Tafuta

Vatican News
2018.07.12 Funerali Card. Tauran 2018.07.12 Funerali Card. Tauran   (� Vatican Media)

Kardinali Jean Louis Tauran alikuwa ni chombo cha majadiliano!

Kardinali Jean Louis Tauran katika maisha yake kama Padre, Askofu na Kardinali alijitosa bila ya kujibakiza katika huduma kwa Kristo na Kanisa lake, akajisadaka katika mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Apumzike kwa amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 12 Julai 2018, ameongoza Ibada ya mazishi ya Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, aliyefariki dunia hapo tarehe 5 Julai 2018 akiwa nchini Marekani kwa matibabu zaidi. Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka, kumwombea na kumsindikiza Kardinali Tauran katika usingizi wa amani kwa kumweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake.

Kardinali Sodano katika mahubiri yake anasema, licha ya salam za rambi rambi zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, lakini hata yeye  binafsi, anakumbuka kwa namna ya pekee sana Marehemu Kardinali Tauran kutokana na juhudi, bidii, weledi, ari na moyo wake wa utume, uliomwezesha kulihudumia Kanisa kwa ari, moyo mkuu na bidii, licha ya uzito wa ugonjwa uliokuwa unamsumbua! Anasema, Liturujia ya Neno la Mungu ni mwaliko kwa waamini kuwa na imani na matumaini kwa wale wote wanaofariki dunia wakiwa mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Katika kilio na maombolezo yao, kwa hakika Bwana atawasikiliza na kuwajibu.

Kumbe, hakuna sababu kwa waamini kukata wala kujikatia tamaa wanapokumbana na mateso, mahangaiko na Misalaba katika maisha! Hata kama mwili wao wa nje ukiharibika, lakini, daima mwili wao wa ndani, utaweza kutukuzwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Heri za Mlimani ni muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Kristo Yesu na katika tukio hili la kuomboleza kifo cha Kardinali Tauran, bado wamekumbushwa kwa namna ya pekee kwa kumwangalia kama nyota angavu. Badala ya kilio na maombolezo, Kanisa linamkumbuka na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Kardinali Jean Louis Tauran.

Kwa miaka mingi anasema Kardinali Sodano amejisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kumbu kumbu ambayo haitakuwa rahisi sana kuweza kufutika akilini na moyoni mwake. Alikuwa ni Padre, Askofu na Kardinali aliyejitosa kimasomaso kwa ajili ya huduma makini na endelevu kwa Vatican na Kanisa katika ujumla wake. Ni kiongozi aliyejitahidi kumwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa hususan katika mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani.

Marehemu Kardinali Tauran alijikita zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kwa kukazia heshima, staha na uelewano, huku kila mmoja akitambua tofauti msingi na kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaitwa kutenda kazi pamoja ili kuujenga ulimwengu katika amani ya kweli!

Kardinali Tauran alianza utume wake katika diplomasia ya Kanisa, akakabidhiwa nyadhifa mbali mbali kati yake ni ule wadhifa wa kuwa Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Akateuliwa na Papa Mstaafu Benedikto XVI kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini. Hapa akaonesha umahiri wake kwa kuwa ni mshauri aliyesikilizwa na wengi, akajenga imani na matumaini na waamini wa dini ya Kiislam katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini.

Kutokana na moyo wake wa sadaka, majitoleo na huduma kwa Kanisa anasema Baba Mtakatifu Francisko akamteua kuwa Camerlengo wa Kanisa Takatifu Katoliki. Ni kiongozi aliyekuwa na imani thabiti, akalihudumia Kanisa kwa juhudi, maarifa, bidii na weledi wa hali ya juu kabisa, hata dakika ya mwisho, licha ya ugonjwa wake uliokuwa unamsumbua kwa muda mrefu! Sasa vita imekwisha, imani ameilinda, Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kumpokea mtumishi wake katika amani na furaha ya milele.

Baba Mtakatifu anapenda kumkabidhi Marehemu Kardinali Tauran kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, kwa mtumishi wake, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kristo!Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa familia ya Kardinali Tauran, Baraza la Makardinali, ndugu, jamaa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema bila kuwasahau waamini wa Jimbo kuu la Bordeaux, nchini Ufaransa.

Historia yake kwa ufupi kabisa! Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini na Camerlengo wa Kanisa Katoliki, amefariki dunia, tarehe 5 Julai 2018, akiwa na umri wa miaka 75 huko Connecticut, nchini Marekani, ambako alikwenda kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa Parkinson. Itakumbukwa kwamba, tarehe 13 Marchi 2013 baada ya Makardinali kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro, akamtangaza hadharani Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Jean Louis Tauran alizaliwa kunako tarehe 5 Aprili 1943 huko Bordeaux, nchini Ufaransa.

Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 20 Septemba 1969. Tarehe 1 Machi 1975 akajiunda na Diplomasia ya Vatican na kushika nafasi mbali mbali katika masuala ya kidiplomasia.  Tarehe 6 Januari 1991 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu na Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Mwaka 2003 akateuliwa kuwa Mkutubi mkuu wa Maktaba ya Kanisa Katoliki. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali kunako mwaka 2003. Mwaka 2007 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Tarehe 20 Desemba 2014, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Camerlengo wa Kanisa Katoliki.

Kutokana na kifo cha Kardinali Jean Louis Tauran, Baraza la Makardinali kwa sasa linaundwa na Makardinali 225 kati yao wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa ucahguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni124 na wengine 101 hawana tena haki ya kupiga kura wala kuchaguliwa wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kifo Kardinali Tauran

 

12 July 2018, 15:21