Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika nia yake ya Misa tarehe 30 Machi 2020 amewakumbuka watu wote walioshikwa na taharuki, woga na wasi wasi ili Mungu anawajalie nguvu ya kusimama tena! Baba Mtakatifu Francisko katika nia yake ya Misa tarehe 30 Machi 2020 amewakumbuka watu wote walioshikwa na taharuki, woga na wasi wasi ili Mungu anawajalie nguvu ya kusimama tena!  (ANSA)

Papa Francisko awaombea watu walioshikwa na taharuki ya Corona

Papa Francisko ametolea nia ya Misa takatifu kwa ajili ya watu wote walioshikwa na taharuki kutokana na kuenea kwa kasi kubwa Virusi vya Corana, COVID-19. Papa anamwomba Mwenyezi Mungu awakirimie waja wake neema na baraka ya kuweza kusimama tena na kusonga mbele kwa imani na matumaini. Watu wa Mungu watoe kipaumbele cha kwanza kwa ustawi na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Antifona ya Mwaliko, Liturujia ya Neno la Mungu, Jumatatu ya V ya Kipindi cha Kwaresima inaonesha kwamba, mwaminifu mbele ya Mwenyezi Mungu kamwe hatashindwa! “Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa, maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi”. Zab. 55:2. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 30 Machi 2020, ametolea nia ya Misa takatifu kwa ajili ya watu wote walioshikwa na taharuki kutokana na kuenea kwa kasi kubwa kwa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corana, COVID-19. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu awakirimie waja wake neema na baraka ya kuweza kusimama tena na kusonga mbele kwa imani na matumaini. Watu wa Mungu watoe kipaumbele cha kwanza kwa ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amechambua kwa kina na mapana Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Nabii Danieli: 13:41-62 kuhusu habari za Susana Binti Helkia, aliyehukumiwa kuuwawa kutokana na hila za wazee wa Baraza waliokuwa wamebobea katika rushwa ya ngono dhidi ya wanawake wa Israeli. Mwenyezi Mungu akatenda kwa haki na kumwokoa Susana kutoka kwenye mikono ya wazee wenye hila. Katika Injili kama ilivyoandikwa na Yohane 8:12-20: Kristo Yesu anamwokoa mwanamke mzinifu dhidi ya Waandishi na Mafarisayo. Mzaburi 23:1- 6; katika Wimbo wa Kati kati kuhusu Mchungaji mwema anasema, Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu, katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafasi yangu na kuniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya, kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji… Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wanapotambua udhaifu wao wa kibinadamu kwamba, ni wadhambi, wawe na ujasiri wa kumshukuru Mungu na kwa imani na matumaini makubwa wakimbilie wema, huruma na upendo wake. Huu ndio uzoefu na mang’amuzi aliyoyapata Susana Binti Helkia. Mababa wa Kanisa wanaona ndani ya mwanamke huyu, Mama Kanisa Mtakatifu sana “Casta meretrix”, lakini mwenye watoto wadhambi. Wanawake wote wawili katika Liturujia ya Neno la Mungu walikata tamaa, lakini wakaendelea kujiaminisha mbele ya haki ya Mungu. Wazee wa Baraza waliteuliwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, haki ya Mungu inatendeka kwa kuwafundisha watu Sheria na Maagizo ya Mungu. Hawa ni wanasheria waliokuwa wamemezwa na rushwa na unafiki katika maisha yao. Lakini wema na huruma ya Mungu vikawaongoza. Wanawake wote wawili walidhalilishwa utu, heshima na haki zao msingi mbele ya umati mkubwa wa watu!

Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, akawaokoa na unafiki wa Wazee wa Baraza, Waandishi na Mafarisayo. Hawa ni watu waliosutwa kutoka katika undani wa dhamiri zao, kila mmoja akajikuta ana hatia mbele ya Mungu. Yesu akampatia yule mwanamke mzinifu muda wa kutubu na kuongoka katika hali ya ukimya, baadaye akamwonjesha wema na huruma ya Mungu kwa wale wote wanaotubu na kumwongokea. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, si rahisi sana kwa wala rushwa na wanafiki kutubu na kumwongokea Mungu. Watu wanapogundua hukumu ya haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu wanamshukuru na kumtukuza na kuendelea kujifunza kumwilisha ndani mwao huruma ya Mungu. Hii ni changamoto na mwaliko kwa kila mwamini kuchunguza dhamiri yake, kutubu na kumwongokea Mungu. Waamini wasione haya kuwa ni sehemu ya Kanisa, bali waone aibu kwa sababu ni wadhambi na wawe na ujasiri wa kukimbilia wema, huruma na msamaha katika maisha yao.

Mwishoni, mwa Ibada ya Misa Takatifu, amewaalika waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Waonje na kufarijika na upendo unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu; daima waendelee kujiachia na kujikabidhi mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili waguswe na upendo wa Mungu sasa na wakati wa kufa kwao.

Papa: Haki ya Mungu

 

30 March 2020, 16:01
Soma yote >