Tafuta

Vatican News
BabaMtakatifu Francisko anasema Roho Mtakatifu analijenga na kulitegemeza Kanisa, lakini Shetani, Ibilisi anataka kuligawa na kuliharibu! BabaMtakatifu Francisko anasema Roho Mtakatifu analijenga na kulitegemeza Kanisa, lakini Shetani, Ibilisi anataka kuligawa na kuliharibu!  (ANSA)

Papa Francisko: Roho Mtakatifu Analijenga na Kulitegemeza Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko: Roho Mtakatifu huwapatanisha na kujenga umoja na Mwenyezi Mungu ili wazae matunda mengi. Kanisa limepelekwa kutangaza na kushuhudia; kutekeleza na kueneza ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kumbe, Roho Mtakatifu analijenga na kulitegemeza Kanisa. Lakini kwa upande mwingine, kuna Shetani, Ibilisi anayetaka kuligawa na kuliharibu Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, utume wa Kristo Yesu na wa Roho Mtakatifu unakamilika katika Kanisa, mwili wa Kristo na Hekalu la Roho Mtakatifu. Ni utume unaowahusisha waamini wote katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Roho Mtakatifu hutayarisha watu, akiwaendea kwa neema yake ili kuwapeleka kwa Kristo. Anamdhihirisha kwao Bwana Mfufuka, anawakumbusha neno lake, anafumbua akili zao kutambua kifo chake na ufufuko wake. Analifanya Fumbo la Kristo liweko kwao  na katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Roho Mtakatifu huwapatanisha na kujenga umoja na Mwenyezi Mungu ili wazae matunda mengi. Kanisa limepelekwa kutangaza na kushuhudia; kutekeleza na kueneza ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kumbe, Roho Mtakatifu analijenga na kulitegemeza Kanisa.

Lakini kwa upande mwingine, kuna Shetani, Ibilisi anayetaka kuligawa na kuliharibu Kanisa. Huyu ni Ibilisi, baba wa wivu anayetumia mali, fedha na malimwengu. Imani na matumaini ya Wakristo yamesimikwa kwa Kristo Yesu na kwa Roho Mtakatifu. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 9 Mei 2020 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Katika utangulizi wake, amemkumbuka Mtakatifu Luisa de Marillac muasisi wa Shirika la Masista wa Pendo la Huruma wa Mtakatifu Vincenti wa Paulo ambaye kimsingi, kumbu kumbu yake inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 15. Lakini kwa vile tarehe hii iliangukia katika Kipindi cha Kwaresima, kumbu kumbu hii ikasogezwa mbele. Watawa wanaohudumia Hosteli ya Mtakatifu Martha na Zahanati ya Mtakatifu Martha ni kutoka Shirika la Masista wa Pendo la Huruma wa Mtakatifu Vincenti wa Paulo lililoanzishwa na Mtakatifu Luisa de Marillac. Huu ni utume ambao wameutekeleza kwa takribani miaka 100 iliyopita. Baba Mtakatifu amewaombea heri na baraka katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa.

Liturujia ya Neno la Mungu, Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume Sura 13: 44-52 na sehemu ya Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane 14:7-14. Lakini kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amejikita zaidi katika Somo la kwanza linaloonesha jinsi ambavyo Paulo na Barnaba walivyowaendea wapagani baada ya Wayahudi kujaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakabisha na kutukana. Wakawafitinisha wanawake watauwa wenye vyeo na wakuu wa mji; wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao. Hii ndiyo kazi ya Shetani, Ibilisi anayetaka kuligawa na kuliharibu Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, haya ni mapambano endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Neno la Mungu linazidi kuenea sehemu mbali mbali za dunia, lakini pia hapakosi hata mara moja madhulumu dhidi ya Wakristo.

Hata hivyo, Kanisa litaendelea kusonga mbele kwa baraka na faraja zinazobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya dhuluma zinazofanywa na walimwengu. Baba Mtakatifu anakaza kusema katika maisha na utume wa Kanisa, daima kuna mapambo kati ya Roho Mtakatifu na Shetani, Ibilisi. Leo hii hata nguvu ya kiuchumi inaweza kuwa ni sababu ya wivu hii usiokuwa na mvuto wala mashiko. Nguzu za giza zinashinda na nguvu ya Mungu. Tangu siku ile ya kwanza ya juma, Pasaka ya Bwana, watu walipania kuhakikisha kwamba wanaunyamazisha ukweli kwa kutumia nguvu za kisiasa pamoja na fedha. Imani ya Wakristo anasema Baba Mtakatifu Francisko imesimikwa kwa Kristo Yesu na Roho Mtakatifu. Hapa si kwa ajili ya mtu kupata nguvu za kisiasa. Imani na Matumaini ya Wakristo yako mikononi mwa Yesu na Roho Mtakatifu. Nguvu hizi si kwa ajili ya malimwengu wala kichaka cha kujitafutia fedha.

Mwishoni mwa Ibada, Baba Mtakatifu Francisko amewaongoza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, akawapatia Baraka kuu na kufunga kwa kusali Sala ya Malkia wa Mbingu, inayotumiwa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha Pasaka.

SALA YA MALKIA WA MBINGU

Malkia wa mbingu, furahi, Aleluya.

Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.

Amefufuka alivyosema, Aleluya.

Utuombee kwa Mungu, Aleluya.

Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Aleluya.

Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.

TUOMBE. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA MALKIA WA MBINGU KWA LUGHA YA KILATINI: Regina Caeli

Regína caeli laetáre, allelúia.

Quia quem merúisti portáre, allelúia.

Resurréxit, sicut dixit, allelúia.

Ora pro nobis Deum, allelúia.

Gaude et laetáre, Virgo María, allelúia.

Quia surréxit Dominus vere, allelúia.

Orémus: Deus, qui per resurrectiónem Filii tui Dómini nostri Iesu Christi mundum laetificáre dignátus es, praesta, quǽsumus, ut per eius Genetrícem Virginem Maríam perpétuae capiámus gáudia vitae. Per Christum Dóminum nostrum. Amen.

Papa: Watawa
09 May 2020, 13:13
Soma yote >