Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawataka waandishi wa habari kuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa ukweli katika jamii! Baba Mtakatifu Francisko anawataka waandishi wa habari kuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa ukweli katika jamii!  (AFP or licensors)

Waandishi wa Habari: Mashuhuda na Wahudumu wa Injili ya Ukweli

Papa Francisko amewakumbuka na kuwaombea wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, ili daima wajitahidi kuwa ni vyombo, mashuhuda na wahudumu wa ukweli. Katika kipindi hiki cha Janga la maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii wamo hatarini kuambukizwa Virusi vya Corona!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linatambua, linaheshimu na kuthamini kazi inayotekelezwa na wadau wa tasnia ya habari, hata pale, wanapotia kidole kwenye madonda ya maisha na utume wa Kanisa. Hii ni huduma muhimu inayosaidia mchakato wa kutafuta ukweli, unaowaweka watu huru na kwamba, daima Kanisa litaendelea kuwa upande wa wadau wa tasnia ya mawasiliano, kwani linatambua uhuru wa vyombo vya habari! Hii ni dhamana inayowajibisha katika huduma inayotolewa kwa maneno au kwa picha pamoja na yale yote wanayoshirikisha katika mitandao ya kijamii. Changamoto endelevu ni kutambua kuwa, kila mtu anawajibika mbele ya mambo mabaya na mazuri yanayotendeka ulimwenguni na kwamba, tabia na mwenendo wa maisha una athari zake hata kwa watu wengine ndani ya jamii.

Hii ni changamoto kwa wadau wa tasnia ya habari kuhakikisha kwamba, wanatenda kadiri ya ukweli na haki, ili mawasiliano yaweze kuwa ni nyenzo ya ujenzi na wala siyo ya uharibifu; chombo cha kuwakutanisha watu na wala si cha kuwasambaratisha; jukwaa la majadiliano ili kutoa dira na mwelekeo sahihi wa maisha na wala si mazungumzo yanayotawaliwa na mtu mmoja. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mawasiliano yawe ni dira, inayowasaidia watu kuelewana, ili waweze kutembea kwa pamoja katika misingi ya amani badala ya kupandikiza chuki; vyombo vya mawasiliano viwe ni sauti ya wanyonge na kamwe si kipaza sauti kwa wale wanaopiga kelele zaidi! Wadau wa tasnia ya habari wanapaswa kujivika unyenyekevu katika maisha yao ya kiroho na kitaaluma, ili kuboresha weledi, kumbu kumbu za kihistoria, udadisi, uwezo wa kupembua mambo kiyakinifu; kwa kuuliza maswali sahihi na hatimaye, kuweza kutoa muhtasari wake kwa haraka!

Baba Mtakatifu, Jumatano, tarehe 6 Mei 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican na kutolea nia ya Ibada hii kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, ili daima wajitahidi kuwa ni vyombo, mashuhuda na wahudumu wa ukweli. Katika kipindi hiki cha Janga la maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii wamo hatarini kuambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19. Ni watu wanaojitoa bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, watu wanapata habari kwa yale mambo msingi yanayoendelea kujiri sehemu mbali mbali za dunia!

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumatano: Somo la kwanza ni kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume: 12: 24; 13:5 na Injili kama ilivyoandikwa na Yohane 12: 44-50. Katika sehemu hii ya Injili inaonesha masharti ya imani ya kweli. Kristo Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba, mtu anayemwamini yeye anamwamini pia hata yule aliyempeleka! Mtu anayemtazama Kristo Yesu, anamtaza hata yule aliyempeleka. Anasema amekuja ulimwenguni ili awe ni nuru ya ulimwengu, ili kila mtu anayemwamini asikae gizani. Kila mtu anayesikia maneno ya Kristo na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yake hatakaa gizani kamwe. Lakini kwa yule atakayeyasikia maneno yake na wala asiyashike, Kristo Yesu hawezi kumhukumu, kwa maana hakuja ili kuhukumu ulimwengu, ila auokoe ulimwengu. Mtu anayemkataa Yesu na kutokubali maneno yake, siku ya mwisho atahukumiwa na neno hilo.

Baba Mtakatifu anasema, hapa Kristo Yesu anaonesha ule umoja na mshikamano uliopo katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kristo Yesu ametumwa na Baba yake wa mbinguni kama nuru inayouangaza ulimwengu, ili wale wanaomwamini na kuyamwilisha maneno yake, waweze kutembea katika mwanga na uzima wa milele. Hawa ndio wale watu waliokuwa wanatembea katika giza lakini sasa anasema Nabii Isaya nuru ya Bwana imewazukia! Mitume wa Yesu pia wamepewa dhamana ya kupeleka nuru ya Kristo Yesu ulimwenguni kote, ili kulifukuzia mbali giza la ulimwengu. Kwa bahati mbaya, nuru ilikuja ulimwenguni lakini wale walioko wake, wakaikataa nuru na kuendelea kutembea gizani walimozoea. Hii ni kwa sababu wao ni watumwa wa giza! Kristo Yesu anaendelea kuwaangaza walimwengu na kuwapatia nuru yake ili waweze kuyaona mambo na ukweli katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa alibahatika kukutana na Mwanga wa Kristo Mfufuka alipokuwa njiani kwenda Dameski. Kwa muda wa siku tatu, akawa hawezi kuona, kula wala kunywa. Alipobatizwa na kujazwa na Roho Mtakatifu, akaanza kuona tena. Ubatizo katika Kanisa la Mwanzo ulijulikana kama “Mwangaza” kwa sababu ulikuwa unatoa mwanga wa kuwaangazia njia. Ndiyo maana hata leo hii Wakristo wanapobatizwa wanapewa Mshumaa wa Pasaka, kielelezo cha mwanga angavu wa Kristo Mfufuka! Bila mwanga, ni rahisi sana kutekeleza na kuanguka dhambini. Ndiyo maana Mwinjili Mathayo anasisitizia umuhimu wa mwanga katika maisha ya mwamini. Hii ni changamoto ya kufanya wongofu kutoka katika giza na kuanza kuambata mwanga wa Kristo Mfufuka unaomwezesha mwamini kuona na kutambua ndani mwake mizizi ya dhambi, ubaya wa moyo na tabia ya kutaka kujikweza kupita kiasi.

Haya ni mambo makuu yanayomfanya mwamini kutoweza kuuona mwanga. Baba Mtakatifu anasema hata katika maisha ya kiroho kuna mafia wa ndani na wale wa kiroho. Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia mwanga wa kuweza kuona undani wa uhalisia wa maisha yao ya kila siku katika nyanja na ngazi mbali mbali za maisha. Ili kufikia hatua hii kuna haja ya kujenga ari na moyo wa ujasiri ili kuona giza la mioyo yao na hatimaye, kuruhusu mwanga wa Kristo Mfufuka uweze kuingia na kuwaokoa. Hakuna sababu ya kuogopa mwanga wa Kristo Mfufuka! Mwishoni mwa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Papa Francisko amewaongoza waamini Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, akawapatia Baraka kuu na kufunga kwa kusali Sala ya Malkia wa Mbingu, inayotumiwa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha Pasaka.

SALA YA MALKIA WA MBINGU

Malkia wa mbingu, furahi, Aleluya.

Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.

Amefufuka alivyosema, Aleluya.

Utuombee kwa Mungu, Aleluya.

Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Aleluya.

Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.

TUOMBE. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA MALKIA WA MBINGU KWA LUGHA YA KILATINI: Regina Caeli

Regína caeli laetáre, allelúia.

Quia quem merúisti portáre, allelúia.

Resurréxit, sicut dixit, allelúia.

Ora pro nobis Deum, allelúia.

Gaude et laetáre, Virgo María, allelúia.

Quia surréxit Dominus vere, allelúia.

Orémus: Deus, qui per resurrectiónem Filii tui Dómini nostri Iesu Christi mundum laetificáre dignátus es, praesta, quǽsumus, ut per eius Genetrícem Virginem Maríam perpétuae capiámus gáudia vitae. Per Christum Dóminum nostrum. Amen.

Papa: Waandishi wa Habari
06 May 2020, 14:01
Soma yote >