Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 5 Mei 2020 amewakumbuka na kuwaombea Marehemu Wote waliofariki dunia mwaka 2020 kwa ugonjwa wa Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 5 Mei 2020 amewakumbuka na kuwaombea Marehemu Wote waliofariki dunia mwaka 2020 kwa ugonjwa wa Corona, COVID-19. 

Papa Francisko Amewaombea Marehemu Wote wa COVID-19

Kimsingi mazingira ya watu waliofariki dunia kwa ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19, wamefariki katika mazingira magumu na hata wakati mwingine kushindwa kupewa maziko anayostahili binadamu. Baba Mtakatifu anawaombea wote hawa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili sasa baada ya mateso na mahangaiko yao, waweze kupokelewa kwenye makao ya milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 5 Mei 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, sehemu mbali mbali za dunia! Wengi wao ni wale ambao wameitupa mkono dunia katika hali ya upweke na majonzi mazito! Hata wakati mwingine, wamefariki dunia bila ya kuonja ukaribu na upendo kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki; au kusindikizwa kwenye safari yao ya mwisho hapa duniani! Kimsingi mazingira ya watu waliofariki dunia kwa ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19, wamefariki katika mazingira magumu na hata wakati mwingine kushindwa kupewa maziko anayostahili binadamu. Baba Mtakatifu anawaombea wote hawa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili sasa baada ya mateso na mahangaiko yao, waweze kupokelewa kwenye makao ya milele, huko mbinguni!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amefanya rejea katika Liturujia ya Neno la Mungu: Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume Sura ya 11: 19-26 na Injili kama ilivyoandikwa na Yohane Sura ya 10: 22-30. Hii ni sehemu ya Injili inayohusu tangazo rasmi na mashitaka ya kukufuru. Wayahudi walimtaka Yesu kutangaza wazi wasi ikiwa kama ndiye aliyekuwa Kristo, Mpakwa wa Bwana! Lakini Yesu aliwajibu kwamba, amekwisha kuwaambia, lakini wao hawakusadiki. Kazi alizokuwa anazifanya kwa jina la Baba yake wa mbinguni ndizo zilizokuwa zinamshuhudia. Wao hawakumsadiki kwa sababu hawakuwa ni miongoni mwa kondoo wake. Kwa sababu kondoo wake wanaisikia sauti yake, anawajua nao wanamfuata.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujiuliza ikiwa kama, hata wao katika mazingira yao ya nyakati hizi wanamwamini Kristo Yesu  au wamegeuka kiasi cha kuwa ni kizingiti katika imani yao kwa Kristo Yesu. Uchu wa mali na utajiri ni kati ya vizingiti vinavyokwamisha waamini kuweza kuwa ni wafuasi amini wa Kristo Yesu. Wengi wamejikuta wakiwa ni watumwa wa mali na fedha, kiasi cha kuwa ni kizingiti cha kushindwa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Si rahisi sana kuwatumikia mabwana wawili, Mungu na mali. Kizingiti cha pili kinachowakwamisha waamini kusonga mbele, ili kumfahamu na hatimaye, kuwa ni wafuasi amini wa Kristo Yesu ni ugumu wa mioyo na tafsiri potofu ya Sheria, Kanuni na taratibu za Kanisa kama ilivyokuwa kwa Waandishi na Mafarisayo. Uaminifu kwa Mwenyezi Mungu ni karama na zawadi, lakini ugumu wa moyo ni ngao ya mtu kutaka kujilinda binafsi.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, hekima na busara ya Kristo inawafanya kuwa huru zaidi. Kuna baadhi ya viongozi wa Kanisa wanaowajengea waamini wao ugumu wa mioyo, kiasi hata cha kushindwa kuweza kuingia katika Mlango wa Kristo Yesu. Kizingiti cha tatu anasema Baba Mtakatifu ni wivu usiokuwa na maendeleo unaowakwamisha watu kusonga mbele na kuwaacha wakiwa vuguvugu katika imani. Jambo jingine ni matumizi mabaya ya madaraka na baadhi ya viongozi wa Kanisa kudhani kwamba, wanafahamu kila jambo, kiasi hata cha kuwaondolea waamini imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mwishoni, tatizo la baadhi ya waamini kumezwa na malimwengu kwa sababu ni kikwazo kikubwa katika neema ya kufahamu uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja na waja wake. Mambo yote haya yanawaondolea watu uhuru, kwani si rahisi sana kuweza kumfuasa Kristo bila ya uhuru na utashi kamili. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, uhuru pia una mipaka yake!

Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu amewataka waamini kumwomba Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwaangazia kutoka katika undani wa maisha yao, ili kuangalia ikiwa kama kweli wako huru kumwendea Kristo Yesu na hatimaye, kuwa ni kondoo wa malisho yake. Mwishoni mwa Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu amewaongoza waamini Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, akawapatia Baraka kuu na kufunga kwa kusali Sala ya Malkia wa Mbingu, inayotumiwa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha Pasaka.

SALA YA MALKIA WA MBINGU

Malkia wa mbingu, furahi, Aleluya.

Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.

Amefufuka alivyosema, Aleluya.

Utuombee kwa Mungu, Aleluya.

Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Aleluya.

Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.

TUOMBE. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

Sala ya Malkia wa Mbingu kwa Lugha ya Kilatini: Regina Caeli

Regína caeli laetáre, allelúia.

Quia quem merúisti portáre, allelúia.

Resurréxit, sicut dixit, allelúia.

Ora pro nobis Deum, allelúia.

Gaude et laetáre, Virgo María, allelúia.

Quia surréxit Dominus vere, allelúia.

Orémus: Deus, qui per resurrectiónem Filii tui Dómini nostri Iesu Christi mundum laetificáre dignátus es, praesta, quǽsumus, ut per eius Genetrícem Virginem Maríam perpétuae capiámus gáudia vitae. Per Christum Dóminum nostrum. Amen.

Papa: COVID-19

 

05 May 2020, 13:58
Soma yote >