Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujenga na kudumisha utamaduni na sanaa ya kusikilizana kwa dhati ili kukuza na kudumisha amani, utulivu, upendo na mshikamano wa kifamilia. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujenga na kudumisha utamaduni na sanaa ya kusikilizana kwa dhati ili kukuza na kudumisha amani, utulivu, upendo na mshikamano wa kifamilia. 

Papa Francisko: Jengeni sanaa na utamaduni wa kusikilizana!

Papa Francisko anasema ukimya huu mpya unapaswa kutumiwa na watu wa Mungu kama kosa lenye heri, ili kujenga na kudumisha sanaa na utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili kuboresha misingi ya: utulivu na amani; umoja na upendo kati ya wanafamilia. Wamsikilize Roho Mtakatifu, kwa unyenyekevu mkuu na hivyo kuondokana na vishawishi vinavyobomoa misingi ya jumuiya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Sinodi ya Vijana kwa Mwaka 2018 wanasema, kuna haja ya kuwasikiliza kwa makini vijana wa kizazi kipya ili waweze kujitambua; kushirikiana nao kwa karibu kwa kutambua lugha wanazotumia, ili kuweza kuwafikishia Habari Njema ya matumaini. Viongozi wa Kanisa wajenge sanaa na utamaduni wa majadiliano na vijana katika ukweli na uwazi, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 21 Aprili 2020 amegusia madhara yanayoendelea kusababishwa na janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kiasi kwamba, watu wamejenga hofu, taharuki na kimya kikuu.

Ukimya huu mpya unapaswa kutumiwa na watu wa Mungu kama kosa lenye heri, ili kujenga na kudumisha sanaa na utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili kuboresha misingi ya: utulivu na amani;  umoja na upendo kati ya wanafamilia. Jambo la msingi kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanamsikiliza Roho Mtakatifu, kwa unyenyekevu mkuu na hivyo kuondokana na vishawishi vikuu vitatu vinayoporomosha tunu msingi za maisha ya kijumuiya yaani: Uchu wa fedha na mali; fahari, maisha ya starehe na anasa pamoja na umbea kwani kwa hakika wambea hawana bunge! Katika kipindi hiki kuna utulivu na kimya kikuu, kiasi kwamba, mtu anaweza kusikia kimya chenyewe. Huu ni mwelekeo mpya katika maisha na tabia ya watu wengi, lakini muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa sanaa na utamaduni wa kusikiliza kwa makini. Hii ni fadhila ambayo waamini na watu wenye mapenzi mema wanapaswa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia kadiri ya huruma na upendo wake!

Baba Mtakatifu Francisko katika Liturujia ya Neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume: Sura ya 4:32-37. Jumuiya ya waamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wakawa na vitu vyote shirika; Mitume wakajikita kutangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka. Kila mtu aliweza kupata mahitaji yake msingi bila wasi wasi wowote! Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ni mfano bora na ni matunda ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Ni Roho Mtakatifu anayewakirimia waja wake amani na utulivu wa ndani! Baadaye, “ndago” za utengano zikaanza kupandikizwa kati yao. Chanzo cha kwanza ni uchu wa fedha na mali na matokeo yake ni maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” kutengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Fedha ni chanzo kikuu kinachoweza kuigawa Jamii na Kanisa katika ujumla wake. Hata wakati mwingine, watu kukengeuka na kutopea kinyume cha Mafundisho ya Kanisa, si bure, ukiangalia kwa undani, hapo kuna fedha imetembezwa! Leo hii ni patashika nguo kuchanika anasema Baba Mtakatifu Francisko kutokana na wanafamilia kugombania mali ya urithi. Jambo la pili ni maisha ya fahari, starehe na anasa na baadhi ya watu kutaka “kujimwambafai” kuwa wao ni bora zaidi kuliko wengine. Jambo la tatu linaloweza kuigawa jumuiya ya waamini ni umbea, kazi kubwa inayofanywa na Shetani, Ibilisi kiasi hata cha kuwagawa watu. Roho Mtakatifu anawakirimia waja wake fursa na kuwapatia nafasi ya kuwaokoa kutokana na hatari zote hizi, zinazoweza kuwafanya wamezwe na malimwengu.

Kumbe, kuna haja kwa waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kugeuza jumuiya zao kuwa ni mahali pa amani na utulivu wa ndani! Baba Mtakatifu amehitimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Baraka Kuu ya Ekaristi Takatifu na hatimaye kusali Sala ya Malkia wa Mbingu inayotumika katika kipindi hiki cha Pasaka ya Bwana!

Papa: Ukimya

 

 

21 April 2020, 12:58
Soma yote >