Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumtafakari Bikira Maria, Mama wa Mateso, ili kumtolea Mungu shukrani kwa B.Maria kukubali kuwa ni Mama wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumtafakari Bikira Maria, Mama wa Mateso, ili kumtolea Mungu shukrani kwa B.Maria kukubali kuwa ni Mama wa Mungu. 

Papa Francisko: Bikira Maria Mama wa Mateso, Utuombee!

Baba Mtakatifu Francisko amewaweka watu wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mateso, anayekumbukwa na Mama Kanisa, Ijumaa inayotangulia Jumapili ya Matawi. Papa anawaalika waamini kutafakari kuhusu mateso ya Bikira Maria katika hija ya maisha na utume wake na hivyo kumshukuru, kwa sababu alikubali kutikia wito wa kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wimbi kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 sehemu mbali mbali za dunia, ni janga ambalo linaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika dimbwi la umaskini, njaa na magonjwa. Watu wengi kwa sasa wana hofu ya fursa za ajira kwa siku za usoni. Ni wakati muafaka kwa watu wa Mungu kujipanga kikamilifu ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa kuweka sera na mikakati itakayowasaidia watu kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 3 Aprili 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.

Baba Mtakatifu amesoma Antifona ya mwanzo kutoka katika Zaburi ya 30:1 isemayo: “Nimekumbilia Wewe, Bwana, nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, unitegee sikio lako, uniokoe hima. Uwe kwangu mwamba wa nguvu, nyumba yenye maboma ya kunikoa”. Baba Mtakatifu ametolea nia ya Ibada ya Misa Takatifu kwa wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili kutafuta suluhu ya kuokoa watu walioathirika kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu amewaweka watu wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mateso, anayekumbukwa na Mama Kanisa, Ijumaa inayotangulia Jumapili ya Matawi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari kuhusu mateso aliyokumbana nayo Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa katika hija ya maisha yake hapa duniani na hivyo kumshukuru, kwa sababu alikubali kutikia wito wa kuwa ni Mama wa Mungu.

Waamini katika Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mateso wanayakumbuka mateso ambayo Bikira Maria aliyapitia katika maisha na utume wake. Kristo Yesu alipotolewa Hekaluni, Mzee Simeoni alitabiri kwamba, upanga utaingia moyoni mwa Bikira Maria, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi! Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu pamoja na Mtoto Yesu, walilazimika kukimbilia ugenini, huko Misri ili kusalimisha maisha ya Mtoto Yesu. Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu waliingiwa na wasi wasi na hofu kubwa, wakaanza kumtafuta Mtoto Yesu kwa muda wa siku tatu bila mafanikio na hatimaye, wakamkuta Yesu akiwa Hekaluni. Katika Njia ya Msalaba, Bikira Maria alikutana na Yesu, akamsindikiza hadi pale Mlimani Kalvari, chini ya Msalaba akashuhudia kifo chake! Wakamteremsha kutoka Msalabani na kumkabidhi Bikira Maria. Baada ya yote haya, Yesu akazikwa kaburini.

Kwa karne nyingi, waamini wamejenga na kukuza Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mateso. Baba Mtakatifu anasema, katika Sala ya Malaika wa Bwana, daima anamkumbuka Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Huyu ni Mama aliyejisadaka na kujitoa kwa ajili ya wengine kama ilivyokuwa kwenye arusi ya Kana ya Galilaya, akakubali kuwa ni Mama wa wote. Bikira Maria katika maisha na utume wake, akawa ni mwanafunzi mwaminifu wa Kristo Yesu, akajifunza kutoka kwake, na kumsindikiza katika maisha na utume wake. Akawasindikiza wanawake wachamungu waliovutwa na huduma ya Kristo Yesu katika maisha yao! Kuna wakati, Bikira Maria na ndugu zake, walidhani kwamba, “Yesu alikuwa amechanganyikiwa” wakaenda kumwona, lakini hawakupata nafasi! Bikira Maria akamfuata Mwanae wa pekee, hadi kudiriki kusimama chini ya Msalaba na kushuhudia jinsi ambavyo walimnyanyasa na kumdharirisha Yesu! Lakini, akaendelea kuwa jasiri kama Mama na hatimaye, Kristo Yesu akiwa chini ya Msalaba, akamkabidhi kwa yule Mwanafunzi aliyempenda na tangu wakati huo, akawa ni Mama wa waamini wote. Ni Mama aliyeshirikiana na kushikamana na Mitume wa Yesu katika kusali!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bikira Maria, aliendelea kuwa ni Mama na mwanafunzi hodari wa Kristo Yesu; mwaliko kwa waamini kumtafuta, ili kukimbilia ulinzi na tunza yake ya kimama. Maria ni Mama na Bikira, mfano hai wa utimilifu wa Kanisa. Hata Kanisa, kwa kuutazama utakatifu wa Bikira Maria, kwa kuiga upendo wake na kutimiza mapenzi ya Mungu, linakuwa pia ni Mama. Kwani kwa njia ya mahubiri na Sakramenti ya Ubatizo linazaa watoto waliotungwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na hivyo kuzaliwa kwa Mungu, kwa uzima mpya usiokufa! Kanisa ni Mama wa wote, watakatifu na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu. Kumbu kumbu ya Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Mateso iwe ni fursa kwa waamini kutafakari Fumbo la mateso katika maisha yao! Waguswe na mateso ya Bikira Maria katika maisha na utume wake, ili hatimaye, waweze kumtolea sifa na heshima kwa kukubali kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa.

Papa: Bikira Maria Mama wa Mateso.
03 April 2020, 12:46
Soma yote >