadamu kwa mwanga wa huruma ya Mungu. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwanza kwa wanataalimungu waliokuwasanyika mjini Sarayevo, kujenga daraja kati yao, ili kuweza kushirikisha mbinu za kuweza kufikia malengo haya pamoja na kukaribiana ili maamuzi yao yaweze kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, msingi wa mageuzi katika vyuo vikuu na taasisi za elimu Katoliki  umebainishwa vyema katika “Katiba ya Kitume Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” kwa kujikita zaidi katika majadiliano mapana zaidi katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu; kwa kuendeleza mwingiliano kati ya vitivo hali inayopaswa pia kujitokeza katika taalimungu maadili. Kuna haja ya kujenga mtandao kati ya taasisi na vyuo vikuu sehemu mbali mbali za dunia ili kujenga na kuendeleza masomo ya kikanisa.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawaalika  na kuwatia shime wanataalimungu maadili kujikita katika mchakato wa ujenzi wa majadiliano ili kuanzisha mtandao huu, ili kupembua kwa kina na mapana mambo msingi, matatizo changamani yanayomkumba mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, daima wakiendelea kuwa waaminifu kwa Maandiko Matakatifu, yanayofafanua historia ya binadamu na mchakato wa mshikamano na walimwengu, ili kuonesha dira na mwongozo wa kufuata; kwa kusindikiza, kuganga na kuponya majeraha pamoja kuwaenzi wadhaifu bila kutoa hukumu!

Mababa Mtakatifu anawashukuru wana taalimungu maadili walioko kwenye mtandao huu unaojulikana kama “Catholic theological ethics in the Word Church”. Mtandao huu umewahi kufanya makongamano huko Padua kunako mwaka 2006 na Trento 2010 yote yakiwa nchini Italia. Kumekuwepo pia na makongamano ya kikanda sehemu mbali mbali za dunia, yaliyowezesha hata kutoa machapisho ya makongamano haya, mafundisho na hivyo kusaidia kwa kiasi kikubwa wajumbe kushirikiana uwezo na mang’amuzi yao, mambo wanayopaswa pia kulishirikisha Kanisa zima. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia heri na baraka viongozi waliomaliza muda wao na wale watakao chaguliwa kuendeleza gurudumu hili!

Papa: Sarayevo

 

27 July 2018, 16:47