Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 4 Mei 2020 amesali ili kuombea umoja wa Kanisa; amani, utulivu na ubunifu kwa familia katika kipindi hiki cha kuwekwa karantini. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 4 Mei 2020 amesali ili kuombea umoja wa Kanisa; amani, utulivu na ubunifu kwa familia katika kipindi hiki cha kuwekwa karantini.  (ANSA)

Papa Francisko: Umoja wa Kanisa; Amani na Utulivu kwa familia!

Papa Francisko ameombea umoja na mshikamano wa Kanisa; amani na utulivu wa ndani kwenye familia hasa katika kipindi hiki ambacho watu wengi bado wamewekwa karantini kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu ameziombea familia ili ziweze kudumu katika amani na utulivu wa ndani na kuendelea kujikita katika kipaji cha ubunifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, “Katika hili upendo wa Mungu ulionekana kwetu, kwamba Mungu Baba amemtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, auchukue mwili, na kwa njia ya ukombozi awahuishe upya wanadamu na kuwakusanya wawe wamoja. Naye, kabla ya kujitoa kama kafara safi juu ya madhabahu ya Msalaba, aliwaombea wamwaminio kwa Baba akisema: “Wote wawe na umoja, kama wewe Baba ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiye uliyenituma” (Yn 17:21). Tena akaiweka katika Kanisa lake Sakramenti ya ajabu ya Ekaristi Takatifu, ambayo ni ishara na chemchemi ya umoja wa Kanisa. Na akawapa wafuasi wake amri mpya ya kupendana, akawaahidia Roho Mfariji, aliye Mungu mtia uzima, ili akae nao daima.

Kristo Yesu alisali na kuwaombea wote ambao watamwamini kwa sababu ya Neno la Mitume wake, wawe na umoja kama wao walivyo wamoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Haya ni maneno ambayo Wakristo kwa miaka mingi wamekuwa wakiliyasikiliza, lakini bado hawajayapatia kipaumbele cha kutosha. Utengano ni kati ya madonda makuu ambayo Kristo Yesu ameyagharimia kwa Damu yake Azizi. Yesu alisali kwa ajili ya umoja na mshikamano wa watu wa Mungu; Umoja wa Kanisa dhidi ya kinzani, magovi, vita na wivu ambao unajionesha kwa namna ya pekee, katika maisha ya familia ya watu wa Mungu. Hiki ni kishawishi kikubwa na kinapaswa kushindwa kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ujenzi wa umoja na mshikamano ili wote waweze kuwa wamoja, changamoto endelevu kwa Wakristo wote.

Kamwe Wakristo wasikubali kutumbukizwa kwenye dimbwi la utengano, bali wajitahidi kutafuta, kujenga na kudumisha umoja, msamaha na upatanisho. Umoja wa Wakristo unapata chimbuko lake katika neema, kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu, ili kutenda na hivyo, kuwasaidia wakristo kubaki wakiwa wameungana na Kristo Yesu, tayari kushiriki naye katika maisha ya uzima wa milele, ili kutafakari pamoja naye, ule utukufu wa Baba yake wa mbinguni. Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 4 Mei 2020, ameombea umoja na mshikamano wa Kanisa; amani na utulivu wa ndani kwenye familia hasa katika kipindi hiki ambacho watu wengi bado wamewekwa karantini kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu ameziombea familia ili ziweze kudumu katika amani na utulivu wa ndani; kwa kuendelea kujikita katika kipaji cha ubunifu na uvumilivu.

Liturujia ya Neno la Mungu kwa Siku ya Jumatatu, ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 11: 1-18, Injili ya Yohane 10: 1-10. Baba Mtakatifu amefanya rejea kwenye Simulizi la Mtakatifu Petro huko Yerusalemu baada ya kushutumiwa kwamba aliingia kwenye nyumba ya watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao! Alisimulia jinsi ambavyo Roho Mtakatifu aliwashukia kama alivyowashukia Mitume kwenye Sikukuu ya Pentekoste na watu hao wakabatizwa kwa Roho Mtakatifu. Huu ni mwelekeo ambao upo ndani ya Kanisa hata leo hii, kwani kuna watu wanaojikinai kuwa wao ni watakatifu na wengine ni wadhambi, ambao tayari wamekwisha laaniwa na kuhukumiwa. Huu ni ugonjwa wa maisha ya kiroho ndani ya Kanisa unaoibuliwa na itikadi pamoja na “vyama vya kidini”. Ni mwelekeo potofu wa kutafsiri Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Matokeo yake, watu kama hawa wanamezwa na malimwengu na kuwa ni chanzo cha kinzani na utengano ndani ya Kanisa.

Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza, ili kuisikiliza ile sauti ya Kristo Mchungaji mmoja, ili wote wawe wamoja. Kristo Yesu ameteswa, akafa na kufufuka kwa ajili ya watu wote wa Mungu. Kristo Yesu ndiye Mkombozi wa Ulimwengu. Kumbe, kuna haja ya kuondokana na mawazo pamoja na vitendo vyote vile vinavyoweza kuligawa Kanisa. Jambo la msingi ni kudumisha umoja katika utofauti wa Kanisa. Kristo Yesu ndiye mchungaji mkuu wa Kondoo wake, awasaidie Wakristo kuondokana na saikolojia inayowatumbukiza katika kinzani, migogoro na utengano na hatimaye, awasaidie kuona kwamba, wao ni ndugu wamoja katika Kristo Yesu! Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu yamekamilishwa kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akawapatia Baraka kuu ya Ekaristi pamoja na kusali Sala ya Malkia wa Mbingu.

SALA YA MALKIA WA MBINGU

Malkia wa mbingu, furahi, Aleluya.

Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.

Amefufuka alivyosema, Aleluya.

Utuombee kwa Mungu, Aleluya.

Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Aleluya.

Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.

TUOMBE. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

Sala ya Malkia wa Mbingu kwa Lugha ya Kilatini: Regina Caeli

Regína caeli laetáre, allelúia.

Quia quem merúisti portáre, allelúia.

Resurréxit, sicut dixit, allelúia.

Ora pro nobis Deum, allelúia.

Gaude et laetáre, Virgo María, allelúia.

 Quia surréxit Dominus vere, allelúia.

Orémus.

 Deus, qui per resurrectiónem Filii tui Dómini nostri Iesu Christi mundum laetificáre dignátus es, praesta, quǽsumus, ut per eius Genetrícem Virginem Maríam perpétuae capiámus gáudia vitae. Per Christum Dóminum nostrum. Amen.

Papa: Umoja wa Kanisa

 

04 May 2020, 13:38
Soma yote >