Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika maadhimisho ya Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema amewakumbuka na kuwaombea Mapadre na Madaktari waliosadaka maisha yao kwa ajili ya waathirika wa COVID-19. Papa Francisko katika maadhimisho ya Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema amewakumbuka na kuwaombea Mapadre na Madaktari waliosadaka maisha yao kwa ajili ya waathirika wa COVID-19. 

Papa amewaombea Mapadre na Madaktari waliofariki kwa Corona

Ni muhimu kwa wanasayansi na watafiti kuunganisha nguvu zao za kisayansi katika ukweli na uwazi ili hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa iweze kupata chanjo na tiba dhidi ya ugonjwa wa Corona, COVID-19. Ni muhimu ikiwa kama, dawa, vifaa tiba na teknolojia muhimu katika mapambano haya itaweza kuwafikia watu walioambukizwa na ugonjwa wa Corona sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka inajulikana pia kuwa ni Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema sanjari na maadhimisho ya Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya kwa Mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu: “Jipeni Moyo Ni Mimi Msiogope: Maneno ya Miito”: Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa. (Rej. Mt.14:22-33). Baba Mtakatifu, Jumapili tarehe 3 Mei 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican kwa kuwakumbuka na kuwaombea Mapadre wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa: Neno, Sakramenti na Ushuhuda wa maisha na wito wa Kipadre.

Tangu kuzuka kwa Janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, zaidi ya Mapadre 100 wamefariki dunia nchini Italia. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii pia kuwaombea madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya wanayosadaka maisha yao kwa ajili ya kulinda na kudumisha Injili ya uhai. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna madaktari 154 waliopoteza maisha nchini Italia kutokana na ugonjwa wa Corona, COVID-19. Kwa muda wa siku 50, Baba Mtakatifu ameendelea kusali kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, kama kielelezo cha upendo na mshikamano kwa wale wote wanaoathirika, kuteseka, kuugua na hatimaye, kufariki dunia kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni mfano bora kutoka kwa Mapadre na Madktari wanaosadaka maisha yao kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka: Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 2: 14, 36-41; Somo la Pili kutoka katika Waraka 1 Pet. 2: 20-25 na Injili kama ilivyoandikwa na Yohane 10:1-10. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu alizichukua dhambi za binadamu katika mwili wake juu ya Msalaba, ili wakiwa wafu kwa mambo ya dhambi, wawe pia hai kwa mambo ya haki na kwa kupigwa kwake, wao wameponywa. Kristo Yesu ndiye mchungaji aliyekuja kuwaokoa kondoo wake. Ni mchungaji mwema anayewaongoza kondoo wake kwenye malisho ya kijani kibichi na kuwanywesha kando ya mto wa maji ya utulivu. Kristo Yesu ni mchungaji mwema na Mlango wa kondoo, wale wote waliokwea zizini bila kupitia Mlango wa kondoo ni wevi na wanyang’anyi.

Baba Mtakatifu anasema, katika maisha na historia ya Kanisa wamekuwepo wachungaji wa namna hii, kwani hawa ni “wachungaji feki” waliojikita katika siasa, mali na fedha” na matokeo yake, kondoo wakatawanyika na kusambaratika kumtafuta Mwenyezi Mungu. Mchungaji mwema anayo sanaa na kipaji cha kusikiliza kwa makini, anawaongoza kondoo wake na kuwahudumia kwa huruma na upendo. Kwa upande wake, kondoo wanamwamini na kujiaminisha kwa Mchungaji mwema. Kristo Yesu ndiye kielelezo na mfano wa Mchungaji mwema! Kristo Yesu aliteswa na kufa Msalabani, lakini aliyakubali mateso yote haya kwa unyenyekevu mkuu. Mchungaji mwema daima anajipambanua kwa fadhila ya unyenyekevu na wema unaomwezesha kuwa karibu pamoja na kondoo wake. Mchungaji mwema anawafahamu na kuwaita kondoo wake kwa majina. Kwa kondoo aliyepotelea nyikani, anamtafuta kwa udi na uvumba na anapompata anamrudisha zizini. Kristo Yesu mchungaji mwema ni kielelezo makini cha wema, upole na unyenyekevu. Haya ndiyo matamanio ya Kristo Yesu kwa Kanisa lake, ili kweli liweze kuvishwa fadhili hizi katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Jumapili ya Mchungaji mwema ni jumapili njema inayosimikwa katika amani na unyenyekevu kwa sababu Kristo Yesu mchungaji mwema, anajibidiisha kuwahudumia kondoo wake!

Mwishoni mwa Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko amewaongoza watu wa Mungu kusali Sala ya Malkia wa Mbingu.

SALA YA MALKIA WA MBINGU

Malkia wa mbingu, furahi, Aleluya.

Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.

Amefufuka alivyosema, Aleluya.

Utuombee kwa Mungu, Aleluya.

Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Aleluya.

Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.

TUOMBE. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

Papa: Mahubiri
03 May 2020, 13:30
Soma yote >