Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, wasanii wanatangaza na kushuhudia uzuri wa Injili kwa njia ya sanaa za maonesho! Papa Francisko asema, wasanii wanatangaza na kushuhudia uzuri wa Injili kwa njia ya sanaa za maonesho! 

Papa: Wasanii wanatangaza na kushuhudia uzuri wa Injili!

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 7 Mei 2020 ametolea nia ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wasanii wa sanaa za maonesho. Hawa ni watu muhimu sana wanaowasaidia waamini kutambua uzuri wa Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu anasema, hivi karibuni amepokea ujumbe kutoka kwa wasanii ndiyo maana ameamua kuwakumbuka kwa mara nyingine tena! Wasanii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 7 Mei 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican na kutolea nia ya Ibada hii kwa ajili ya wasanii wa sanaa za maonesho. Hawa ni watu muhimu sana wanaowasaidia waamini kutambua uzuri wa Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu anasema, hivi karibuni amepokea ujumbe kutoka kwa wasanii na hivyo kuwakumbuka kwa mara nyingine tena katika Ibada ya Misa Takatifu. Liturujia ya Neno la Mungu ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume Sura 13: 13-25 na Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane Sura 13: 16-20. Somo la Kwanza ni safari ya Mtume Paulo na wenzake huko Pisidia na hotuba aliyoitoa kwenye Sinagogi siku ya sabato, kwa kuelezea kwa ufupi historia ya Waisraeli kama taifa teule la Mungu alilolikomboa kwa mkono wenye nguvu kutoka utumwani Misri, akawaongoza jangwani kwa muda wa miaka arobaini.

Baadaye akawapatia waamuzi zamani za Nabii Samweli. Na walipoomba Mfalme, Mwenyezi Mungu akawapatia Sauli na hatimaye Mfalme Daudi. Mtakatifu Yohane Mbatizaji akatangaza na kushuhudia ujio wa Kristo Yesu, Masiha na Mkombozi wa Ulimwengu. Mtakatifu Paulo alitumia fursa hii kutangaza historia ya ukombozi inayopata utimilifu wake kwa Kristo Yesu kama kielelezo cha historia na ahadi ya taifa teule la Mungu. Mwenyezi Mungu katika historia nzima ya wokovu ameamua kuambatana na watu wake hatua kwa hatua, tangu kwa Ibrahamu, Baba wa imani hadi kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Ukristo una historia na mafundisho yake kama ahadi ya Mungu inayofumbatwa katika Agano kati ya Mungu na binadamu kwa sababu kwa upendeleo wake mwenyewe, amewachagua Waisraeli kuwa taifa lake teule. Kumbe, Kanisa lina kanuni maadili na utu wema, lakini pia ni watu walioteuliwa kutangaza na kushuhudia ukweli.

Ukristo unasimikwa katika historia ya watu walioteuliwa na Mwenyezi Mungu bila hata mastahili yao. Wakristo wa kweli anasema Baba Mtakatifu wanatambua kwamba, wao ni sehemu na urithi wa taifa teule la Mungu. Mafundisho tanzu ya imani, kanuni maadili na utu wema lazima yafumbatwe katika uelewa kwamba, Wakristo ni sehemu ya taifa teule la Mungu linalopata chimbuko lake kutoka katika ukoo wa Ibrahimu na kwamba, Kristo Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ahadi ya Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii, historia nzima ya wokovu inasimikwa katika matumaini, changamoto na mwaliko kwa waamini kutangaza historia yao ya wokovu, kwa kuwa na kumbukumbu angavu kwamba, wao ni watu wateule wa Mungu, historia ambayo inafikia kilele chake kwa Kristo Yesu.

Katika muktadha wa mazingira kama haya, historia ya wokovu imeweza kuandikwa na watu wengi, kati yao wamo wadhambi, watakatifu na watu wa kawaida tu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, hatari kubwa iliyoko mbele ya Wakristo ni kukosa kumbukumbu hai ya utambulisho wao kama ni wateule wa Mungu. Utambulisho huu unapokosekana na matokeo yake ni kuibuka kwa mifumo yenye mielekeo potofu kuhusu mafundisho tanzu ya Kanisa; kanuni maadili na utu wema pamoja na baadhi ya waamini kujiona kuwa wao ni bora zaidi kuliko wengine. Utambulisho wa taifa teule ni muhimu sana, kwa sababu hili ni taifa linalotembea kwa kuongozwa na ahadi ya Mungu; taifa ambalo limeweka agano na Mwenyezi Mungu, hata kama taifa linashindwa kua aminifu mbele ya Mungu, lakini Mwenyezi Mungu kwa upande wake, anaendelea daima kuwa mwaminifu. Hata kama taifa linashindwa kutekeleza ahadi za Mungu, lakini lina utambuzi thabiti kwamba, limeteuliwa.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili awakirimie utambuzi kwamba, waoni taifa teule la Mungu kama alivyofanya Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificat” na Zakaria katika wimbo wake wa Kinabii “Benedictus”. Hawa ni watu waliotambua kwamba, wao ni sehemu ya watu wateule wa Mungu hata kama kuna wakati wamekengeuka na kwenda kinyume cha Sheria ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko amewaongoza waamini Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, akawapatia Baraka kuu na kufunga kwa kusali Sala ya Malkia wa Mbingu, inayotumiwa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha Pasaka.

SALA YA MALKIA WA MBINGU

Malkia wa mbingu, furahi, Aleluya.

Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.

Amefufuka alivyosema, Aleluya.

Utuombee kwa Mungu, Aleluya.

Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Aleluya.

Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.

TUOMBE. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA MALKIA WA MBINGU KWA LUGHA YA KILATINI: Regina Caeli

Regína caeli laetáre, allelúia.

Quia quem merúisti portáre, allelúia.

Resurréxit, sicut dixit, allelúia.

Ora pro nobis Deum, allelúia.

Gaude et laetáre, Virgo María, allelúia.

Quia surréxit Dominus vere, allelúia.

Orémus: Deus, qui per resurrectiónem Filii tui Dómini nostri Iesu Christi mundum laetificáre dignátus es, praesta, quǽsumus, ut per eius Genetrícem Virginem Maríam perpétuae capiámus gáudia vitae. Per Christum Dóminum nostrum. Amen.

Papa: wasanii

 

07 May 2020, 13:29
Soma yote >